SoC04 Mpango wa kupunguza ukosefu wa ajira na kujenga nguvu ya kiuchumi kwa vijana wanaohitimu chuo

SoC04 Mpango wa kupunguza ukosefu wa ajira na kujenga nguvu ya kiuchumi kwa vijana wanaohitimu chuo

Tanzania Tuitakayo competition threads

black abdu

Senior Member
Joined
Dec 2, 2022
Posts
156
Reaction score
212
Tunaposhuhudia ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu na serekali kuongeza wigo wa wanafunzi kupata mikopo, tunakumbana na changamoto ya ongezeko la vijana wanaohitimu elimu ya chuo lakini wanakosa ajira kutokana na uhaba wa nafasi za ajira.

Suala hili nalichukulia kwa uzito, kwa sababu vijana kama mustakabali wa Taifa hapana budi kujenga juu yao mustakabali wa weledi na maarifa utakaotegemewa kuzalisha wataalamu wa baadae. Wataalamu ambao watalitoa Taifa kutoka kutegemea wataalamu kutoka nje wanaoletwa kufanya kazi kwa gharama kubwa. Natamani kuiona Tanzania inayotegemea zaidi wataalmu wa ndani kukuza uchumi na kulinda rasilimali. Wakati tunapofungua milango kukaribisha wawekezaji zaidi nchini ni vema wawekezaji hawa wakakuta vijana wetu wana uwezo wa kusimamia miradi inayoanzishwa ili kulinda maslahi ya nchi kwa upana zadi.

Kiuhalisia, Taifa linapoteza mtaalamu mzawa kwa kila kijana anayekosa ajira ya fani aliyosomea. Mfano mtu amesoma usimamizi wa masoko lakini analazimika kwenda kufungua biashara ya maziwa kwa mtaji mdogo. Kwa namna moja ni vizuri kuwa kijana huyu atakuwa amejinasua kutoka kadhia ya utegemezi lakini amekosa nafasi ya kuwa mshauri mkubwa wa mambo ya masoko kwa hapo baadae.

Nini serekali inaweza kufanya?

Kwa mpango wa muda mfupi, serekali ianzishe program za mafunzo kazini (internship) kwa wanafunzi wote wanaomaliza masomo ya chuo kama ilivyo kwa wanafunzi wa fani ya afya wanaopangiwa kufanya kwenye hospitali mbalimbali. Programu hii husaidia sana wanafunzi wa afya kufanyia mazoezi walichojifunza darasani na kuwapa uzoefu wa kutenda kazi. Fursa kama hiyo inakosekana kwa wanafunzi wa fani zingine ambao wengi wao wanakumbana na ugumu wa kupata ajira kwa kukosa uzoefu.

Serekali isimamie hili kupitia wizara ya kazi na vijana kwa kuweka kipengele cha kutaka kila kampuni iliyosajiliwa na kufanya kazi nchini kutenga nafasi ya mafunzo kazini kwa ajili ya wahitimu kutoka vyuoni sawa na ile internship program kwa wanafunzii wa fani ya afya na makampuni haya yatajumuisha taarifa za utekelezaji wa hili kwenye taarifa zao za mwaka.

Licha ya kuwa mpango huu utawawezesha vijana kujifunza zaidi kwa vitendo wanakuwa na uwezekano wa kupata ajira zinazoweza kujitokeza wanapokuwa kwenye kipindi hiki cha mafunzo. Kuna uwezekano pia wasimamizi wa kampuni hayo kuamua kuwabakisha vijana hao wanapomaliza muda wao wa kujifunza, kutokana na uwezo wa utendaji watakauonesha.

Sanjari na hilo serekali ianzishe jalada la kutunza taarifa za kitakwimu za vijana wanaomaliza mafunzo ya kifani pamoja na taarifa zao za hali ya ajira na muendelezo wa kitaaluma kwa fani zao ili kuwapatia msaada wanapohitaji.

Kwa upande mwingine serekali itengeneze mpango wa kuongeza ufadhili wa masomo ya juu zaidi ya kifani kwa kushirikiana na wahisani kutoka nchi rafiki zenye uwezo mkubwa wa fani husika, ambapo vijana kutoka nchini wataenda kujifunza kwenye nchi hizo ili watakaporudi wapige hatua zaidi katika utaalamu wa fani zao. Hii itasaidia vijana wasikae kwenye nafasi moja ya ajira kwa muda mrefu sana, na badala yake watoe nafasi kwa wengine wanaowafatia.

Ama kwa mpango wa muda mrefu, serekali ianzishe utaratibu wa kuwapima vijana wanaomaliza programu za mafunzo kazini na wenye uwezo wa kujiajri ili kuwadhamini kupata mitaji ya kuanzisha makampuni yao wenyewe. Mpango huu unaweza kufanyika kwa ushirikiano na taasisi za fedha hasa mabenki ambayo yatatoa mitaji kwa vijana hawa na serekali itasimama kama mdhamini kuhakikisha makampuni yanayoanzishwa na vijana kwenye mpango huu yanastawi na kuwa na uwezo wa kuajiri vijana wengine.

Kituo cha uwekezaji nchini (TIC) kinaweza kusaidia kuunganisha vijana walionzisha makapuni yao na wawekezaji kutoka nje wanaokuja kuwekeza nchini. Wawekezaji hawa wanaweza kununua hisa kwenye makampuni yanayomilikiwa na vijana wazawa na kuyaongezea nguvu badala ya kuja kuanzisha kampuni yao kutoka hatua za awali. Hii itavutia wawekezaji kuwa wataokoa muda kwa kuepuka mchakato wa awali ambao huwa na usumbufu na gharama.

Muhimu ni vijana wetu wanaoanzisha makampuni yao kuwa na taarifa zilizofanyiwa tafiti na kutoa majibu ya maswali ya wawekezaji wataoonesha nia ya ushirikiano. Serekali inaweza kuweka makampuni haya kwenye tovuti zinazotoa taarifa za kuwavutia wawekezaji ili iwe rahisi kuunganishwa nao.

Serekali inaweza kupanua wigo wa manufaa kwa vijana hawa kwa kuwajumuisha kwenye orodha ya wajumbe wanaoongozana na raisi na viongozi wengine kwenye ziara za kiserekali kwa nchi za nje, zinazokusudiwa kuvutia wawekezaji. Itapendeza endapo vijana hawa watapata wasaa wa kuwasilisha taarifa za makampuni yao huko nje ili kuwa rahisi kukutana na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini.

Faida ya mpango huu katika kuwavutia wawekezaji pia ni kuwapa uhakika wa nia ya serekali ya kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji nchini na kupata uhakika wa thamaniwa uwekezaji wao na matokeo yake kuiweka Tanzania kwenye orodha ya nchi zinazopendekezwa kwa uwekezaji. Wakati huo huo soko la ajira kwa vijana wazawa litaongezeka kwa kiasi kikubwa na kuwapa nafasi ya kuona matunda ya muda walioutumia masomoni.

Mpango huu si tu kuwa utapunguza tatizo la ajira kwa vijana wetu bali pia utawapa nguvu ya kufanya maongezi (bargaining power) na wawekezaji kwa kusimamia maslahi yao badala ya kuwa wapokeaji wa mapendekezo ya wawekezaji zaidi. Tutajenga kizazi cha baadae chenye nguvu ya kufanya maamuzi ya kiuchumi na kushirki kikamilifu katika kujenga dira ya uchumi wa Taifa.
 
Upvote 4
Back
Top Bottom