tpaul
JF-Expert Member
- Feb 3, 2008
- 24,225
- 22,632
WAKATI wanachama wa Yanga wakiwa hawafahamu wanakwenda kujadili kitu gani katika mkutano mkuu wa klabu hiyo keshokutwa Jumamosi, rekodi za bilionea kijana Afrika, Mohammed Dewji zimeibua hofu katika klabu hiyo yenye makao yake makuu katika makutano ya mtaa wa Jangwani na Twiga, Kariakoo.
Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kuwa MO amewahi kuidhamini Simba kwa awamu mbili tofauti ambapo ni kati ya mwaka 1999-2001 na kisha 2001-2004 kipindi ambacho Yanga ilipotea kabisa kabla ya kuja kupata afueni baada ya MO kuondoka.
Katika udhamini wa kwanza wa miaka miwili MO aliwapa Simba sh 900 milioni kabla ya baadaye kutoa Sh 1.5 bilioni katika udhamini wa pili uliomalizika mwaka 2004.
Rekodi zinaonyesha kuwa wakati MO anaingia Simba mwaka 1999, timu hiyo ilikuwa imetoka kukaa miaka minne bila kutwaa taji lolote la Ligi Kuu Bara ambapo ubingwa wao wa mwisho ulikuwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 1995, ambapo pia mwaka huo ilitwaa ubingwa wa Kombe la Tanzania (Tanzania Cup).
Katika kipindi cha miaka yake mitano ya udhamini ndani ya Simba, timu hiyo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu wakati watani wao Yanga waliambulia patupu. Simba ilitwaa ubingwa huo mwaka 2001, 2002 na 2004 huku Mtibwa Sugar ikitwaa mara mbili 1999 na 2000.
Katika kipindi hicho Simba ilitwaa pia ubingwa wa Kombe la Tusker mara tatu mwaka 2001, 2002 na 2003 na Kombe la Kagame 2002 ambapo ilikuwa imelikosa tangu mwaka 1996.
Katika kipindi hicho Simba ilitamba Afrika na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia jambo ambalo liliishtua Yanga ambayo ilionekana kumbwelambwela na kupoteza muda tu nchini.
Katika hatua hiyo ya makundi Simba ilikusanya pointi saba ambazo hazijawahi kufikiwa na timu nyingine ya Tanzania ambapo, Yanga mwaka huu mbali na kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ina pointi moja tu mpaka sasa ikiwa imecheza mechi nne.
Hata hivyo, licha ya rekodi hiyo ya kuvutia ya MO bado kumekuwa na hali ya sintofahamu Msimbazi juu ya uwezekano wa kuruhusu bilionea huyo kumiliki asilimia 51 ya hisa ama chini ya hapo kwa hofu ya kuweka maamuzi yote ya klabu katika mikono ya mtu mmoja.
MATAJIRI WAUNGANA
Katika hatua nyingine matajiri Said Salim Bakhresa na Mohammed Dewji ‘MO’ wameonekana kuungana kuongeza nguvu ndani ya Simba huku kila mmoja akipitia njia yake.
Azam ambayo inamilikiwa na Bakhresa imeipa Simba nyota wawili ambao ni kipa Mwadini Ally na straika Ame Ali huku MO Dewji akiipa timu hiyo ya Msimbazi Sh 100 milioni kwaajili ya kufanya usajili.
Mwadini na Ame tayari wametua kambini mjini Morogoro kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kikosi kinachonolewa na Mcameroon Joseph Omog.
Chanzo: Mwanaspoti