Robert Heriel Mtibeli
JF-Expert Member
- Mar 24, 2018
- 28,297
- 68,017
MNAZI NA WATU WENYE MAFANIKIO
Na, Robert Heriel
Maandishi ya Robert Heriel kwa Lugha ya Kiswahili. Haki zote zimehifadhiwa.
Leo tutaangazia habari ya Mti wa Mnazi na namna ulivyo na ufanano na watu wenye mafanikio. Bila shaka baada ya andiko hili tutakuwa tumejifunza mambo fulani yenye manufaa katika kujifanikisha kwa jambo lolote lile(Nikidhamiria jambo jema)
Naziona akili za Mungu ni kubwa mno, nashindwa kuzieleza. Mungu aliumbe mimea ya kila aina, yenye kuvutia, kupendeza na yenye kutisha. Yenye maua mazuri yanukiayo vizuri na yale yanukayo Fuuu!
Kwenye mmea kuna mambo yafuatayo, Mizizi, shina, matawi, majani, maua, tunda na mwishowe Mbegu. Kila sehemu ni muhimu na yalazima kwenye mti. Leo nitajikita zaidi kwenye Matunda na Mbegu, ingawaje naweza kugususia kidogo kwa uchache kuhusu sehemu zingine za mti.
Mungu alipoumba Matunda iwe sehemu kwenye mimea alitumia akili nyingi sana, hakuna awezaye kuzieleza akamaliza.
Nafikiri Mungu alizingatia mambo yafuatayo alipokuwa anaumba matunda kwenye mimea
1. Ukubwa au udogo wa tunda (Size)
2. Gamba la tunda (gumu au laini)
3. Tabia ya nchi na hali ya hewa.
4. Umri wa mmea
Hapa ndipo somo letu lilipo.
Kama utachunguza utagundua hivi; Matunda yenye magamba laini na makubwa huwa yapo kwenye mimea ya kutambaa na ile yenye vimo vifupi kama vile Matikiti, na maboga, na yenye udogo wa wastani lakini yanamagamba laini kama vile nyanya. Huishi muda mdogo nadhani aina hii ya matunda haiwezi kuwa na umri unaozidi mwaka mmoja.
Pia matunda yenye magamba laini na na ukubwa wa wastani huwa kwenye miti yenye vimo wa wastani kama vile Maembe machungwa, parachichi, Miti hii huishi miaka ya kawaida japo sio miaka mingi. Huweza kuishi miaka zaidi ya 30 na isizidi 50.
Matunda yenye magamba laini makubwa yaliyokwenye miti ya yenye vimo vya wastani lakini miti hiyo haina umri mrefu(haiishi miaka mingi) kama vile mapapai. Huishi miaka isiyozidi mitano.
Matunda yenye maumbile madogo kabisa yaliyokwenye miti mikubwa na mirefu yenye magamba laini. Miti yao huishi miaka ya kawaida, miaka 30 na isiyozidi 70. Mara nyingi miti hii huwa ni dawa na matunda yake hayaliwi na binadamu huliwa na wanyama na ndege, japo wanadamu hata wakiyala hawapati madhara.
Matunda yenye maumbile madogo yenye gamba laini kabisa yaliyokwenye miti yenye vimo vifupi, huishi miaka michache huishi miaka kuanzia 1 - 4. kisha hufa. Matunda yake huliwa na wadudu na baadhi ya ndede.
Matunda yenye ukubwa mkubwa yenye magamba magumu, yalipo kwenye miti mirefu kama Nazi na mibuyu. Huishi miaka mingi si pungufu ya miaka 50 na si zaidi ya miaka 500, Mibuyu inauwezo wa kuishi mpaka miaka mia tano (500). Minazi huweza kuishi hata miaka 300.
Somo letu lipo hapo.
Mnazi ni jamii ya mti wa mitende ambayo huishi mara nyingi kwenye tabia ya nchi ya Kitropiki na hupenda kuotea pembezoni mwa bahari. Matunda yake huitwa Nazi.
Nazi ni mojawapo ya matunda makubwa yaliyopo duniani yanayoliwa na binadamu, Nazi ndio tunda pekee kubwa linaloliwa na lenye gamba gumu.
Ugumu wa gamba la tunda la Nazi na umbali wake kutoka juu ya mnazi ndio umenivutia na kufanya mikono yangu leo iandike.
KWA NINI NAZI INA GAMBA GUMU?
1. Ili likianguka juu ya mnazi lisipasuke
Unajua mnazi ni mti mrefu, kumaanisha kama nazi lingekuwa na gamba laini basi pindi linapoanguka chini basi tunda hilo lingepasuka. Lakini Mungu amelipa gamba gumu kusudi likianguka lisipasuke
2. Kujihami na adui
Nafikiri ni viumbe vichache sana vilivyoweza kufanikiwa kufua na kupasua tunda la nazi. Kwa wanyama ni binadamu pekeake ndiye anauwezo wa kula nazi, viumbe wengine ni wadudu wadogo hasa bacteria ambao wengi hutumia kikonyo kuingia ndani ya nazi na kuifanya iharibike. Hii ni tofauti na matunda mengine yenye gamba laini ambayo hushambuliwa na adui yoyote.
Nilivyokuwa mdogo kama watoto wengine tulipokuwa tukienda shambani kuiba matunda ya watu, moja ya matunda yaliyotupa tabu kuyaiba ilikuwa ni Nazi. Mara nyingi tulifanikiwa kuiba kwa urahisi kabisa maembe, mapapai, matikiti, matope tope, miwa, n.k hatukuhitaji umakini wowote tukiiba matunda hayo, tulichohitajika zaidi ni kuangalia mwenye shamba asije akatukuta.
Matunda hayo yaani maembe, mapapai, miwa, matope tope na matikiti hayakuhitaji akili yoyote, ujuzi au ujasiri. Hata mimi Taikon niliyekuwa muoga wa kupanda miti niliyamudu kwani nilikuwa na uwezo wa kutyatupia mawe yakashuka, au kushukua mti na kuyapiga yakashuka. Lakini sio kwa nazi na mti wake.
Kuzipata nazi zilihitaji watu SPESHO, JASIRI, wenye wa kupanda miti na wenye PUMZI bila kuchoka yaani wasiokata tamaa. Kwenye kundi letu alikuwepo mmoja tuu mwenye uwezo huo. Sisi wengine tulikosa sifa za kupata nazi.
MAMBO YA MTI WA MNAZI
1. HAUNA MATAWI (HAKUNA MSAADA WA PEMBENI)
Unajua mti wa mnazi umekaa kimkakati mno, umakataa kimtego sana. Kwanza hauna matawi, yaani hutapata msaada wa kushika zaidi ya kujikumbatia kwenye shina kuu la mnazi. Hii inatuambia kuwa tunapotafuta mafanikio hasa yale makubwa ni ngumu sana kupata msaada, na kama msaada upo basi huwa mwisho kabisa kama yalivyo matawi/makuti ya Mnazi ambapo huwa mwishoni kabisa tena karibu na nazi kabisa.
Watu karibia wote waliofanikiwa walipanda mnazi, wengi watakuambia hawakuwa na msaada wowote yaani matawi ya kujishikilia isipokuwa shina tuu. Na walipofika karibia na mafanikio ndipo msaada ukajitokeza.
2. UNAHITAJI PUMZI (KUTOKATA TAMAA)
Kama nilivyosema mti wa mnazi hauna matawi ya pembeni(msaada) alafu ni mrefu sana. Hivyo lazima uwe na pumzi ya kupanda na ya kushuka. Mimi nikiwa mdogo wakati wa harakati za utoto tukiwa tunaiba nazi za watu mashambani huko kijijini niliwahi kujaribu kupanda Mnazi lakini niliambulia aibu kwani sikufika hata robo ya mti ule. Siku na pumzi, nilitegemea matawi, na ujanja wa kurusha mawe kwenye miti mingine lakini kwa mnazi nilikwama. Kwanza hata nirushe mawe yalikuwa hayafiki na yakifika yanakuwa hayana nguvu ya kupiga nazi ikaanguka. Pili hapakuwa na matawi.
Waliopanda mnazi wote watakuambia jambo moja kuwa nazi inahitaji uwe na pumzi na kutokukata tamaa
Hata mafanikio yanahitaji watu wenye pumzi, watu wasiokata tamaa. Lakini wale wenzangu na miye wazee wa kurusha virungu juu ya miti au kutegemea matawi mafanikio makubwa tutayasikia tuu.
Waliofanikiwa karibu wote kwenye jambo lolote lile walikuwa na pumzi na hawakukata tamaa. Wote tunajua kupata elimu ya juu ilivyokazi ngumu, waliojitahidi waliipata, wote tunajua biashara ilivyongumu lakini waliokaza wengi wamefanikiwa, wote tunajua kumpendeza Mungu ilivyongumu, lakini watakaokaza ndio watakao fanikiwa.
3. KUCHUMA NAZI YAHITAJI UJUZI
Unaweza kufanikiwa kupanda Mpaka juu ya Mnazi na bado ukashindwa kuichuma Nazi. Kuitoa nazi kwenye kikonyo chake yahitaji ujuzi, mbinu na akili. Kama hutaki shida labda utumi dhana kama kisu kuitoa nazi kwenye kikonyo chake. Vinginevyo unaweza kuhangaika kutwa hata nazi moja hujaitoa licha ya kuwa umeifikia nazi. Jambo hili nililiona enzi hizo tukiwa tunaiba nazi, aliyepanda alikuwa akihenyeka kweli kuzichuma nazi.
Hata kwenye mafanikio unaweza ukakaza mpaka ukafikia mafanikio yenyewe lakini ukashindwa kuyachuma, kuyapata, hujawahi ona watu wameajiriwa kwenye makampuni makubwa, wenye elimu kubwa na mishahara minono lakini maisha yao ya kawaida au hawana mafanikio yoyote licha ya kufika kileleni. Hujawahi kuona mtu ni mashuhuri huenda ni mwanamuziki, muigizaji, au mtu wafani fulani lakini hana mafanikio yoyote licha ya kuwa kwenye ukanda wa mafanikio. Anaishia kupoteza muda na baadaye akishashuka watu husema yule alikuwa juu ya mnazi kileleni kabisa lakini alishindwa kushuka na nazi.
4. KUIFUA NAZI
ukishafika kileleni ukahangaika wee mpaka ukazipata nazi. Usije ukadhani umemaliza kazi. Bado kuna kimbembe cha kufua nazi. Unaweza kuipata nazi lakini ukashindwa kuifua, wakafua wengine nazi uliyoichuma na mkagawana au wasikupe hata kidogo.
Kuifua nazi yahitaji ujuzi, umakini, na yahitaji werevu mkubwa,
Mafanikio nayo yapo hivyo hivyo, unaweza ukapata kazi ya kukuingizia kipato lakini ukashindwa kuifanya kazi vizuri mpaka ikawa haikulipi au huoni faida yake. Yaani unashindwa kuitumia kazi yako ikupatie matunda.
5. KUITUMIA NAZI
Hii ndio level ya juu kabisa ya mafanikio. Wanaofika huku ni wachache, yaani mmoja kwa mia. Tayari ushapata nazi, sasa unaamua kuipangia matumizi, unaweza kuchukua yale maji yaliyondani ya ile nazi ukayatumia kwa matumizi mengi, kisha ile nguta(nyama ya tunda la nazi nyeupe) unaweza itumia kwenye mboga, au kuzalisha mafuta au jambo lolote ile, kisha kifuu unaweza kukitumia kama kuni, mapambo, au dawa ya mbu, mwisho nazi nyingine ukaifanya kuwa mbegu.
Sasa wengi tukishapata nazi tunatupa kifuuu, machicha, na wakati mwingine maji ya ndani ya nazi. wakati vyote vinakazi.
Hii ipo hata kwa waliofanikiwa, unaweza mtu ukafanikiwa ukapata pesa lakini kwenye matumizi ndipo mziki ulipo. Pesa inamatumizi mengi, lakini kazi kubwa ya pesa ni kuleta pesa. Kwani 90% pesa huvuta pesa, kisha 10% akili huvuta pesa. Sasa ukiitumia pesa kukupa starehe, kukupendezesha kaa ukijua pesa hiyo haitadumu. Watu wengi waliofanikiwa walipopata pesa waliitumia kuvuta pesa zaidi, na sio starehe, burudani na mambo ya anasa. Baadaye walipozipata zikawa nyingi ndio wakaanza kuzitumia kwa matumizi mengine.
Matajiri 90% ni wabahili au wachumi. Hiyo ni sifa inayowaunganisha. Sio rahisi ule hela ya tajiri kiholela. Ukiona Tajiri kakupa milioni moja basi jua anazo kama hizo mara mia moja. Au ukiona kakupa milioni moja basi jua kwako atapata milioni kumi. Ukiona anakulipa lakini ujue kwako anapata milioni moja. Pesa yake yaani laki aliyokupa inavuta laki tisa nyingine.
Naomba niishie hapa, kama imekupendeza waweza kutoa
maoni yako.
Kumbuka; Tunda lenye gamba laini haliwezi kuwa kubwa alafu likawa kwenye mti mrefu, kwani siku litakapoiva likianguka litapasuka. Lakini tunda lenye gamba gumu kubwa ndio hukaa kileleni kwenye miti mirefu ili hata likianguka kamwe halitapasuka
Ulikuwa nami;
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa Dar es salaam