Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Mzee Mohamed Omari Mkwawa au kwa jina lingine Tindo alilopewa na Karume wakati wa harakati za ukombozi Zanzibar katika miaka ya 1950 amefariki dunia usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili tarehe 5 May 2015 nyumbani kwake Mwahako Tanga.
Marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho Jumatatu Tanga mjini. Mzee Mkwawa alipata umaarufu mwaka 2010 baada ya kutoka kitabu cha Dr. Harith Ghassany, “Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,” kitabu kilichokuja kueleza historia ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa usahihi kuliko vitabu vyote vilivyopata kuandikwa kabla.
Ilikuwa Mzee Mkwawa ndiye aliyefichua siri kubwa iliyokuwa imefichwa kwa miaka mingi ya jeshi la askari mamluki wa Kimakonde waliochukuliwa kutoka mashamba ya mkonge ya Sakura wakapewa mafunzo katika mapori ya Kipumbwi na kuvushwa kwenda Zanzibar kusaidia mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964.
Mzee Mkwawa ndiye alikuwa akilivusha jeshi hili kwa majahazi kutokea Kipumbwi kwenda Zanzibar usiku wakiwa wamevaa mavazi kama wavuvi. Mzee Mkwawa alikuwa na mchango mkubwa katika kutegua kitendawili cha mchango wa Tanganyika katika Mapinduzi ya Zanzibar kiasi mwandishi Dr. Ghassany alipatapo kusema kuwa, "Ufunguo wa kitabu changu anao Mzee Mkwawa."
Hii picha ya pili hapo chini akiwa na Prof. Malima ni picha yangu ya kwanza kumpiga Mohamed Omar Mkwawa wakati wa kampeni za uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995.
Mzee Mkwawa wa kwanza kushoto amevaa picha ya mgombea wa CUF Ibrahim Lipumba, Juma Duni Haji na Ibrahim Haruna Lipumba.
Hapa ni Ngamiani Tanga nyumbani kwa Mama Ummie bint Anzuani. Ilikuwa baada ya mkutano mkubwa sana Viwanja vya Tangamano ambao haujapata kutokea.
Mama Ummie mmoja wa viongozi wa juu wa CUF alitualika chai nyumbani kwake. Wakati ule sikuwa namjua Mzee Mkwawa baada ya miaka miwili 1997 ndipo tulipokuja kufahamiana wakati nilipohamia Tanga.
Hii picha nimempiga Mzee Mkwawa tarehe 29 Oktoba 2013 na ndiyo ilikuwa mara yetu ya mwisho kuonana.
Huyo nyuma ni mkewe.
Nilikwenda nyumbani kwake Tanga na mtafiti wa Kimarekani aliyetaka kufanya mahojiano na yeye.
Hili unaloona ni banda la kuku nyuma ya nyumba ya muhisani mwema ameligeuza kuwa makazi yake.
Mzee Mkwawa katika mazungumzo yetu na ndiyo yalikuwa ya mwisho baina yetu aliniambia, "Hivi kweli Mohamed katika kujitolea kwangu kote katika Mapinduzi ya Zanzibar ijaza yangu ndiyo hii mimi na mke wangu kulala kwenye banda la kuku?"