Ni muhimu kujua ameongea nini...suala si kupongeza tu!
Nadhani Mwananchi wameicover hapa
Boniface Meena
KATIBU mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na katibu wa itikadi na uenezi, John Chiligati wamepatwa kigugumizi kuhusu madai ya Spika Samuel Sitta kwamba ofisi ya makao makuu ya chama hicho ilizuia viongozi wa Mkoa wa Tabora kumpokea kwenye ziara yake.
Viongozi hao pia wamekwepa kusema chochote kuhusu maelezo ya Sitta, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC), kwamba anasikitishwa na namna makao makuu inavyoshughulikia baadhi ya mambo, akihoji sababu za wao kuzungumzia masuala ambayo yako mikononi mwa kamati maalum.
Sitta alilalamikia kitendo cha viongozi wa mkoa wa Tabora kususia mapokezi wakati wa ziara yake mkoani humo akituhumu kwamba walitimiza maagizo ya viongozi wa juu wa chama hicho.
Sitta alinusurika kuvuliwa uanachama wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM wakati baadhi ya wajumbe walipotaka arejeshe kadi kwa madai kuwa, amekuwa akiendesha vikao vya Bunge kwa kuruhusu na kuishabikia mijadala inayokichafua chama na serikali.
Jaribio hilo, ambalo linadaiwa kufanywa na watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, lilikwama na tangu wakati huo mbunge huyo wa Urambo Mashariki anaonekana kuwa kwenye hali ngumu ndani ya chama.
Mwishoni mwa wiki alitumia mkutano wa hadhara kunena yaliyoujaza moyo, akilalamikia kauli zinazotolewa na viongozi tofauti kuhusu maazimio ya Nec na madai kuwa ofisi ya makao makuu ya CCM ilizuia viongozi wa chama hicho mkoani Tabora kushiriki kwenye mapokezi yake, kitu ambacho kimetafsiriwa kuwa ni kulalamika nje ya vikao vya CCM.
"Analalamika kwenye magazeti badala ya kuleta taarifa kwetu; aje na malalamiko yake nitayashughulikia; sijayaona malalamiko yake," alisema Makamba jana alipoongea na Mwananchi kwa njia ya simu.
Makamba, ambaye pia aligoma kuzungumzia malalamiko ya Sitta kwamba, amekuwa akizungumzia mambo yaliyojadiliwa na Nec nje ya vikao badala ya kuiachia kamati iliyoundwa, alimtaka Sitta kuwasilisha malalamiko hayo kwake ili ayafanyie kazi.
Naye Chiligati alisema: "Halmashauri inasema mambo hayo yazungumzwe ndani ya chama na magazeti yaandike mambo ya maendeleo."
Chiligati alisema Sitta anapaswa kutoa malalamiko yake ndani ya vikao vya chama, ili yajadiliwe na kupatiwa ufumbuzi kuliko kuzungumza nje ya vikao kama anavyofanya sasa.
Juzi Spika Sitta aliwaambia waandishi wa habari nyumbani kwake Urambo, Tabora kuwa amesikitishwa na wakuu wa chama kumzuia katibu na mwenyekiti wa mkoa wasimpokee wakati alipowasili mkoani humo. Hata hivyo, wanachama wengi walijitokeza kumpokea.
"Nimesikitishwa na wakuu wa chama ambao waliruhusu, (Andrew) Chenge na (Edward) Lowassa wapokewe, lakini wanawazuia katibu na mwenyekiti (Wa Tabora) wasinipokee, ingawa wanachama walijitokeza kunipokea; hii ndiyo inatufanya wanachama tuamini kuwa kuna wanachama wenye haki na wasio na haki; hii si dalili nzuri,"alisema Spika Sitta.
Alishangazwa na kitendo cha ofisi ya makao makuu ya CCM kuushinikiza uongozi wa mkoa usimpokee wakati alifika kwenye ofisi ya mkoa na kuweka saini katika daftari la wageni, lakini akashangazwa kuwa viongozi hao hawakujitokeza pamoja na kuwa wanachama walijitokeza kwa wingi.
Akizungumzia kuhusu uamuzi uliotolewa na CCM mjini Dodoma, alisema anashangaa kuona kila mtu anatoa kauli katika mambo ambayo ni dhahiri yanayoonekana kuwa ni tuhuma bila ya kuacha vyombo vilivyoundwa na chama vifanye maamuzi yake.
"Nasikitishwa na jinsi ambavyo makao makuu ya CCM yanashughulikia baadhi ya mambo kwa kuwa ingekuwa ni mara moja kama kutoa taarifa, basi kauli ya katibu wa itikadi na uenezi, Kapteni John Chilligati ingetosha, lakini inashangaza wanavyorudiarudia mambo ambayo bado yanatakiwa yashughulikiwe na kamati maalumu," alisema.
Alisema anashangazwa jinsi kikundi cha watu kinavyojaribu kuzungumza mambo ya uzushi kuhusu yeye na kujaribu kusema mambo ambayo hata hayapo.
Sitta, ambaye alikuwa kwenye hali ngumu wakati wa kikao cha Nec ambacho kilitawaliwa na maombi ya baadhi ya wajumbe ya kutaka avuliwe uanachama, alisema kuwa anasikitishwa na kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa CCM ambazo alisema zilionyesha kuhukumu hata kabla tume iliyoundwa na NEC haijatoa matokeo yake.
Kuhusu malalamiko ya Sitta kuwa Makamba amekuwa akizungumza zungumza nje, Chiligati alisema kuwa suala hilo pia linatakiwa lizungumzwe ndani ya chama.