Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,286
Moyo wangu ewe moyo, naomba sikiza sana,
Moyo ulinde unyayo, na njia zenye laana,
Moyo na uwe na mbuyo, bahari ni chafu sana,
Moyo sifanye uchoyo, mtoaji ni Rabana,
Moyo ninasema nawe, njano sifanye machungu.
Moyo sifanye machungu, yao yasikuumize
Moyo tegemea Mungu, maneno siendekeze,
Moyo nawapige gungu, tulia siwakataze,
Moyo sivunje mkungu, ngoma yao usicheze.

Moyo usipige fundo, waja ukawachukia,
Moyo sibadili mwendo, usije kuwashukia,
Moyo jiweke kando, na fujo nakuusia,
Moyo sifanye kondo, usije ukaumia,

Moyo sifanye papara, ulo nayo ukasema,
Moyo sifanye harara, ukaikosa hekima,
Moyo usije kuchura, nataka omba salama,
Moyo sipoteze dira, na njia ya waja wema,

Moyo japo wachunika, kishike ulicho nacho,
Moyo kama watishika, Allah ni lako ficho
Moyo usije kuchoka, wala usione kicho,
Moyo naomba futika, Mola wako ana macho,

Moyo usione joto, sijibu wenye kuzoza,
Moyo sione fukuto, ingawa wakuchokoza,
Moyo sifanye utoto, ujinga hauna jaza,
Moyo dunia mapito, upite bila kucheza,
Moyo ninasema nawe, moyo sifanye machungu.
Moyo usiwe mkali, wajinga hupenda shari,
Moyo bora stahamili, subira huvuta heri,
Moyo sijione dhuli, nguzo yako ni Jabari,
Moyo usifike mbali, shetwani asikughuri,

Moyo sigeuke chui, ingawa dhiki waona,
Moyo hayakuchefui, waendelee tukana,
Moyo jifanye hujui, usipende kushindana,
Moyo upunguze tui, walaji wasije nuna,

Moyo sigeuke simba, swala waka kukimbia,
Moyo usije wakumba, ingawa wakuchukia,
Moyo kwa furaha imba, yano kusibu fukia,
Moyo wangu kuwa mwamba, ishinde hino dunia,

Moyo sigeuke ndege, kila mti ukatua,
Moyo wacha wakutege, midhali umetambua,
Moyo hata wakupige, mdomo sije inua,
Moyo sicheke matege, Mola ndiye muumbua

Moyo bora uwe zuzu, mengi yapate kupita,
Moyo na uwe kauzu, wallahi hutaudhika,
Moyo usome ufuzu, elimu ya kufutika,
Moyo si mlambizu, sipae unavyotaka,

Moyo jifunze sikia, yale usio yapenda,
Moyo ewe angalia, viumbe wanayotenda,
Moyo kesho subiria, leo usiwe na inda,
Moyo hutaangamia, japo mbio wanaenda,

Moyo kama wanipenda, nilinde na mitihani,
Moyo nisije kukonda, vya wenzangu kutamani,
Moyo heri ya shinda, iliyo mwangu chumbani,
Moyo ridhika na kunda, aliye mwangu bandani,

Moyo kuwa Sultani, cha mtu usitamani,
Moyo usiwe Shetwani, ukaiba majumbani,
Moyo usiwe jununi, ukaivunja amani,
Moyo usiwe fatani, usalata wafaani?

Moyo siogope jasho, pato haliwi ngekewa,
Moyo sifanye mshusho, subiri kufanikiwa,
Moyo na ufanye mbisho, upate kufunguliwa,
Moyo nimefika mwisho, nadhani umeelewa,

Njano5
0784845394.