Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Jicho la camera siku zote linahifadhi kile jicho la binadamu lilishuhudia.
Katika utafiti wa historia ya TANU niligundua kitu kimoja.
Ile kamati ya ndani, ndani ya kamati kubwa wale watu watano hawa ndiyo walikuwa New Street TANU Office Dar es Salaam: Mzee John Rupia, Abdul na Ally Sykes, Dossa Aziz na Julius Nyerere wakipendana sana.
Hamza Mwapachu hapo yuko ''jela'' kisiwani Nansio, hawa wakipendana sana na wale watu waliokuwa pembeni yao ndani ya TANU waliwapa majina ya utani.
Abdul wakimwita, ''The Sweet Abdul Sykes,'' kwa ule ukarimu wake na Dossa, ''The Bank,'' kwa ajili ya utajiri wake.
Mzee Rupia bila shaka kwa ule utu uzima wake hawakuweza kumfanyia maskhara kiasi cha kumpachika jina.
Nyerere baadae na yeye akapachikwa jina na Bi. Titi katika mkutano wa hadhara akasema, ''Huyu ni Mwalimu,'' akiwa na maana Nyerere atawasomesha Waingereza na Gavana Twining wao siasa katika kupambananao na toka siku ile jina likashika.
Mwalimu akaingia na jina hili kaburini.
Alikuwapo mwalimu Steven Mhando lakini TANU hata siku moja hawakumwita kwa jina hilo.
Siku hizo Julius Nyerere alikuwa akivuta sigara.
Kwenye meza yake pale meza kuu kama wako kwenye dhifa Ukumbi wa Arnautoglo au wapi wakimwekea pakiti ya sigara na kibiriti.
Nyerere alikuwa akivuta, ''Pall Mall Cigarettes,'' sigara za Kimarekani zikipendwa sana na vijana watanashati wa mji wa wakati ule.