Rorscharch
JF-Expert Member
- Jul 22, 2013
- 878
- 2,014
Ukoloni na Umisionari umechangia kustaarabisha na kuiunganisha Afrika kuliko sisi Waafrika wenyewe
Najua nitakachoandika hapa kitaleta ukakasi kwa watu wengi, lakini ukweli lazima usemwe.Wakoloni kutoka Magharibi walitumia nguvu zao za kijeshi na kiuchumi kutanua himaya zao, wakitafuta rasilimali na maeneo ya kutawala kote duniani. Walivuka bahari na kufika mabara mbalimbali, wakifanya ziara zao za kwanza katika Amerika Kusini, kisha Amerika Kaskazini. Baada ya hapo, waligeukia bara la Asia, na mwishowe walipenyeza Afrika. Hata hivyo, katika kueleza athari za ukoloni, nitajikita zaidi kwenye Afrika na Asia, kwani ujuzi wangu juu ya yaliyotokea Amerika ni mdogo.
Kila wakati mjadala kuhusu ukoloni unapochipuka, huwa napendelea kukaa kimya. Hii ni kwa sababu mitazamo yangu juu ya historia yetu kama Watanzania na Waafrika, mara nyingi inakwenda kinyume na maoni ya wengi, na inaleta hisia za ukakasi. Lakini ukweli hauepukiki, na kuna mambo ya msingi ambayo lazima yasemwe wazi.
Wazungu walipoingia Asia kwa lengo la kutawala, walikumbana na mazingira yaliyokuwa tofauti kabisa na yale ya Afrika. Walikutana na historia ndefu ya utamaduni thabiti wa uongozi wa kifalme, yaani dynasties, ambazo zilikuwa na misingi ya uongozi iliyojengwa kwa karne nyingi. Huko Asia, walikuta mataifa yaliyokuwa na mifumo iliyoeleweka ya utawala, ikiwa ni pamoja na sarafu imara, ukusanyaji wa kodi ulioendelea, na huduma za kijamii kama mifumo ya elimu na tiba. Zaidi ya hayo, dini na falsafa kama Confucianism ziliunganisha watu na kujenga umoja wa kitaifa. Falsafa kama hizi zilisaidia kuunda utaratibu wa kijamii ulio imara na wenye maendeleo ya kifikra, na mkoloni alitambua kwamba hakuwa na haja ya kuvuruga mifumo hiyo imara. Mfano mzuri ni falsafa ya Confucianism nchini China, ambayo inachukuliwa kama sababu mojawapo ya mafanikio ya haraka ya China chini ya karne moja. Hivyo basi, Wazungu walitumia “utawala usio wa moja kwa moja” (indirect rule), ambapo hawakubomoa kabisa mifumo iliyopo. Walitumia kile kilichokuwepo kwa manufaa yao, na hivyo mataifa mengi ya Asia yaliweza kuendelea haraka baada ya kupata uhuru, kwa kuwa misingi ya kitaifa ilikuwa imara tayari. In fact, London ya miaka ya 1800 ilifanana zaidi na miji waliyoikuta Asia kuliko miji waliyoikuta Afrika (ndio maana mpaka Leo mabaki ya nyumba za kale barani hapa kwa asilimia kubwa ni kazi ya mmisionari, mkoloni na mwarabu kuliko sisi wenyewe)
Tukirejea Afrika, hali ilikuwa tofauti sana. Mazingira ya kuanzisha “utawala usio wa moja kwa moja” hayakuwa na manufaa kwa mkoloni, kwa sababu alikuta jamii zetu zikiwa katika mifumo ya kikabila badala ya kuwa na mataifa makubwa yaliyosimama imara. Badala ya falme zenye uongozi thabiti, alikuta machifu na watemi waliokuwa wakiendesha mambo kwa msingi wa ukoo na mila za kikabila. Hata mifumo ya sarafu ilikuwa dhaifu, na matumizi ya biashara ya kubadilishana bidhaa (barter trade) yalikuwa makubwa zaidi kuliko sarafu zenyewe. Tofauti na Asia, sarafu za dhahabu na shaba hazikuwa zimeenea sana, na uchumi wetu ulikuwa umejikita zaidi katika biashara ya moja kwa moja.
Pia, kulikuwa na pengo kubwa katika mfumo wa dini. Badala ya dini kubwa zinazounganisha watu kitaifa, kulikuwa na imani za jadi za kikabila zilizojikita kwenye ibada za mizimu na matambiko. Hii ilimaanisha kuwa kulikuwa na ukosefu wa umoja wa kitaifa, na hakukuwa na mifumo thabiti ya falsafa ya kijamii inayoweza kudumisha taifa kama ilivyokuwa Asia. Hata baadhi ya falme zilizokuwepo kama Baganda, Mwenemutapa, na Dola ya Mali hazikuwa na mifumo imara ya ukusanyaji kodi au utoaji wa huduma za kijamii kama elimu au tiba. Wengi wa watawala hawakuwa na ujuzi wa kusoma na kuandika, na huduma za kijamii, kwa muktadha wa kipindi hicho, zilikuwa za kiwango cha chini sana.
Kwa hivyo, mkoloni alilazimika kubomoa jamii zetu na kuzijenga upya kwa mtazamo wa Magharibi ili kufanikisha malengo yake. Alikuta tamaduni ambazo, kwa mtazamo wao, zilionekana hazijastaarabika na zisizo na muundo imara wa kiserikali. Hata baadhi ya mila za makabila yetu zilionekana kuwa za ajabu, kama vile kuozesha watoto katika umri mdogo au kukata vidole kama sehemu ya mila za maombolezo. Wamisionari walitumika kama chombo cha kuunganisha jamii hizi chini ya mwavuli wa Ukristo, na wakoloni waliona ni muhimu kuingilia moja kwa moja na kuunda mifumo ya kitaifa. Walikusudia kuunganisha makabila mbalimbali na kuunda mataifa mapya, huku wakitumia Ukristo kama njia ya kuleta umoja na utulivu wa kijamii.
Ni ukweli mchungu kwamba tamaduni zetu na mifumo ya maisha ilidharauliwa, lakini lazima tukubali kwamba hata sisi tungekuwa katika nafasi ya wakoloni na tukawakuta Wazungu wakiwa katika hali kama yetu, pengine tungefanya walichofanya wao.
Kwanini tulichelewa kufikia maendeleo Yao? Kuna watu hili swali hawataki kujiuliza kabisa na hata majibu yanayotolewa utakuta lawama zinarudi kwa mkoloni, "waliharibu Kila kitu!", "Tulikuwa na vya kwetu!"; nimejiuliza hili swali kwa muda mrefu Sana na Kwa kuchimbua chimbua hapa na pale nimepata hoja mbili tatu za msingi kama ifuatavyo:
1. Sababu ya Jangwa la Sahara: Jiografia ya Bara la Afrika ilitengeneza gereza ambalo liliifungia kusini ya Afrika na muingiliano na jumuiya ya watu wa magharibi na Asia kwa maelfu ya miaka; Jangwa la Sahara lilififisha Sana muingiliano wa kibiashara kati ya mabara ya ulaya , Asia na Afrika kusini (ukanda unaoishia Sahel), maeneo yetu hata hayakuwa na muingiliano wowote mpaka pale zilivyovumbuliwa mashua na tukapata wageni kutoka eneo la Oman na Yemen
2. Mwinuko wa Bara la Afrika ukilinganisha na mabara mengine; bara Letu hili limeinuka Sana kima Cha bahari ukilinganisha mabara mengine (continental plate), ni kwasababu hii bara Letu halina mito ambayo inafaa kwajili ya usafirishaji wa mizigo ukilinganisha mito ya mabara mengine (mto pekee unaoweza kufanya hivi bara zima ni Nile), Imani yangu kutokana na sababu hii uchumi wa kusafirisha mizigo mikubwa ndani ya Bara haukuwepo kabisa hivyo mataifa imara hayakuweza kuchipua (Kuna uwezekano mkubwa ujenzi wa mapiramidi ya Misri ulifanikishwa na uwepo wa mto Nile ambao ulitumika kusafirisha miamba mikubwa)
3. Mifumo ya Imani iliyokuwepo barani, kwenye hili sijachimba Sana ila kwa ninavyojua tamaduni zetu ni kwamba kwa asilimia kubwa zilikuwepo imani nyingi sana ambazo zilikuwa zimetengeneza utaratibu wa kuabudu Miungu mingi na ni sababu hii nadhani tulikuwa nyuma katika kuunda mataifa na mifumo imara ya kijamii; kwasababu Imani za Ki-Abraham (Ukristu, Uislamu na Uyahudi) zilikuwa zinasisitiza kuabudu Mungu mmoja basi ziliweza kuunganisha makabila mbalimbali na mataifa chini ya mwamvuli mmoja