Has anyone confirmed this rumour?
Natamani majibu kwa hili jamani, isijeikawa ndo tunaanza kumshawishi hapa
MKE wa mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa, Bi. Rose Kamili aliyekuwa akigombea ubunge Jimbo la Hanang kwa tiketi ya CCM, ametangaza kujitoa kwenye chama hicho tayari kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Bi. Kamili ambaye alikuwa diwani wa CCM wa Kata ya Basuto, kabla ya Baraza la Madiwani la Hanang kuvunjwa, alitoa tamko hilo hadharani juzi baada ya kumalizika kwa mchakato wa kura za maoni za wagombea kupitia CCM.
Akizungumza juzi mbele ya viongozi wa CCM wa wilaya na waangalizi wa uchaguzi wa kura za maoni akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Bw. Frederick Sumaye na wanachama waliofika ndani ya ukumbi wa CCM kupokea matokeo ya uchaguzi uliompa ushindi Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko Dkt. Mary Nagu, Bi. Kamili alisema ameamua kujiengua kutokana na mizengwe iliyojitokeza wakati wa mchakato wa kura za maoni.
Dkt. Nagu alishinda kwa kura 20,042 wakati Bi. Kamili alipata kura 5,372.
"Nimeamua kuchukua uamuzi huo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za uongozi wa CCM kunikataza kuwatembelea wapiga kura kwa madai kwamba kutangaza nia ni mara moja, vile vile wafuasi wangu kunyimwa kadi za CCM, na makatibu wa matawi kutakiwa kuhakikisha kuwa Mary Nangu anashinda katika uchaguzi huu," alisema.
Hata hivyo, Bi. Kamili hakuzungumza bayana kama anakusudia kwenda chama gani cha siasa, lakini baadaye alilieleza Majira kuwa anahamia kwenye chama cha mumewe, na alikuwa akabidhi kadi yake ya CCM kwa viongozi wa CHADEMA kwenye mkutano ulikuwa umeandaliwa jana katika eneo la Kateshi.
Mapema, akizungumza na gazeti hili kuhusiana na uamuzi huo, Bw. Sumaye, alisema ni kawaida ya mgombea yeyote anaposhindwa kuwa na hasira.
"Naamini hayo ni maneno ya hasira, na hasira yake ikiisha atabadilisha mawazo yake na atabaki kuwa mwanachama wa CCM," alisema Bw. Sumaye.
Naye Katibu wa CCM wilaya ya Hanang, Bw. Michael Tsakhara alisema tuhuma hizo ni za uongo na kwamba walipokuwa kwenye mzunguko wa kuomba kura, kila asubuhi walikuwa wanafanya tathmini ya kuona kama kuna dosari
zilizojitokeza, ili wazifanyie kazi, lakini hata siku moja mgombea huyo hakutoa lalamiko lolote.
Dkt. Nagu baada ya kutangazwa mshindi aliwashukuru wananchi wa Hanang kwa kujitokeza kwa wingi na hatimaye kumpa kura nyingi, hali aliyosema ni ishara kuwa wananchi bado wanamhitaji.