Mkutano wa nchi za BRICS ulifanyika mjini Kazan, Russia wili iliyopita ikiwa ni mara ya kwanza kwa kundi hilo kukutana kwa jina la BRICS Plus, ikiwa na maana kuwa uanachama wa kundi hilo umepanuka kutoka wanachama watano wa awali (Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini) hadi wanachama kumi pamoja na Ethiopia, Iran, Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu. Mbali na mkutano huo kuhudhuriwa na wanachama 10 kwa mara ya kwanza, kinachovutia zaidi ni maudhui ya mkutano na maana yake katika mazingira ya sasa kwenye siasa za kimataifa. Mbali na mambo ya ushirikiano kati ya nchi wanachama, ajenda ya mkutano pia inahusu majadiliano kuhusu masuala ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na mgogoro wa Mashariki ya Kati, na ushirikiano kati ya nchi za BRICS na Kusini.
Ajenda ya mgogoro wa mashariki ya kati ni mwiba mchungu kwa baadhi ya nchi za magharibi, ambazo kwa makusudi kabisa zimeamua kuufumbia macho mgogoro huo kwa kuwa wao si wahanga na hawaathiriki na mgogoro huo kwa namna moja au nyingine. Ni mwiba mchungu kwa kuwa unawavua nguo na kuwaacha na aibu ya kuruhusu hali mbaya iendelee kutokea katika eneo la mashariki ya kati.
Ajenda ya ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi kati ya BRICS na nchi za kusini, pia ni ajenda ambayo kimsingi inaonesha umuhimu wa kundi la BRICS katika kuhimiza maendeleo ya nchi za kusini. Pamoja na ukweli kwamba nchi nyingi za kusini bado zina changamoto kubwa kiuchumi, nchi za Kaskazini zinatumia hali hiyo kama mbinu ya kujiingiza kwenye nchi hizo kwa maslahi yake ya kiuchumi na kutafuta nafasi kwenye siasa za kijiografia, na sio maendeleo halisi ya nchi hizo. Hali hii pia inaonesha kuwa kundi la BRICS linakuja na mtazamo mpya na hata kuleta njia mpya za maendeleo ya nchi za kusini.
Kinachoweza kushangaza baadhi ya watu ni mwitikio mkubwa ulionekana kwenye ushiriki wa mkutano huo. Nchi za magharibi zimefanya kila njia kujaribu kuitenga Russia kisiasa, na kutaka hata nchi nyingine duniani ziitenge Russia. Ushiriki wa nchi mbalimbali kutoka Amerika Kusini, Afrika na Asia, na uwakilishi wa wakuu kutoka mashirika mbalimbali ya kimataifa, umeonesha kuwa nchi nyingi hazikubaliani na mtazamo wa nchi za magharibi kuwa ‘adui yangu, lazima awe adui yako”.
Ajenda za mkutano na wingi wa ushiriki wa wajumbe kutoka nchi mbalimbali duniani, vinaonesha kuwa kundi la BRICS linaendelea kuwa na mvuto mkubwa, na linaendelea kuwa jukwaa kwa nchi mbalimbali duniani kujadili mambo ya amani na maendeleo kwa uhuru, na sio kwa kusukumwa kama inavyoonekana kwenye baadhi ya mikutano ya kimataifa. Licha ya kuwa baadhi ya nchi za magharibi hazifurahishwi na kundi la BRICS kwa kisingizio kuwa kundi hilo linamega himaya zao, ukweli ni kwamba ombwe lililoachwa na nchi za magharibi kutokana na kutotekeleza wajibu wao, ndio unafanya kundi hili liwe na mvuto mkubwa kwa nchi mbalimbali duniani.