Madiwani wataka Magufuli ajiuzulu
2007-02-17 11:03:18
Na Frank Mbunda
Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam, wamemtaka Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Bw. John Magufuli, kujiuzulu kutokana na kile walichodai aliingilia mamlaka ya manispaa hiyo kutoa hati kwa mmiliki wa mgahawa wa Rose Garden.
Wakizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika jana chini ya Meya wa Manispaa hiyo, Bw. Salum Londa, madiwani hao walisema hatua ya Waziri Magufuli ni sawa na upuuzwaji wa mamlaka nyingine za serikali.
Madiwani waliotoa hoja ya kumtaka Waziri Magufuli aachie ngazi ni Diwani wa Kata ya Kimara, Bw Mohammed Mringo, Diwani wa Kata Kibamba, Bw Ignas Mwitula, Diwani wa Kata ya Makuburi, Bw Busee Gigabase na Diwani wa Kata ya Mabibo, Bw Kassim Lema.
Aidha, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Bw Londa pia aliwaunga mkono Madiwani hao.
Diwani wa Kata ya Kimara, Mringo alisema hatua ya Waziri huyo kuruhusu kutolewa hati ya umiliki wa eneo hilo, ni sawa na kuwapuuza madiwani waliozuia eneo hilo la barabara kutumiwa kama makazi na biashara.
?Mheshimiwa Meya na Mwenyekiti, hapa inaonekana kuna aina fulani ya matusi, sisi ni madiwani katika mamlaka halali kwa mujibu wa sheria, lakini hapa tumedhalilishwa na Waziri wa Ardhi, alisema Bw. Mringo.
Diwani huyo alisema kwamba baraza hilo linapaswa kutoa tamko kali la kulaani uamuzi wa kupuuzwa kwa madaraka na mamlaka yake kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Manispaa hiyo, hatua iliyochukuliwa na Waziri huyo.
``Hivi kwa nini sisi kama madiwani tunaweza kukaa katika vikao kama hivi humo ndani kwa dhamana kubwa kutoka kwa wananchi waliotuchagua, tukamua kwa mujibu wa sheria kuzuia jambo lakini baadaye tukapingwa na kudharauliwa kiasi hiki,`` alisema Bw. Mringo.
Diwani wa Kata ya Kibamba Bw. Ignas Mwitula, alilalamikia hatua hiyo na kuifafanisha na uchokozi kwa mamlaka halali na kutaka Waziri huyo aifute hati aliyoitoa au ajiuzulu wadhifa wake.
``Msimamo wetu sisi madiwani wa Manispaa ya Kinondoni ni kumtaka Waziri Magufuli kujiuzulu nafasi aliyonayo hivi sasa, au aifute hati aliyoitoa, kwani ni kinyume cha sheria na taratibu,``alisema Diwani Mwitula.
Madiwani wengine waliochangia suala hilo na kusisitiza kumtaka Waziri Magufuli kuitema nafasi hiyo ni Bw. Lema, wa Kata ya Mabibo na Bw. Busee Gigabase wa Kata ya Makuburi.
Madiwani hao kwa pamoja walisema kitendo cha wizara kutoa hati kwa mmiliki wa mgahawa huo ni sawa na kuingilia uhuru, kulinyima au kuliondolea haki baraza la madiwani kushughulikia masuala ya ndani.
``Sina hakika kama tunaweza kutembea kifua mbele kama Madiwani, kwani tayari tunapanga jambo hapa, Waziri na mamlaka nyingine zinaingilia jambo hilo na kusitisha kasi yetu,`` alisema Bw. Lema.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Hassan Kattanga, alisema ndani ya kikao hicho kuwa watendaji wake wanashindwa kutekeleza azma ya kuvunja mgahawa huo, kutokana na kinga iliyotolewa na Waziri.
``Tunashindwa kutekeleza yale yaliyofikiwa na baraza la madiwani, kwani inaonekana kuwa yupo pale kihalali, amepewa hati na wizara``, alisema Bw. Kattanga.
Hata hivyo, akionyesha kuunga mkono malalamiko ya madiwani wake Meya Londa, alisema suala hilo limewavuruga watendaji na madiwani wengi na kuanza kuwapotezea heshima.
``Wapo wanaodhani kwamba suala hili lilikuwa likifanywa na Manispaa kwa ajili ya kutisha ili kujipatia kitu kutoka kwa mmiliki huyu, lakini sio kweli, tulifikia uamuzi huo kulingana na taratibu zetu, ``alisema Bw. Londa.
Meya huyo alimuagiza mkurugenzi kuendelea na mkakati wa kuuvunja mgahawa huyo licha ya kuwapo kwa hati iliyotolewa na Waziri, akidai kitendo hicho kimefanywa bila kuishirikisha manispaa na mmiliki hakupewa ofa,`` alisema Bw. Londa.
``Lile sio eneo la biashara wala makazi, kwa hiyo sisi kama mamlaka kamili tutaendelea na utaratibu wetu, hatuwezi kuogopa kwani haya tunayafanya kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu za uendeshaji wa halmashauri,`` alisema Bw. Londa.
SOURCE: Nipashe