Wakuu,
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema haijapokea taarifa rasmi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusu kusudio la kutohudhuria hafla ya utiaji saini wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi, wala maoni yoyote ya maandishi kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya kanuni hizo.
Akizungumza baada ya hafla hiyo iliyofanyika leo Aprili 12, 2025 katika ukumbi wa Tume hiyo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima, amesema kuwa licha ya Tume kuwasiliana na vyama vyote kwa barua na simu, CHADEMA hawakufika ukumbini kusaini wala kutuma mwakilishi, jambo ambalo kwa mujibu wa Tume linachukuliwa kama kutoridhia rasmi kushiriki.
Pia soma >
Pre GE2025 - Tume ya Uchaguzi: Vyama 18 kati ya 19 vyasaini kanuni za maadili ya uchaguzi. Visivyosaini havitaruhusiwa kushiriki Uchaguzi Mkuu
"Hatujapokea taarifa rasmi wala hatujamwona akitokea. Kwa sababu ni hiari kusaini maadili, usiposaini, huwezi kusemekana umetia saini. Tulitaka tuone mwakilishi wa chama amefika na kusaini hapa ukumbini. Kama wameamua kutokusaini na kutangaza hilo mitandaoni, hiyo ni kwao. Lakini sisi hatukupata taarifa rasmi," amesema Kailima.
Ameongeza kuwa CHADEMA haikutuma maoni kuhusu rasimu ya kwanza ya kanuni hizo, wala haikuwasilisha maoni ya pili yaliyopelekwa Aprili 4, 2025.
“Kuna vyama havikuleta maoni na vimesaini; tunaamini vimeridhika. Kwa hiyo, CHADEMA kutotuma chochote kunatufanya tuchukue kuwa waliridhika" ameongeza.
Tume imethibitisha kuwa kwa mujibu wa Kanuni hizo mpya, CHADEMA itakosa sifa ya kushiriki siyo tu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, bali pia chaguzi zote ndogo zitakazotokea ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo hadi 2030.
"Kanuni hizi zinatungwa kila baada ya miaka mitano. Chama ambacho hakikusaini hakitashiriki uchaguzi wowote ndani ya kipindi hicho," amesisitiza Kailima.
Vyama 18 vilihudhuria hafla hiyo ya utiaji saini, vikiwemo CCM, ACT-Wazalendo, CUF, CHAUMMA, ADC, NCCR-Mageuzi, TLP, na vingine.
Hatua hii inaweka bayana changamoto mpya kwa demokrasia ya vyama vingi nchini, huku ikizua maswali kuhusu nafasi ya vyama vya upinzani katika michakato ya uchaguzi iwapo watakosa kushiriki kwa vipindi virefu kwa sababu za kikanuni.