Wakuu hiiimekaaje? ni upi uhalisia wa hili kwamba Mbowe ana mpango wa kuwadhuru viongozi wa CCM ifikapo februari 2025?
- Tunachokijua
- Freeman Mbowe ni Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA akianza kuitumikia nafasi hiyo mwaka 2004 ambapo ameendelea kuishikilia mpaka sasa 2024, (rejea ukurasa wa 18). Watu wengi wamekuwa na shauku ya kushuhudia uchaguzi ujao wa viongozi ndani ya Chama hicho ngazi ya taifa, jicho kubwa likiwa katika nafasi ya Mwenyekiti, nafasi ambayo imeshikiliwa kwa zaidi ya miaka 20 na Mbowe. Itakumbukwa pia Mbowe alikuwa ni moja kati ya waasisi wa chama hicho mwaka 1992.
Uongozi wa Mbowe ndani ya CHADEMA kwa miaka 20 umekuwa na mchango mkubwa katika kujijenga kwa chama hicho kisiasa. Mara kadhaa kumekuwa na upotoshaji ambao umekuwa ukimlenga kiongozi huyo, njia ambayo imekuwa ikitumiwa na wapotoshaji kusambaza taarifa zisizo za kweli na zenye nia isiyokuwa njema dhidi ya kiongozi huyo na chama chake. Rejea hapa, hapa, hapa, na hapa.
Hivi karibuni kumekuwapo na Chapisho linalodaiwa kutolewa na The Chanzo likisema mpango wa Mbowe waumbuka, ni kutaka kuwadhuru baadhi ya viongozi wa CCM na serikali ifikapo februari 2025.
Je ni upi uhalisia wa Chapisho hilo?
Chapisho hilo linaonesha lilitolewa mnamo Disemba 06, 2024, aidha ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck ulibaini chapisho hilo halikuchapishwa kabisa katika kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya The Chanzo huku siku ya tarehe hiyo ikiwa haina hata taarifa inayofanana na hiyo katika kurasa hizo.
Hata hivyo JamiiCheck imebaini mapungufu kadhaa katika chapisho hilo yanayobainisha utofauti wake dhidi ya machapisho rasmi ambayo hutolewa na The Chanzo. Sehemu ya mapungufu hayo ni pamoja na matumizi ya mwandiko (fonts) katika kichwa cha habari ambao haufanani na ule unaotumiwa na The Chanzo, matumizi ya rangi tofauti kwenye uandishi wa tarehe, kutokuwepo kwa sehemu ya mstari mweupe wa pili unaotenganisha kati ya kichwa cha habari na picha.
Mapungufu hayo yanadhihirisha kuwa chapisho hilo lilitengenezwa na wapotoshaji wakitumia alama na nembo za The Chanzo ili kusambaza taarifa zisizo za kweli halijatolewa na The Chanzo.
Kabla ya kuamini taarifa ni vema kukagua alama za utambulisho wa chombo kinachodaiwa kutoa taarifa husika ili kubaini kama zinawiana hatimaye kupata uhalisia. Pia wapotoshaji wamekuwa wakitumia mara kadhaa alama na utambulisho wa The Chanzo kutengeneza na kusambaza taarifa zisizo za kweli. Rejea hapa, hapa na hapa.