Mohamed Ali: Barua kwa Duale, Moses Kuria, Mutahi Ngunyi na wenzao

Mohamed Ali: Barua kwa Duale, Moses Kuria, Mutahi Ngunyi na wenzao

Ab-Titchaz

JF-Expert Member
Joined
Jan 30, 2008
Posts
14,630
Reaction score
4,253
Mohamed Ali: Barua kwa Duale, Moses Kuria, Mutahi Ngunyi na wenzao

Je, wataka kuwa maarufu Kenya? Ni rahisi kabisa - unga viongozi pamoja na serikali mkono.

Bora wakishuta wasifu kwa kusema ni harufu ya marashi, walimbikizie sifa wakituhumiwa kuiba, sifu kabila zao na wake zao, heshimu maamuzi ya mipango yao ya kando serikalini.

Ukifanya hivyo, bilashaka utaogopewa na kila mtu kwani sheria yao itakukinga.

Ukipenda, fungua hospitali kisha uwabake wanawake wanaotafuta matibabu, simama kwenye jukwaa na useme kabila fulani likatwe kwa upanga likipinga mwito wa serikali iliyo madarakani, watusi kwa kuwaita maskini baada ya serikali hiyo hiyo unayoabudu kuwafilisi raia wake, kuwa mbunge na ubake ndani ya ofisi yako kwani sheria ni ya mama zenu si yetu sote, tena waite viongozi wadini kwa kigezo cha kuombea taifa baada ya kufanya maasi kwa wananchi wako, cheza na jina la Mungu kila kukicha kwani mungu wako ni senti, simama imara na serikali kisha vunja sheria. Hakika utalindwa.

Kenya hamna sheria. Wakenya watakumbuka jinsi mahakama ya Willy Mutunga mnamo mwaka wa 2013 ilivyotoa uamuzi wa dakika tatu dhidi ya kesi ya uchaguzi iliyo wasilishwa na upande wa Cord. Ndio, dakika tatu! Sisemi majaji hao walikosea, bali kutoa maamuzi ya taifa kwa dakika tatu ni sawia na kutwanga maji kwenye kinu.

Daktari Willy Mutunga sasa kiza kinene kimetunga mithili ya ukungu. Haiheshimiwi tena, ni sawia na simba wa matopeni anayeteleza ovyo ovyo. Wakenya waliheshimu maamuzi yenu, lakini sasa waliotangazwa washindi hawaheshimu maamuzi mliotoa kuhusu waalimu.

Moses Kuria

Sitaki kumwita mheshimiwa kwani vitendo vyake na matamshi yake si vya kiheshimiwa. Waliomchagua na wamwite mheshimiwa, mimi simo. Kumbuka nchi hii itakapoteketea kwa sababu ya matamshi kama yako, hata shetani hatakuwa na wasaa wa kusikia umaarufu wako wa kuwatenganisha Wakenya. Iko siku haki itashinda na hiyo ndio siku utakapojua tofauti ya kuvua chupi na kuvua samaki.

Mutahi Ngunyi

Sisi ni maskini. Tumesalitiwa na serikali, tumeibiwa na kudhalilishwa na hiyo hiyo serikali unayoabudu. Lakini, kumbuka aliyekupa wewe ndiye aliyeninyima mimi. Itakuwaje Mutahi atutusi kisha atualike kunywa pombe naye? Kumbuka dawa ya maskini si pombe, bali chakula. Kama wataka kufanya ukuruba na sisi, iambie serikali ipunguze bei ya vyakula ikiwemo maziwa ili watoto wetu wafaidi. Pia serikali ambayo unaitetea sana, iambie maafisa wake waache kutumia nguvu za bunduki kuwaua vijana ovyo ovyo, na maafisa wakome kupora mali ya umma. Usisahau kueleza kuhusu walanguzi wa dawa za kulevya, sio kuwahangaisha wateja. Pitisha ujumbe kuwa vijana hawana ajira na uchumi umezidi kuzorota - shilingi ya Kenya imefika 107 dhidi ya dola ya Merekani.

Ukifikisha salamu hizi, basi sisi maskini hatutaki pombe yako, hatutaki kuleweshwa kisha mali yetu kuibiwa tukiwa ulevini. Sisi hatuna kinyongo nawe, lakini tutakusamehe na umaskini wetu kwani sisi ni maskini lakini wakubwa kimapenzi moyoni.

Aden Duale

Juzi nilikuona ukijipiga kifua na kutetea viranja wa Jubilee na kusahau wana-Garissa hawana vitambulisho, vijana wanatekwa nyara na watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa polisi na kuuawa, hamna waalimu Garissa na Mandera. Mtihani unabisha hivyo jitayarishe kuwa na vizazi visivyo na elimu kwa sababu umefeli kuwashughulikia waliokuchagua na badala yake kupiga domo ukiitetea serikali.

Kipchumba Murkomen


Ni hatari sana msomi anayefahamu sheria kwenda kinyume na sheria. Kumbuka kuwa siasa sio mchezo mchafu, bali mtu binafsi ndiye mwenye siasa chafu. Kuwa kibaraka sio dhambi, lakini kujidhalilisha ndio dhambi kuu. Tumewaona wanasiasa wengi, makalulu na wenye vihoja chungu nzima. Leo hawapo tena. hata chama ambayo kwao ilikuwa kama baba na mama haipo tena.

Kumbuka, wanaotawala sasa ni Wakenya kwa nguvu za Rabuka ambaye leo kila mtu anacheza na jina lake.

Mbona sikukuona ukiwaombea waliouawa na wakimbizi wa ndani kwa ndani? Mungu atatulipia sisi wanyonge, Mungu atasikia maombi yetu na ya wale waliouawa mwaka wa 2007. Hatutaombea kabila hili wala lile, bali tutaombea makabila yote kwa maana sisi twaabudu Mungu aliye mkuu. Kipchumba Murkomen Mungu ni mkuu.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha upekuzi KTN.

Wasiliana naye kupitia thenairobian@standardmedia.co.ke ama mali@standardmedia.co.ke. Unaweja pia kujumuika naye katika mitandao ya kijamii - Facebook: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: Mohajichopevu


http://www.sde.co.ke/thenairobian/a...-moses-kuria-mutahi-ngunyi-na-wenzao?pageNo=2
 
Ali is just another aspiring politician, his bias is discernible through his veins
 
https://www.facebook.com/permalink.php?story_fbid=10154244473464056&id=781769055

BARUA KWA WILLIAM RUTOHujambo bwana kusema na kutenda. Naomba safari hii kabla hujatenda nikujulishe mawili hivi. Najua huna raha, hupati usingizi na unahofia maisha yako licha ya utajiri uliyonayo. Leo hii umejipata kubanwa na uliowaamini. Ndoa za haraka na tama zina shida bwana Ruto. Ukipenda viazi usiogope mimba ndio msemo wetu kule vilima vya raha. Ndoa yako na Uhuru Kenyatta imefikia kiwango cha mtu mmoja kati yenu kupata mimba.

Si mimba ya mtoto bali mimba ya machungu na kusalitiana. Miaka ya nyuma kabla ya wewe kuwa HUSTLER wa kizazi kipya niliwahi kukutembelea mara kwa mara katika afisi zako katika jumba la Transnational. Tulizungumza na kutaniana na hata kuzungumza kwa simu. Ulikuwa machachari na mtu wa watu. Mwaka wa 2007/ 2008 baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wewe na Raila mlikuwa chanda na pete mkijaribu kuunda serikali ya muungano na kupigania nafasi ya ukubwa wa wana odm katika serikali hiyo iliyowaibia kura. Katika pilka pilka hizo usaliti wa hali ya juu ulitendeka. Wabakaji wa demokrasia walianza kunoa kisu huku nyinyi mkidhani mambo yalikuwa yashakwisha. Baada ya kufanyiwa unyama na PNU nilidhani mmejifunza mawili kuhusiana na ndoa za kipumbavu.

Lakini naona mlisahau kuwa ukila na kipofu kuwa mwangalifu kwani akikosa nyama atakushika mkono. Sasa nahofia chakula cha jubilee kimeisha na vipofu wote wanataka kukushika wewe mkono uwe kitoweo chao cha mwisho. Hamna anayekupenda, wewe ulikuwa chombo, chombo cha kuwavukisha wao kutoka masaibu yao. Kila mwenda kwa mganga lazima atoe kafara na kafara ni wewe. Nahofia utafungwa ama utakuwa mkimbizi wa ndani kwa ndani na ndio hio siku utajua masaibu ya kuishi kama wakimbizi wa ndani kwa ndani mwaka wa 2007/8.

Utakuwa huna raha, utadhalilishwa, utakuwa mnyonge bila haki na hatimaye utakuwa huna maana kwa serikali ya TNA. Wacha niseme TNA kwa sababu URP haina usemi tena. URP imebakwa peupe wazi wazi, URP inalea mimba haramu, mimba ya kujitakia. William Ruto usidanganywe na maombi za kinafiki zinazotekelezwa na wafuasi na maadui wako. Kama unataka kutatua shida zako binafsi na maombi tasa pole. Maombi ni ya kuondoa usinzi, wanaofumaniwa na wake za watu, mapepo na kumshukuru mungu na kumwogopa. Sio safari za mahakamani. Ruto, imefika wakati wa kucheza karata yako ya mwisho.

Katika kucheza kwako jiepushe na Adan Duale na Kipchumba Murkomen hawa wawili ni wajuzi wa ligi za kitoto au wacha niseme ligi za mchezo wa tufe( mpira wa karatasi) unaochezwa na watoto. Hawatokusaidia ila watazidi kuongeza kuni kwenye moto. Moses Kuria anafanya yanayofanywa na Duale na Kipchumba ndani ya TNA sasa moto umewaka na ni sharti chakula kipikwe. Kabla wakupike janjaruka. Kenya imekuwa taifa la kuzalisha wanafiki na watu waoga. Tumekubali ukiritimba itawale.

Profesa hana tofauti na mtoto wa darasa la kwanza. Jiepushe na wanaokuzunguka na kujifanya wasomi ila ni watu wa maslahi. Maji tayari yamemwagika lakini ni wewe kuamua mkondo wa maji hayo. Huna budi kurudi kwa marafiki zako wa zamani kwani tayari wakenya washajua kikulacho ki nguoni mwako. Kwa maoni yangu binafsi na naomba unikosoe ni wewe kujiondoa mara moja kwenye muungano wa kinafiki. Warudie uliowakosea na uombe msamaha hakika Mungu anatuamrisha kuwasamehe maadui.

Najua ni aibu kwako lakini kumbuka una familia. Aidha usiwahi kuwaona ama uishi bila ya kuwaona. Uamuzi umo mikononi mwako. Kuna uwezekano wa kujifunza na haya na kuamua kuunda muungano wa ukombozi wa tatu kina nyinyi mkiwa nyuma muwaachie vijana usukani. Kuna ile kadi moja ya mwisho ya wewe kuwatumia wana URP kupasisha mswaada na wana CORD wa kumwondoa Uhuru Kenyatta mamlakani kwa wingi wa kura bungeni lakini kwa yale umewafanyia wakenya miaka mitatu sioni kama CORD itakubali uwe Rais kwa miaka miwili iliyosalia kwa mujibu wa katiba ya Kenya. Bwana Ruto huu ni wakati wako wakuwaza na kuwazua.

Tunazo changamatoto zinazotukabili kama taifa. Badala ya kukaa na kujiuliza kwa nini tuko hapa na tutatoka vipi, tunakaa na kuongea mambo ya kinafiki na ukabila. Akili ndogo kutawala akili kubwa. Watu wenye akili kubwa wanaweka akili zao mfukoni kwa sababu ya ushabiki wa kivyama badala ya kukaa na kutatua matatizo ya wakenya. Bunge limekuwa bunge la kitototo. Wakenya sasa wanataka bunge la mapinduzi. Badala ya kuwazomea wakenya waskilizeni. Deni la Kenya linazidi kuongezeka. Kila mkenya anadaiwa hata mimba inadaiwa. Ndio taifa tuliyonayo sasa. Williama Samoei Arap Ruto huna la ziada sasa.

Tayari chama chako na uongozi wako umebakwa ki-demokrasia. Waswahili wanasema mimba ya mwanaharamu huingia mara moja ya pili ni kusudi. Je, ulisahau mimba ya mwaka wa 2007? Kwa nini umekubali mimba nyengine mwaka wa 2013? Umechezewa shere tangu na mwanzo wa ndoa yenu ya vichochoroni. Huna sura sasa, wakenya hawatokukubali tangu watoto wao wapigwe na vitoa machozi wakipigania uwanja wa shule yao ya msingi wa langata. Huna sura tena, ufisadi umekuwa jina lako la pili. Wakenya hawakuamini tena. Iwapo ulijikakamua na kuwasaidia wakenya tangu mchukue uongozi leo hii wangekusitiri na kukupokea lakini ulisahau kuna kupanda na kushuka. Leo zamu ya kushuka kukutana na sisi kina yahe.

Hatutakudhulumu wala kukuita majina, sisi tutaoongozwa na dini na hekima. Karibu nyumbani lakini kumbuka sisi hatuna nguvu za kukusaidia maana sote ni maskini kama mlivyotufanyia mlipokuwa masimba. Mlitufanya maskini kwa kutudhulumu na uongozi wenu wa kusema na kuenda. Leo bwana Ruto hakuendeki. Huna budi kumkumbatia Raila Amollo Odinga na kumwomba msamaha kwa semi zako za chuki dhidi yake. Akufaye kwa dhiki ndiye rafiki. Kumbuke hata simba ni mkali lakini hutiwa mimba. Kuwa na ijumaa njema. Ni mimi rafiki wako wa zamani, Mohammed Ali.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN.Kuwasiliana naye: mali@standardmedia.co.ke, FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu
TWAOMBA RADHI.

Katika makala ya wiki iliyopita ( kuna serikali kweli Kenya ), tulisema kuwa tangu jubilee iingie mamlakani, wakenya zaidi ya laki tatu wamepoteza maisha yao kutokana na hali mbaya ya usalama. Tungelipenda kusahihisha na kusema kuwa tulikuwa tukimaanisha watu zaidi ya 300
 
Back
Top Bottom