Mkutano wa Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF na waandishi wa habari Januari 29, 2025

Mkutano wa Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF na waandishi wa habari Januari 29, 2025

Boveta

JF-Expert Member
Joined
Jul 23, 2019
Posts
3,174
Reaction score
3,804
Ndugu wanahabari!
Karibuni sana kwenye tukio letu hili ambapo leo CUF- Chama Cha Wananchi kinaongea na Umma wa Watanzania, hususan Wazanzibar kupitia vyombo vya habari.Tunaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyefanikisha uwepo wetu hapa katika muda huu. Nawashukuru nanyi wanahabari kwa kuitikia mwaliko wetu kwenye tukio hili muhimu la Kihistoria, ambalo bila ya uwepo wenu haliwezi kukamilika.

Ndugu wanahabari!
Leo ni Jumatano Januari 29, 2025. Ni sawa na Mwezi 28 au 29, Rajab. Leo CUF- Chama Cha Wananchi kinaandika historia mpya. Kwa mara ya kwanza mwanamke ameaminiwa kupewa jukumu la kukiongoza Chama hiki kama KATIBU MKUU. Alipozaliwa Maryam mama wa Nabii Issa (Yesu), Imraan baba mzazi wa Maryam alipoteza furaha na kuingia unyonge kwa sababu tu Maryam ni mwanamke. Kinyume na matarajio ya wengi, Familia ya Maryam leo inatajwa kwa heshima na wema na historia yake haitofutika kwa sababu mwanamke Maryam ameipa heshima kubwa familia. Na miongoni mwa Sura 114 za Quran,Kuna sura imepewa jina la bi Maryam (suratul maryam). Mwenyezi Mungu akiamua, mwanamke anaweza kuwa sababu ya Ukombozi wa jamii yenye wanawake na wanaume.

Namuomba Allah aliyeniumba mimi mwanamke Husna Mohammed Abdallah, anijaalie kuwa sababu ya kuendeleza na kuipaisha Heshima kubwa ya CUF- Chama Cha Wananchi. Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba unisaidie katika hili na ukipe heshima Chama changu kilichoniamini.

Ndugu wanahabari!
Kiongozi yeyote mmoja, awe maarufu na mwenye nguvu kuliko wote, hawezi kufanikisha Ushindi wa TAASISI yoyote ile bila KUPATA mashirikiano kutoka kwa viongozi wenzake na walio chini yake. Nitumie fursa hii kutoa shukrani za dhati kwa Mwenyekiti wa Chama Taifa Prof. Ibrahim Lipumba kwa kuniamini na kunipendekeza kugombea nafasi hii na nawashukuru pia wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa kunichagua. Kwa namna ya kipekee nawashukuru sana viongozi wenzangu wa Bara na Zanzibar kwa kunionesha mapenzi makubwa tangu nilipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu. Mapokezi makubwa niliyoyapata leo ni kielelezo cha upendo wenu na imani yenu kubwa kwangu. Licha ya vikwazo mbalimbali vilivyojitokeza kukwamisha tukio hili na kupelekea wengine wasijitokeze leo kwa kukosa uhakika wa kufanikiwa kwa ratiba hii ya mapokezi, nyinyi hamkukatishwa tamaa na mkaacha ratiba zenu nyengine muhimu ili tu mshiriki Mapokezi ya KATIBU MKUU wenu. Nawashukuru sana, kwa hakika mmenipa hamasa kubwa ya kujituma katika nafasi hii huku nikijiamini kwamba sipo peke yangu. Umoja wetu ndio nguvu yetu.

Ndugu wanahabari!
Huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu kwenye nchi yetu. Ili kufanikisha Uchaguzi Mkuu, ratiba ya Uboreshaji wa daftari la Kudumu la wapiga kura imeshatoka na tayari zoezi hilo limeanza maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Natoa wito kwa watanzania wote, hususan kwa Wazanzibar kuhakikisha wanajiandikisha na viongozi wa Wilaya na majimbo wahakikishe wanafuatilia na kulisimamia vizuri zoezi hili.

Ndugu wanabari!
Juzi tulikuwa tunawakumbuka ndugu zetu waliouawa Kinyama Januari 26 na 27, 2001 kutokana na Maandamano ya Amani yaliyoratibiwa na CUF- Chama Cha Wananchi. Pamoja na madai mengine, Maandamano hayo yaliyoacha majeraha yasiyopona yalibeba Ajenda ya Katiba Mpya na Tume huru ya Uchaguzi. Sasa ni miaka 24 tangu mauaji hayo yatokee, lakini bado kama taifa hatuna Katiba Mpya wala Tume huru ya Uchaguzi. Ni muda muafaka sasa kupaza sauti zetu na kutumia kila mbinu halali kuhakikisha Katiba Mpya itakayoitambua Zanzibar kama nchi huru ndani ya Muungano inapatikana. Katiba Mpya ni muhimu sana katika kuhakikisha nchi inapiga hatua Kimaendeleo na Kidemokrasia, Haki za Binadamu na Sheria, Utawala Bora na pia kuimarisha Muungano katika namna itakayoifanya Zanzibar ijihisi haimezwi na upande wa Pili wa Muungano.

Ndugu wanahabari!
Nchi yetu inaendelea kuathiriwa sana na mmomonyoko wa Maadili. Vijana wengi wanajiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya, mapenzi ya jinsia moja na biashara za ngono. Nikiwa kama mama, naumia sana kuona kila siku matendo haya yanakithiri hata huku kwetu Zanzibar. Japokuwa matendo haya kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na umaskini ambao sisi CUF- Chama Cha Wananchi tuna tiba yake endapo tutashika dola, hatuwezi kufumbia macho uharibifu huu. Tunatoa wito kwa wazazi na wananchi wote kwa ujumla kushikamana katika kupambana dhidi ya mmomonyoko wa Maadili nchini kote.

Ndugu wanahabari!
Ningependa sasa kuzungumzia UWAZI KWENYE SUALA LA MASLAHI YA WAZANZIBAR. Tunatambua uwepo wa mfumo wa Rais Dkt Mwinyi unaoitwa "SEMA NA RAIS MWINYI". Sisi CUF- Chama Cha Wananchi tunaamini Mfumo huu bado hauna msaada mkubwa kwa Mzanzibar. Tunahitaji Uwazi katika masuala yote yanayohusu maslahi ya Mzanzibar ikiwemo kwenye suala la ajira rasmi na zisizo rasmi, fursa za uwekezaji, Zabuni (Tenda) za Serikali na fursa nyinginezo. Ni aibu na kashfa kwa Zanzibar kama nchi kuona hata fursa ambazo wazawa wana uwezo wa kuzitumikia wanapewa wageni. Zaidi ya kuidhalilisha nchi, utaratibu huu unawazidishia umaskini Wazanzibar. Ni wakati muafaka sasa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kumfanya Mzanzibar kuwa kipaumbele katika fursa na harakati zote za Kimaendeleo, hususan za Kiuchumi.

Ndugu wanahabari!
Ingawa bado ninayo mengi ya kusema, lakini leo si siku yangu rasmi ya kuongea. Ni siku ya Mapokezi yangu. Ni siku ya kutambulishwa kama KATIBU MKUU mpya wa CUF- Chama Cha Wananchi. Nitumie fursa hii kuwashukuru tena kwa kazi yenu nzuri ambayo daima mmekuwa mkiifanya kwa maslahi mapana ya wanaadamu.


HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!


Mhe. Husna Mohammed Abdallah
Katibu Mkuu
CUF- Chama Cha Wananchi
Januari 29, 2025```
 
Lipumba kashamaliza kazi yake hamna chama humo.
 
Back
Top Bottom