Dr Mathew Togolani Mndeme
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 201
- 809
Ndugu wana JamiiForum,
Leo waziri wa maliasli na Utalii, Mh Dkt Kigwangala, ameshirikisha umma kupitia anuani yake ya twitter mkakati wa kuvutia watalii kutoka nchi za kiafrika (a strategy for regional tourism). Kwa kifupi, mkakati huu umelenga kuzifikia na kuzivutia nchi zenye mapato makubwa zaidi kama inavyoonekana kwenye kiambatanisho.
Pamoja na uzuri wa wazo lake na timu yake, mimi ninaona mkakati huu sio muafaka (relevant) kwa muktadha wa “watalii” wanaowalenga. Kama ningepewa nafasi ya kuishauri wizara yake au serikali kwa ujumla juu ya namna ya kuvutia “watalii” toka nchi za kiafrika, ningeshauri tofauti na mkakati wao kwa maana kuu tatu: (i) nini cha kuvutia; (ii) nani wa kuvutia; (ii) namna ya kuvutia.
Naomba nifafanue:
- Duniani kote, kutalii ni anasa wafanyayo watu baada ya kujikidhi kwa mahitaji mengine ya msingi. Waafrika wanaosafiri kwenda kutalii nchi nyingine za Afrika kuona vivutio vya asili (ambavyo ndio mtaji wetu mkuu wa utalii) ni wachache sana kwa sababu waafrika walio wengi bado tunahangaika na mahitaji ya lazima.
- Hata hivyo, data zinaonesha waafrika wanasafiri kwa wingi sana kwenda nchi tajiri au zenye maendeleo makubwa kama watalii. Wachache kati yao wanakwenda kuona vivutio vya utalii lakini wengi wanakwenda kuona ukisasa (modernisation), kusoma shahada mbalimbali au mafunzo ya muda mfupi (educational tourism), na kutafuta huduma za matibabu ya magonjwa yasiyotibika kwenye nchi zao au kwa kua tu hawana imani nna kiwango cha utoaji huduma wanayohitaji (medical tourism).
- Hivyo, mkakati wa kuvutia watalii kutoka nchi za kiafrikahauwezi kufanikiwa ikiwa malengo ni kuwavutia kuona vivutio vya asili maana kwa wengi vitu hivi sio vipya kwao na hata kama ni vipya, kuviona sio kipaumbe. Mkakati wa kuvutia waafrika wenzentu kuja Tanzania unatakiwa kujielekeza kwenye “vivutio vya utalii” ambavyo waafrika wanavifuata kwenye nchi zilizoendelea. Hivyo ningeshauri yafutayo kama mkakati muafaka na wa muda mrefu:
- Tuboresha vyuo vikuu na taasisi zingine za kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi, ziwe za kisasa na kukidhi mahitaji ya elimu yanayotafutwa nje ya Afrika. Ukisasa uonekane kwenye miundombinu, rasilimali watu, huduma kwa mteja, na ubora wa elimu au mafunzo yanayotolewa.
- Tuwekeze kwenye huduma bora za afya. Tuwe na hospitali kubwa, bora, na zinazotoa huduma za afya ambazo waafrika wanakwenda kutafuta Asia, Ulaya na Marekani.
- Tuwekeze kwenye rasilimali watu tuwe na watalamu na watoa huduma waliobobea na wanaoongea kwa ufasaha lugha zinazotumiwa na waafrika walio wengi (Kiswahili, Kiarabu, Kingereza, Kifaransa, Kireno, Kiibo, Yoruba, Kizulu, nk). Pia, kuhakikisha wataalamu na watoa huduma kwenye sekta za kimkakati (elimu, afya, usafiri, nk) wana mitizamo sahihi ya huduma kwa mteja (attitude to delivering quality/good customer care services).
- Kiswahili ni mtaji mkubwa wa kiutamaduni tulionao kuliko mwingine wowote ule. Hivyo, tujenge taasisi kubwa na ya kisasa ya lugha ya Kiswahili (Tanzanian Centre for Kiswahili Studies) kwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu itakayomvutia kila mgeni anayetaka au kulazimika kujua Kiswahili. Hii ni pamoja na wageni wanaokuja kufanya kazi Tanzania, kulazimika kuelewa Kiswahili kwa kiwango fulani kama nchi nyingine zifanyavyo.
- Miradi yote ya kimkakati inayojengwa na serikali, ndani yake kuwe na mtizamo wa utalii. Miundombinu ya umeme wa maji, barabara, reli, umeme wa jua, umeme wa upepo, bandari, viwanja ya ndege na michezo, nk; ifanye kilichokusudiwa lakini pia iwe na mwonekano wa ukisasa na kuvutia.
- Tuboreshe mipango miji na kuwekeza kila nyumba au makazi yawe na anuani rasmi ya kudumu. Hii ina faida nyingi sana kihuduma, usalama, uwekezaji, nk.
- Tuwe na jeshi la polisi rafiki na la kisasa lililofunzwa kutoa huduma ya ulinzi, usalama na kuzuia uhalifu badala ya fikra za kuadhibu, kudhibiti, ubabe na kukomoa. Hali ya usalama wa ndani ya nchi, ni uhitaji mkubwa kwa mgeni.
- Kuwe na uwekezaji mkubwa wa rasilimali watu na utaalamu wa mifumo ya TEHAMA ili yote niliyoorodhesha hapo juu, yarahisishwe, kuboreshwa na kuwezeshwa na mifumo ya kisasa ya TEHAMA.
- Tuboresha vyuo vikuu na taasisi zingine za kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi, ziwe za kisasa na kukidhi mahitaji ya elimu yanayotafutwa nje ya Afrika. Ukisasa uonekane kwenye miundombinu, rasilimali watu, huduma kwa mteja, na ubora wa elimu au mafunzo yanayotolewa.
Badala ya kwenda kulipia ada au kutafuta matibabu kwa maelfu ya dola huko Asia, Ulaya au Marekani, na kutafuta visa kwa gharama kubwa na masharti magumu kama ya kwenda mbinguni, mwafrika toka Malawi, Zambia, Kongo, Burundi, Msumbiji, nk, atakuja kupata huduma hiyohiyo Arusha, Mwanza, Mbeya, Dar au Mtwara kwa nusu au robo ya gharama ya usafiri, malazi/makazi na ada husika.
Mwafrika huyu atajisikia salama zaidi kupata anachohtaji toka kwa waafrika wenzake. Kwa sehemu fulani, Kenya na Afrika Kusini wanapata watalii wengi toka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa njia hii hata kama sio mikakati wa kitaifa. Watu wanaamini zaidi shule na huduma za afya na Afrika Kusini. Maafisa wa Balazi wan chi nyingi na wa makampuni makubwa ya kigeni, hawatibiwi kwenye hospital zetu. Wanachota pesa nchi ila wakiumwa wanarushwa na ndege kwenda Nairobi au Afrika Kusini. Pia ndipo Watoto wao wanaposoma kwa wingi. Rwanda wanawekeza kwenye eneo hili kwa kasi. Tusipojiongeza hata sisi tusipojiongeza tutaanza kwenda kutafuta "baadhi ya huduma za kisasa" Kigali
Raia wa Kongo au Burundi anaweza asiwaze kuja kutazama Mlima Kilimanjaro lakini anaweza kuunza mali zote alizonazo aweze kusafiri kuja Muhimbili kutibiwa figo au moyo kama ana hakika na ubora wa huduma atakayoipata. Mzazi aliyeko Malawi anaweza asiwaze wala kutaka kujua habari za Ngorongoro, lakini anaweza kufanya liwezekanalo kumsafirisha mtoto wake kwenda UDSM kupata degree kama ana hakika atapata elimu ya kiwango na atasoma akiwa kwenye mazingira safi, salama, na yanayohakisi kiwango cha fedha atakacholipa.
Tutoke nje ya boksi la vivutio vya asili pekee tunavyojimwambafi navyo ili tujiongeze kuwekeza katika kuvutia “watalii wenye kutafuta hudama " toka nje ya nchi tajiri na nyingi maskini zilizotuzunguka.
Ni mawazo binafsi.
Mathew Mndeme
mmtogolani@gmail.com