KwetuKwanza
Member
- Mar 13, 2023
- 82
- 150
Kama kuna sehemu uongozi wa Mkoa wa Simiyu, Wilaya ya Bariadi na vyombo vya kiuchunguzi wanatakiwa kutupia macho sana ni hili eneo la mnada wa mifugo Bariadi,
unaopatikana kwenye eneo la Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mtaa unaitwa KIDINDA.
Kwenye huu mnada wetu ambao kwa wiki unafanyika mara mbili, siku ya Jumanne na Jumamosi, watu wanaowekwa mara nyingi udanganya takwimu za mifugo inayoingia kwenye mnada kwa siku ili wajinufaishe.
Serikali ya Mkoa na Wilaya lazima itambue huu mnada wetu ni mkubwa sana kwa Kanda ya Ziwa.
Mfano kwa siku moja ya Jumanne, huu mnada wetu unaingiza takribani ng’ombe 4,000 hadi 5,000, mbuzi siyo chini ya 3,000, kondoo siyo chini ya 2,000.
Pamoja na idadi hiyo, utaratibu uliopo hapa, mfugaji yeyote kuingiza mfugo wake mmoja ni bure lakini kutoa ni pesa, ambapo Ng’ombe mmoja anatozwa Sh. 7,500 ukimtoa nje ya mnada.
Mbuzi na kondoo wanatozwa shilingi 6,500, kwa hesabu hizo kwa siku huu mnada unaweza kukusanya zaidi ya Shilingi Milioni 30.
Kama kiwango cha chini kabisa, ukichukua hiyo Shilingi Milioni 30, ukazidisha kwa wiki nne ndani ya mwezi, Serikali inapata zaidi ya Shilingi Milioni 120 kwa mwezi.
Huu mnada unaweza kuwa chanzo ambacho kinaweza kuendesha hii Halmashauri ya Mji wa Bariadi na kukawepo maendeleo makubwa lakini sidhani kama hilo linafikiriwa.
Utozaji wa gharama hizo za mifugo ambayo inatoka kwenye eneo la mnada, siyo kwamba anatozwa aliyeuza au kununua mfugo wowote, hapana, ni mfugaji yeyote awe ameuza au hajauza.
Awe mnunuzi amenunua ndani ya mnada, lazima alipie mfugo wake akitaka kutoka nje ya mnada kuweza kusafirisha mfugo wake.
Licha ya makusanyo hayo kuonekana ni makubwa lakini asilimia kubwa yanaishia kwenye mifuko ya Wakusanyaji na siyo Serikalini.
Wanachofanya wafanyakazi ambao wamepewa dhamana ya kukusanya mapato kwenye mnada huo, hawapeleki takwimu sahihi za mifugo ambayo imeingia na kutoka ndani ya mnada huo.
Wanachofanya kama ng’ombe wameingia 3,000 wao watapeleka 2,000 na inayobaki ni kwa ajili ya mapato yao, hivyo hivyo kwenye mbuzi na kondoo.
Badala ya Serikali kupata Sh Milioni 30 kwa siku moja, utakuwa inapata Milioni 10 hadi 15, hivyo mapato mengi yanaishia kwenye mifuko ya watu wachache ambao walipewa dhamana ya kukusanya kodi ya Serikali.
Mamlaka zinatakiwa kuamka kuanzia sasa, kuweka jicho la tatu kwenye huu mnada, Serikali inatakiwa kuzinduka kuweka jicho la tatu kwenye huu mnada, kwani mapato mengi yanaishia mifukoni mwa Watumishi.