PLEASE DON'T MOVE IT IS NOT APRIL FOOL JOKE PLEASE DON'T
*Fagio kuwapitia Makamba, Membe, Mkuchika
*Lukuvi, Jack Mwambi, Chiligati kurithi mikoba
*UVCCM wamtajia JK mawaziri 9 wanaosaka urais
KUNA siri nzito ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayofanyiwa kazi kwa uangalifu na unyeti wa aina yake, ambayo ikihitimishwa yatatokea mabadiliko ya kutisha ndani ya chama hicho.
Mwezi Aprili, utakuwa mwezi wa kusuka au kunyoa kwa CCM, ambapo ndani ya mwezi huu, baadhi ya viogozi wa Sekretarieti ya CCM wanapaswa kuwa wamefunga virago vyao tayari kuondoka, kwani litapita fagio la chuma.
Hoja inayojadiliwa kwa sasa, ni pangua pangua ya nafasi za juu za wajumbe wa Sekretarieti, ambapo kuna kila dalili kuwa Mzee Yusufu Makamba, ameomba kupumzika na kuwaachia kazi hiyo damu mpya, hali itakayowalazimu kufanya mabadiliko si zaidi ya Aprili.
Vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM vitakavyofanyika Aprili, mwaka huu, vinaelezwa kuwa vitafanya mabadiliko mazito ndani ya chama, kwa nia ya kurekebisha makosa yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba, mwaka jana.
Majina yanayotajwa kumrithi Makamba, ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM mcheshi na mwenye nahau na semi za kila aina, ni matatu. Mbunge wa Isimani (CCM), William Lukuvi, anapewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Makamba.

Yusuph Makamba
Wengine wanaotajwa kwa kiwango ambacho si cha kubezwa ni Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Kapteni Jack Mwambi na Katibu wa sasa wa Uenezi na Itikadi, Kapteni John Chiligati. Mweka Hazina wa CCM, Amos Makala, ambaye ni Mbunge wa Mvomero (CCM), ishara zinaonyesha kuwa atarithi mikoba ya Chiligati kwa kupewa kitengo cha Uenezi na Itikadi. Haikujulikana mara moja nafasi anayoishikilia itakwenda kwa nani. Hapa wanalenga kutoa fursa kwa damu ya vijana kukinadi chama mara nyingi kadri iwezekanavyo.
Mawaziri wenye nyadhifa kwenye Sekretarieti ya Halmashauri Kuu; ambao ni Bernard Membe, ambaye anasimamia Idara ya Kimataifa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Kapteni George Mkuchika, hawa wanatajwa kupumzishwa.
Inaelezwa kuwa umefanywa uamuzi wa makusudi kuhakikisha wajumbe wa Sekretarieti wote hawapewi majukumu mengine ya kiserikali, hali itakayowapa muda wa kutosha kufanya shughuli za chama tofauti na hali ilivyo sasa.
Kwa upande mwingine, uongozi wa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umempelekea Rais Jakaya Kikwete waraka wenye siri nzito ambazo zinadaiwa kujadiliwa katika kikao cha Baraza Kuu la jumuiya hiyo kilichomalizika Jumapili iliyopita mjini Dodoma.
Vyanzo vyetu vya habari vinasema pamoja na Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Beno Malisa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu kilichojiri katika Baraza hilo, kuna masuala mengi nyeti yaliyojadiliwa ambayo hakuyatolewa ufafanuzi kwa kuwa hakutaka kuyaanika hadharani kabla ya ujumbe huo kumfikia Rais Kikwete.
Kwa mujibu wa habari zilizoifikia Rai, waraka huo unatokana na sehemu ya maazimio mazito zaidi yaliyofikiwa na Baraza hilo, ambayo wajumbe walikubaliwa yasizungumzwe hadharani kwa kuwa yalilenga kutoa ushauri kwa Rais Kikwete juu ya uendeshaji wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ingawa haijaweza kufahamika kwa uhakika nini kilichomo ndani ya waraka huo, ambao ulitarajiwa kuwasilishwa kwa Rais Kikwete na uongozi wa UVCCM makao makuu pamoja na Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, habari kutoka vyanzo mbalimbali vya habari zinasema vijana hao wameeleza namna baadhi ya viongozi ndani ya Serikali na katika chama, wanavyochangia kuzorotesha harakati za kukiimarisha chama kwa wananchi.
Kingunge ndiye aliyechaguliwa na Baraza Kuu la UVCCM la Dodoma kuwa Kamanda wa jumuiya hiyo, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na marehemu Mzee Rashid Kawawa, aliyefariki dunia jijini Dar es Salaam Desemba 31, 2009.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alipoulizwa kuhusu waraka huo wiki hii, alikanusha kuwapo kwake, akisema kila kitu kilichozungumzwa katika mkutano wa Baraza Kuu, kilifafanuliwa kwa waandishi wa habari.
Hakuna waraka kama huo, kila kitu kilichoamuliwa na Baraza Kuu kilizungumzwa katika mkutano na vyombo vya habari. Hakuna cha kuficha. Hata kama kuna waraka maalum kwa Rais Kikwete tungewaambia upo, lakini tusingewaeleza kilichomo ndani, alisema Shigela, ambaye pia alikiri kuwa Kingunge sasa ndiye ameshikilia rasmi mikoba ya marehemu Mzee Kawawa.
Inaelezwa kwamba moja ya mambo aliyoambiwa Rais Kikwete katika waraka huo ni namna baadhi ya mawaziri wanavyohangaika katika kampeni za kujenga mitandao yao kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kusahau kabisa jukumu lao kubwa la kumsaidia Rais kutekeleza ahadi zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 2010.
Vyanzo vyetu vya habari vinasema pamoja na mambo mengine kwamba, UVCCM inamshauri Rais Kikwete katika waraka huo kuwatema mawaziri hao ili waendelee na mipango yao ya kujenga mitandao ya uchaguzi wa 2015 badala ya kuendelea kuikwamisha Serikali katika kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.
Inaelezwa kuwa mawaziri hao wametajwa kwa majina kuthibitisha namna mawaziri hao wanavyotumia rasilimali za Serikali kujijengea mitandao yao ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rai iliwahi kuandika katika matoleo yake ya nyuma namna baadhi ya mawaziri wanavyohaha katika maeneo mbalimbali mikoani, wakijenga mitandao yao ndani ya CCM nyakati za usiku wanapokuwa katika ziara za kiserikali, badala ya kuumiza vichwa kutatua matatizo mengi yanayowakabili wananchi.
Ilielezwa katika habari hizo kwamba mawaziri tisa wanaofanya ziara mikoani, wamekuwa wakitumia ziara hizo kujenga mitandao yao na marafiki zao kwa kufanya vikao vya kampeni ndani ya chama nyakati za usiku badala ya kufuatilia majukumu mazito yaliyowapeleka katika ziara hizo.
Waraka huo haukuwagusa mawaziri peke yao, bali pia umeeleza namna Kamati Kuu ya CCM inavyoshindwa kumshauri Mwenyekiti katika masuala mbalimbali mazito yanayolikabili taifa, huku wakitaka mabadiliko makubwa yafanyike ndani ya chombo hicho.
Haikuweza kufahamika mara moja iwapo suala la kujiuzulu kwa Sekretarieti ya chama hicho inayoongozwa na Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, limo katika waraka huo, unaoelezwa kuwa ni mkali kuwahi kutolewa na UVCCM kwa kiongozi wa nchi.
Kwa wiki kadhaa sasa, vyombo vya habari vimekuwa vikiandika kuhusu azma ya kujisafisha kwa CCM kutokana na matokeo mabaya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana uliosababisha chama kipoteze majimbo mengi yaliyokuwa ngome yake, huku vikieleza kwamba moja ya njia za kujisafisha ni pamoja na kuunda upya Sekretarieti ya chama hicho.
Hata UVCCM Mkoa wa Pwani pia walionyesha kuunga mkono hoja hiyo, pale Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Mkoa, Abdallah Ulega, alipoitaka sekretarieti hiyo ijuzulu kwa madai kwamba ndiyo iliyokuwa ikivujisha siri na mikakati ya chama kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na kushindwa kumshauri vizuri Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.
Inaelezwa kuwa Baraza Kuu la UVCCM liliitishwa kutoa mapendekezo yake kwa Mwenyekiti kabla vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa vya chama hicho vinavyotarajiwa kukutana katika siku za karibuni, havijakaa.
Vikao hivyo ndivyo vinavyotarajiwa kufanya maamuzi kadhaa mazito baada ya kupata taarifa ya tathmini ya Uchaguzi Mkuu kutoka katika maeneo mbalimbali ya nchi inayofanyika kutokana na agizo la Rais Kikwete katika kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya CCM yaliyofanyika mjini Dodoma Februari 5, mwaka huu.
Katika mkutano wake na waandishi Jumapili iliyopita, Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Malisa, alieleza namna Baraza Kuu pamoja na mambo mengine, lilivyopitisha azimio la kujipanga upya katika nyanja zote, ikiwamo uanachama, uongozi, maadili, uimarishaji kiuchumi na kiitikadi kwa lengo la kuboresha zaidi muundo wa jumuiya hiyo.
Kutokana na uzito wa kazi hiyo, baraza hilo liliteua kamati maalum, itakayokuwa chini ya mjumbe wa Baraza Kuu, Hussein Bashe, ambayo itafanya uchambuzi yakinifu wa namna ya kuifanyia mabadiliko jumuiya hiyo na kisha kuwasilisha mapendekezo yake katika vikao vya maamuzi vya UVCCM.
Mbali na Bashe, wajumbe wengine wa kamati hiyo walitajwa kuwa ni Riziki Pembe, Fadhili Ngajilo, Zuberi Bundala, Rogers Shemelekwa, Daud Ismail, Ashura Sengondo na Athony Mavunde.