KWELI Mlaze chali mtoto mchanga tofauti na kifudifudi au ubavu kipindi ambacho hajamudu kujigeuza mwenyewe

KWELI Mlaze chali mtoto mchanga tofauti na kifudifudi au ubavu kipindi ambacho hajamudu kujigeuza mwenyewe

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Nimeona kuna taarifa zinadai kuwa kumlaza mtoto katika mitindo tofauti na chali kunawesza kumletea madhara ikiwemo vifo vya ghafla, hili jambo limekaaje?
kumlaza mtoto.jpg
 
Tunachokijua
Watoto wachanga hutumia muda mwingi kulala lakini hali hiyo hupungua kadri wanavyozidi kukua. Stamford Medicine wanaeleza kuwa mtoto mchanga anaweza kulala kwa vipindi tofauti tofauti kwa masaa 8 hadi 9 kwa wakati wa mchana na masaa 8 kwa wakati wa usiku na muda wa kulala hubadilika kadri anavyozidi kukua.

Imekuwepo taarifa inayoeleza kuwa kuna mtindo ukimlaza mtoto mchanga anaweza kupata madhara mbalimbali ikiwemo kifo ghafla.

Ukweli upoje?

JamiiCheck imepitia machapisho mbalimbali na kubaini kuwa inapendekezwa kumlaza mtoto mchanga katika mtindo wa chali kuliko mitindo mingine yani kifudifudi ama ki ubavu ili kupunguza hatari ya watoto kupata vifo vya ghafla.

Kwa mujibu wa tovuti ya taasisi ya Taifa ya afya ya mtoto na maendeleo ya binadamu ya nchini Marekani (NIH) kupitia kitini chao cha maswali na majibu kuhusu namna ya kumlaza mtoto na vifo vya ghafla kwa watoto wameelezea kuwa mwaka 2005 kituo cha American Academy of Pediatrics (AAP) kupitia kikosi kazi chake cha kuchunguza aina za ulalaji na vifo vya ghafla kwa watoto wachanga ilitoa mapendekezo yaliyofanyiwa marekebisho kuhusu namna ya kupunguza vifo vya ghafla kwa watoto wachanga na miongoni mwa mapendekazo hayo ni kuwa, ni vizuri watoto wenye afya njema kulazwa chali kama njia kuu ya kupunguza vifo vya ghafla kwa watoto wachanga.

Taasisi ya NIH imekuwa na kampeni ya kuhamasisha watoto kulazwa chali tangu mwaka 1994 na wanaeleza kuwa imekuwa na mafanikio makubwa sana.

Kwa mujibu wa tovuti ya MedicalNewsToday inaeleza kuwa hatari kubwa ya kumlaza mtoto ki ubavu ni kuwa mtoto anaweza kujikuta amelala kifudifudi na kupelekea kujiziba uso ikiwemo pua katika godoro, au vitu vingine vilivyopo mahali alipolala na kumletea athari ikiwa mtoto huyo hatokuwa bado na uwezo wa kuinua kichwa. Watoto wengi huweza kumudu na kuinua vichwa vyao wakifikisha umri wa miezi 4.

Mtoto mchanga anaweza kujigeuza kutoka upande mmoja kwenda mwingine akiwa na umri wa miezi 3 hadi 4, na kujigeuza kutoka kulala chali hadi kifudi fudi au kifudifudi kwenda chali akifikisha umri wa miezi 4 hadi 6. MedicalNewsToday wameeleza kuwa watu wengi wanaamini kwamba kumlaza mtoto mchanga ki ubavu inamsaidia kutopata shida anapocheua au kutapika jambo ambalo si sahihi kwani hali hiyo hain uwezekano mkubwa wa kumuathiri mtoto huyo.

Ikiwa mtoto atakuwa amefikisha umri wa kuweza kujigeuza mwenyewe basi hakuna haja ya kuwa na hofu ama kumgeuza ikiwa atakuwa amelala kifudifudi, ki ubavu ama chali iwapo mazingira aliyopo sio hatarishi.

Taasisi ya Lullaby trust ya nchini uingereza inayojihusisha na tafiti na kuzuia vifo vya watoto wachanga walichapisha kipande cha video katika mtandao wa facebook kuonesha namna ya kumlaza mtoto mchanga ili kupunguza hatari ya vifo vya ghafla kwa watoto hao.

Lullaby trust wameonesha kupitia kipande hiko cha video kuwa namna bora ya kumlaza mtoto mchanga ni kumlaza chali kuliko kiubavu ama kifudifudi wakati wowote alalapo iwe usiku ama mchana. Sambamba na hayo pia wamependekeza kutomfunika mtoto na mavazi ama mashuka mazito, kutokuweka vitu vingi mahali anapolala mtoto mfano midoli na mito.
Back
Top Bottom