TAARIFA KWA UMMA
UKWELI KUHUSU MOROGORO PARALEGAL
Kwamba, habari iliyoandikwa na mwanachama huyo wa Jamii forums aliyejitambulisha kwa jina la Inkognito, hazina ukweli wowote, ni habari yenye lengo la kupotosha umma, kuharibu jina na kazi nzuri inayofanywa na Kituo cha wasaidizi wa kisheria cha Morogoro Paralegal. Kwa msomaji yoyote aliye makini, atagundua kuwa mwandishi wa habari hiyo ameiandika habari hiyo kwa msukumo wa chuki binafsi dhidi ya Bi. Flora Masoy, ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo anayefanya kazi kwa kujitolea (Nitatoa ufafanuzi zaidi hapo baadae).
Katika kujibu yale yaliyoandikwa kwenye habari hiyo, nitajaribu kuonyesha ushahidi unaothibitisha kuwa ndugu "Inkognito" alikuwa na lengo la kupotosha, kuharibu taswira ya Morogoro Paralegal na Kufanya shambulio binafsi kwa Bi. Flora Masoy (Character Assassination), jambo ambalo si la kistaarabu na halipaswi kupewa mashiko hata kidogo.
Histori yangu na Morogoro Paralegal
Nilijiunga na Morogoro Paralegal mwaka 2007 wakati huo nikichukua shahada yangu ya Sheria kutoka chuo kikuu cha Mzumbe. Nilijiunga na Morogoro Paralegal nikiwa kama Mwanasheria wa kituo wa kujitolea na baadae kuwa afisa Mradi wa haki za ardhi katika maeneo ya kifugaji, uliofadhiliwa na shirika la Care International, kupitia program yake ya "Pastoralists Basket Fund". Mradi huo kwa upande wa Morogoro ulitekelezwa katika wilaya ya Mvomero. Hiyo ilikuwa ni mwaka 2008.
Baada ya kumalizika kwa mradi huo, niliendelea kuwa afisa mradi kwa miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na mashirika mbalimbali. Baadhi ya Mashirika ya ufadhili ambayo nimewahi kuwa Afisa mradi nikiwa na Morogoro Paralegal ni pamoja na Family Health International (Fhi-2008-2009) na ActionAid Tanzania (2009-2011). Miradi yote hiyo niliyoisimamia pamoja na miradi mingine iliyokuwa ikisimamiwa na maafisa miradi wengine ilitekelezwa kwa mafanikio makubwa kiasi cha kuifanya Morogoro Paralegal kuwa moja ya mashirika yenye mafanikio makubwa mpaka sasa.
Baada ya kuipitia kwa umakini mkubwa habari aliyoiandika ndugu Inkognito, nimebaini upotoshaji mkubwa katika maeneo yafuatayo:
Historia ya Morogoro Paralegal
Morogoro Paralegal Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria kilichoanzishwa mwaka 1993 na baadae kupata usajili Namba. 39135, kutoka kwa Msajili wa Makampuni (BRELA) february 17, 2000. mwaka 2010 Morogoro Paralegal ilifanya mchakato wa kuhamisha usajili wake kutoka BRELA kwenda kwa Msajili wa Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) na kupata cheti cha Certificate of Compliance No.0000139 mwaka (2011).
Hivyo Basi; Maelezo ya Inkognito kwamba Morogoro Paralegal ni shirika la kifamilia hayana ukweli wowote kwakuwa Sheria na Taratibu za nchi yetu haziruhusu kusajili shirika ambalo waanzilishi wake wote ni wanandugu. Aidha, Morogoro Paralegal ni Shirika lilioanzishwa na watu wasio na mahusiano ya kindugu na baadhi ya Waanzilishi (Founder Members) wa Morogoro Paralegal mpaka leo bado wako hai na wanashirikiana na shirika kwa ukaribu.
Kuhusu Bi. Flora Masoy
Bi. Flora Masoy ni mmoja wa wanachama waanzilishi wa Morogoro Paralegal ambaye chini ya uongozi wake shirika limeweza kujipatia mafanikio mbalimbali hadi leo hii. Robo tatu ya maelezo ya Inkognito yanamlenga Bi. Flora Masoy kama mtu binafsi na si shirika.
Tuhuma dhidi ya Bi.Flora Masoy:
Inkognito ametoa tuhuma kwamba, Bi. Flora Masoy Anawachukia wanasheria na Maafisa Miradi katika shirika lake: Tuhuma hizi si za kweli na zina lengo la kuwagombanisha wanasheria na Maafisa miradi wa Morogoro Paralegal ambao wanatumia muda wao wa kujitolea katika kuhudumia jamii pana inayozunguka mkoa wa Morogoro.
Tuhuma hizo si za kweli kwakuwa Mimi mwenyewe, Amani Mwaipaja ambaye nimetajwa kuwa nimewahi kuwa Mwanasheria wa Morogoro Paralegal mpaka sasa bado ni Mwanasheria wa Morogoro Paralegal na nimekuwa nikishiriki katika shughuli mbalimbali za kituo kwa kujitolea tangu mwaka 2007 hadi hivi sasa. Kama Bi. Flora Masoy angekuwa na Moyo huo basi hata mimi binafsi nisingeweza kufaya naye kazi kwa miaka yote hiyo.
Ndugu Inkognito alipaswa kueleza au kuwataja kwa majina ni wanasheria gani wa kituo hicho ambao ana ushahidi wao kuwa wanachukiwa na Bi. Flora Masoy na sababu za kuchukiwa kwao.
Mwanasheria mwingine ambaye bado anaendelea kujitolea kama Mwanasheria wa kituo hicho ni Theodora Mlelwa. Mwanasheria huyu alianza kazi katika kituo hicho tangu mwaka 2009 na mpaka leo bado ni Mwanasheria wa Kituo hicho. Hivyo basi, hoja ya Inkognito kuwa Bi. Flora Masoy anawachukia wanasheria wake ni hoja ya kitoto na isiyo na maana kwa kuwa Mkurugenzi yoyote wa shirika hawezi kuwachukia wafanyakazi wake wanaojitolea kwa manufaa ya shirika analoliongoza yeye mwenyewe.
Hoja ya Iknognito ya kuwachukia maafisa miradi ni hoja ya kitoto na isiyo na msingi kwakuwa Bi. Flora Masoy, kwa nafasi yake ya Ukurugenzi wa Shirika hawezi kuwachukia watu wanaosimamia miradi ya shirika analoliongoza yeye mwenyewe.
Kwa hili, Inkognito alikuwa na lengo la kujenga chuki miongoni mwa watendaji wazuri, na wanaojitolea katika kufanikisha malengo ya Morogoro Paralegal.
Kuhusu kubadilisha magari
Tahuma za kuwa Bi. Flora Masoy anatumia fedha za mradi ni tuhuma za uongo, na zina lengo la kumchafua tu Bi. Flora Masoy kutokana na sababu zifuatazo:
Bi. Flora Masoy anamiliki gari moja tu aina ya Cresta ambayo aliinunua tangu mwaka 2009 hadi leo hii bado anaitumia gari hiyo hiyo. Isitoshe, kwa umri aliofanya kazi akiwa kama mwalimu (Alianza kazi ya ualimu mwaka 1972 na Amestaafu mwaka 2011), kwa Huduma anayoipata kutoka kwa watoto wake, kitendo chake cha kuwa na gari si jambo la kushangaza kiasi cha Inkognito kulalamika.
Hivyo basi, si kweli kwamba Bi. Flora Masoy anabadilisha magari au kwamba gari analomiliki limetokana na fedha za miradi. Isitoshe, Bi. Flora Masoy anafanya kazi za Morogoro Paralegal kwa kujitolea ambapo kwa sasa analipwa kiasi cha shilingi 150,000/= tu kwa mwezi. Ni wakurugenzi wachache sana mfano wa Bi. Flora Masoy wanaoweza kuwa na moyo wa kumlipa mfanyakazi wake shilingi laki sita au saba au nane wakati yeye mwenyewe analipwa laki moja na nusu.
Kuhusu kukaimu nafasi ya Mkurugenzi
Tuhuma za kwamba Mkurugenzi wa Morogoro Paralegal anapokuwa hayupo ofisi huwa hakuna mtu wa kukaimu nafasi yake si za kweli kwakuwa kila anapokuwa nje ya ofisi Mkurugenzi huyo, kupitia fomu maalum hukaimisha nafasi yake kwa mtu mwingine na shughuli za shirika huendelea kama zilivyo pangwa. Hata suala la kuhodhi nafasi za shirika si za kweli kwakuwa kila mmoja aliyepo ndani ya Ofisi za Morogoro Paralegal ana kazi yake, na hufanya kazi zao kwa kufuata taratibu zilizopo.
Hakuna Wizi wala Usanii wa fedha za Miradi
Inkognito ametoa tuhuma kuwa Bi. Flora Masoy amekuwa akifanya wizi na usanii katika matumizi ya fedha za Mradi. Maelezo hayo si ya kweli. Yana lengo la kumchafua Bi. Flora Masoy na Morogoro Paralegal kwa ujumla mbele ya macho ya wafadhili, wadau wa shirika na wapenda maendeleo wote.
Naamini, pasipo shaka, kuwa, Inkognito hajui masharti na taratibu zinazotumiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali na wafadhili katika suala zima la usimamizi wa fedha za ruzuku. Katika kumwelimisha Inkognito, ningependa kutoa maelezo yafuatayo:
(i). Kwamba, pamoja na ukweli kuwa kila mfadhili huwa na masharti na taratibu zake katika utoaji wa ruzuku lakini lipo jambo moja linalowaunganisha wafadhili wote hao.
Kwanza kabisa, hakuna mfadhili ambaye anaweza kutoa fedha zake kwa shirika asilolijua undani wake, utendaji wake, wahusika wake na ufanisi wa shirika husika ambapo baada ya kujiridhisha huendelea na taratibu nyingine za kuandikiana mkataba wa utekelezaji wa shughuli husika.
Pili, hakuna mfadhili ambaye anaweza kutoa fedha za ruzuku bila kufanya ufuatiliaji wa fedha hizo (Monitoring) na kufanya tathmini (Evaluation) juu ya maendeleo ya mradi husika, mafanikio yake na changamoto zake.
Tatu, pamoja na ufuatiliaji na tathmini zinazofanywa Kuhusu shughuli za mradi husika, bado taarifa za mradi/miradi hiyo huasilishwa kwa wafadhili na wadau wengine wa mradi ili kupitiwa kuona kama zina ukweli au la.
Nne, Morogoro Paralegal imekuwa ikifanyiwa ukaguzi wa mahesabu yake kila mwaka na haijawahi kupata hati chafu Kuhusu ubadhilifu au upotevu wa fedha za shirika ikiwemo fedha za miradi mbalimbali. Taarifa ya hesabu ya mwaka huwasilishwa kwa bodi, wanachama na wafadhili wa shirika kila mwaka, katika hili Morogoro Paralegal, haijawahi kuwa na historia yoyote mbaya ya matumizi ya fedha za miradi.
Kwa kifupi, maelezo ya Inkognito kuhusu wizi, ubadhilifu na usanii Kuhusu fedha za miradi hayana mashiko, yanalenga katika kuwafundisha wafadhili, wakaguzi wa mahesabu na wana taaluma wengine namna ya kufanya kazi.
Kwa mantiki hiyo, anajaribu kuonyesha kuwa yeye anafahamu zaidi namna ya ufuatiliaji wa fedha za mashirika kuliko wafadhili wenyewe ambao ndio watoaji wa fedha hizo na wakati huo huo hana ushahidi wa kile anachokiongea. Kwa msingi huo, hata maelezo kuwa Bi. Flora Masoy anamtumia Mhasibu Regina Solomon kama sehemu ya wizi wa fedha ni maelezo ya kupotosha. Hakuna nyaraka yoyote iliyowahi kufojiwa.
Kuhusu vikao vya Bodi
Maelezo ya Inkognito kuwa Morogoro Paralegal haijawahi kufanya vikao vyake vya Bodi kwa miaka mingi si maelezo ya kweli. Ukweli ni kwamba Morogoro Paralegal imekuwa ikiendesha vikao vyake kama kawaida na imefanya kikao chake cha mwisho cha Bodi tarehe 15/03/2013. Kumbukumbu za kikao hicho na vingine zipo.
Kuhusu ofisi za kupanga
Inkognito ametoa tuhuma kwamba mpaka leo Morogoro Paralegal inafanya kazi zake katika ofisi za kupanga na kwamba kuna fedha kiasi cha milioni 11 zilitolewa kwa ajili ya kiwanja. Taarifa hiyo sio sahihi kutokana na sababu zifuatazo: (i). Hakuna mfadhili aliyetoa fedha hizo (Milioni Kumi na Moja) kwa ajili ya kiwanja na kujenga ofisi. (ii). Shirika kuendesha shughuli zake katika ofisi za kupanga ni jambo la kawaida. Katika hili nitatoa mfano wa shirika kubwa la Foundation for Civil Society ambalo limepanga katika jengo la Haidery Plaza jijini Dar es Salaam licha ya shirika hilo kuwa na fedha za kutoa kwa mashirika mengine kama Ruzuku.
Mfano mwingine ni Shirika kubwa kama ActionAid Tanzania, licha ya shirika hilo kutoa fedha za Ruzuku kwa mashirika yasiyo ya kiserikali lakini lenyewe linaendesha shughuli zake katika nyumba ya kupanga huko Mikocheni. Kwa mfano, zipo taasisi kubwa pia za fedha ikiwemo benki kama CRDB, NMB,NBC, na benki nyinginezo ambazo hutoa fedha kwa mashirika, makampuni na watu binafsi ambao wengine hutumia fedha hizo kujengea maofisi makubwa na yenye hadhi huku benki husika ikiendelea kuendesha shughuli zake katika ofisi za kupanga.
Hivyo basi, hoja ya Morogoro Paralegal kuendesha shughuli zake katika ofisi za kupanga ni hoja isiyo na maana kwakuwa ili shirika (Hasa mashirika kama Morogoro Paralegal) lijenge ofisi zake lazima yawe na fedha ya kufanya hivyo hasa ukizingatia kuwa ni wafadhili wachache sana wanaotoa ruzuku za ujenzi wa ofisi za mashirika. Kuzungumzia paralegal kupanga ni uchochezi wenye lengo la kuchafua jina la shirika na Bi. Flora Masoy
Kuhusu kujitoa Uanachama
Kwa mujibu wa katiba ya Morogoro Paralegal, mtu yoyote anayekidhi masharti na vigezo vya uanachama anaweza kuwa uanachama wa shirika. Uanachama wa Morogoro Paralegal upo wa aina tatu ambao ni wanachama waanzilishi, wanachama wa kujiunga na shirika na wanachama wa heshima (Honorary Members).
Moja ya haki za mwanachama ni kujitoa uanachama kwa hiari. Ukweli ni kwamba, Wanachama anaowazungumzia Inkognito kuwa wamejitoa kutokana na madhaifu ya Bi. Flora Masoy sio ya kweli bali walijitoa kwa hiari yao na kwa kufuata taratibu ingawa bado wanashirikina na Morogoro Paralegal mpaka sasa.
Kujitoa kwa wanachama hao hakuna uhusiano wowote na utendaji wa Bi. Flora Masoy kwa kuwa wanachama hao walieleza pia sababu za kujitoa kwao ikiwa ni pamoja na kukabiliwa na majukumu ambayo yaliwafanya kushindwa kushiriki kikamilifu shughuli za shirika. Wanachama wanaozungumzwa kujitoa ni wawili tu.
Kuhusu Sakware:
Inkognito amemtaja Sakware kuwa alikuwa Mwenyekiti wa UNGO-MORO, madai hayo si ya kweli. Sakware hakuwahi kuwa Mwenyekiti wa UNGO-MORO bali alikuwa ni katibu wa UNGO-MORO. Isitoshe, tangu alipomaliza muda wake akiwa kama Katibu wa UNGO-MORO mpaka leo hii Ndugu Sakware hana sehemu maalum ya kufanyia kazi. Naomba ieleweke kuwa katika mashirika yanayofanya kazi zake sawa sawa kama Morogoro Paralegal, hakuna suala la kutosana au kubebana kama anavyodai Inkognito kuwa Sakware ametoswa, mtu anateuliwa kusimamia au kufanya kazi fulani baada ya kukidhi vigezo mbalimbali.
Kama ilitokea ndugu Sakware akakosa ajira ndani ya shirika la Morogoro Paralegal kama alivyotegemea (kama alitegemea hivyo) basi ieleweke kuwa ni kutokana na kushindwa kwake kukidhi vigezo hivyo, na si suala la kutoswa au kubebana.
Kuhusu Regina:
Ukweli ni Kwamba Regina hajawahi kuwa na gari aina ya harrier kama anavyodai Inkognito, bali ana gari aina ya Ipsum mbayo nayo amenunuliwa na mume wake. Ni Binti mahiri katika fani yake ya uhasibu kiasi cha kuaminiwa sio tu na Morogoro Paralegal bali hata na wahasibu wenzake, wakaguzi wa fedha na wafadhili mbalimbali.
Kucheleweshwa kwa fedha za Miradi:
Ni jambo la kawaida sana kwa wafadhili, wahisani na wadau wengine wa maendeleo kuchelewesha fedha za mradi kwa Mashirika au Halmashauri mbalimbali. Morogoro Paralegal, haijawahi kucheleweshewa fedha au kunyimwa fedha kutokana na sababu ya ubadhilifu kama anavyodai Iknognito.
Kuhusu gari la Morogoro Paralegal
Gari inayotumiwa na Morogoro Paralegal kwa shughuli za ofisi ni aina ya Hiace ambayo ilinunuliwa kupitia mradi wa Mama Ardhi, mradi uliofadhiliwa na shirika la ActionAid. Wakati huo mimi ndiye niliyekuwa Afisa Mradi wa mradi huo wa Mama Ardhi. Baada ya kumalizika kwa mradi huo, gari hilo limeendelea kutumiwa na Morogoro Paralegal kwa shughuli za kituo ikiwemo kusaidia shughuli za ufuatiliajii wa miradi. Kwa kifupi Gari hilo limekuwa msaada hata kwa miradi inayofadhiliwa na wafadhili wengine.
Kwa kuwa mradi uliokuwa umefadhili ununuzi wa gari hilo umeshaisha, hakuna fedha yoyote inayotolewa na wafadhili kulihudumia gari hilo. Kimsingi, gari hilo linahitaji kulipiwa Bima, Motor Vehicle, kubadilisha vipuri, mafuta na Huduma nyingine. Morogoro Paralegal iliona ni busara gari hilo likatumiwa kutoa Huduma ya kubeba wanafunzi pale linapopata kazi za namna hiyo ili liweze kupata fedha za kujiendeshea lenyewe ili liendelee pia kuhudumia kazi za shirika.
Kuhusu Dereva "Bob"
Inkognito amemtaja dereva wa gari hilo aitwaye Bob kuwa ameajiriwa na Morogoro Paralegal. Ukweli ni kwamba, dereva huyo hakuajiriwa na Morogoro Paralegal, bali hujitolea kufanya kazi za shirika pale anapohitajika kufanya hivyo. Hana ajira na hilo Inkognito inawezekana anaujua ukweli huo ila anataka tu kuchafua jina la shirika na Bi. Flora Masoy.
Kuhusu Msumba Lisungu
Msumba Lisungu ambaye ni Askari Magereza hajawahi kuwa Afisa mradi wa mradi wowote ule unaotekelezwa na Morogoro Paralegal katika kipindi chochote kile. Kama ilivyo kawaida kwa mashirika na taasisi mbalimbali kuwa na mahusiano mema na wadau kutoka kada tofauti tofauti, halikadhalika, Morogoro Paralegal hushirikiana na watu wa kada katika utekelezaji wa majukumu yake.
Aidha, Inkognito ameishia tu kumtaja Msumba Lisungu na kumbebesha tuhuma zisizo na ukweli wowote ndani yake. Ni vema ikaeleweka kuwa, Morogoro Paralegal itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali, makundi ya kijamii na watu binafsi katika kutimiza malengo yake. Ukiacha chuki binafsi za ndugu Inkognito, hakukuwa na haja ya kumhusisha Msumba Lisungu na masuala ya Morogoro Paralegal.
Kuhusu Sylivesta Masawe
Huyu ni mmoja kati ya wanachama wa Morogoro Paralegal. Anafanya kazi zake kwa kujitolea (Halipwi Mshahara) mpaka sasa. Amekuwa msaada wa karibu kwa masuala mengi ya kituo. Kumtuhumu ndugu Sylivesta Masawe kuwa haelewi kinachoendelea ndani ya Morogoro Paralegal ni kitendo chenye lengo la kumdhalilisha kwani Binafsi namfahamu vizuri jinsi alivyo Comitted kwa kazi za shirika
Kuhusu Isabela Katungutu
Huyo ni mmoja kati ya wanachama waanzilishi wa Morogoro Paralegal tangu lilipoanzishwa Shirika mwaka 1993 chini ya Usimamizi wa kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC). Kwa muda wote huo amekuwa akifanya kazi kwa kujitolea mpaka hivi leo. Amekuwa msaidizi wa kisheria mwenye uzoefu wa muda mrefu anayekalia dawati la UNASIHI katika kituo. Wanufaika wengi wanamfahmu n kuheshimu mchango wako katika shirika na jamii kwa ujumla.
Majibu ya jumla dhidi ya tuhuma za Inkognito ·
Morogoro Paralegal Haijawahi kupiga dili wala kushirikiana na kiongozi yeyote wa serikali au mtu yoyote katika kujipatia fedha za mradi. · Hakukuwa na sababu ya kuandika namba za Bi. Flora Masoy kwenye Mtandao wa jamiiforums. Ingekuwa busara sana iwapo Inkognito angeweka namba zake yeye mwenyewe kwenye mtandao huo ili wanaohitaji kupata ukweli kutoka kwake watumie fursa hiyo kumuuliza yeye ambaye anadai ana ushahidi wa kile anachokisema.
Aidha, Jamiiforums si chombo cha kuwajibisha kisheria (It is Not a Lawful entity) kama ilivyo kwa jeshi la polisi, mahakama au Takukuru), ingekuwa busara iwapo Iknognito angetoa namba za hao aliowataja kuwa wanaweza kutoa ushahidi wa kile anacho kituhumu. ·
Kitendo alichokifanya Inkognito ni kutaka kumletea Bi. Flora Masoy Usumbufu usio wa lazima kwa kuwa, ni jambo la kushangaza kugawa namba ya mharifu/mtuhumiwa kwenye mtandao ili aulizwe na kujibu kama ni kweli ametenda kosa analotuhumiwa kulitenda au la. ·
Morogoro Paralegal inaendeshwa kwa kufuata taratibu za usajili wa NGO. Mara ya mwisho, Morogoro Paralegal imelipa ada yake ya mwaka kwa Msajili wa NGO tarehe 25.4.2013 kupitia Risiti Namba. 37486110. · Morogoro Paralegal haina utaratibu wa kuingilia maisha binafsi ya wafanyakazi wake. Suala la mfanyakazi au mtu anayejitolea kuishi nyumba ya kupanga, au ya udongo au ya ghorofa ni suala lililo nje ya malengo ya Morogoro Paralegal.
Nimelazimika kusema haya kwakuwa, Inkognito alitoa maelezo kuwa mmoja kati ya waanzilishi wa Morogoro Paralegal anaishi nyumba ya Udongo ni udhalilishaji, Inkognito alipaswa kueleza ni kwa chanzo gani cha fedha kingetumika kujenga nyumba za wanaojitolea. ·
Kama kuna hoja yoyote inayohitaji majibu mahususi, ni vema wahusika wakafika kwenye ofisi za Morogoro Paralegal ili wapatiwe majibu yaliyo sahihi badala ya kuegemea kwenye uzushi na upotoshwaji uliofanywa na Inkognito. · Kwa watakaohitaji mawasiliano na Mimi, ni vema wakawasiliana nami kupitia namba zangu ambazo ni 0714-559910 au 0787-070707 Asanteni Nawasilisha