3rd August 10
Mpendazoe aibukia ubunge Kinondoni
Mwandishi Wetu
Baada ya kuangushwa kwenye kura za maoni za kuwania ubunge jimbo la Segerea jijini Dar es Salaam kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyekuwa Mbunge wa Kishapu (CCM), Fred Mpendazoe, ameombwa na chama hicho kuwania ubunge wa jimbo la Kinondoni .
Ni baada ya Mpendazoe kuangushwa kwenye kura za maoni wa jimbo la Segerea hivi karibuni na Rachel Mashishanga katika uchaguzi ndani ya chama hicho uliofanyika hivi karibuni.
Katika uchaguzi huo, Rachel alipata kura 41 na kumbwaga Mpendazoe aliyeambulia kura 28.
Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema, Wilaya ya Kinondoni, Fred Kimath, sekretarieti ya chama hicho jimbo na Wilaya ya Kinondoni ilikaa jana na kutoa uamuzi wa kumshauri Mpendazoea kuwania ubunge katika jimbo hilo.
" Kwa kutambua umuhimu wa kuwa na watu mashuhuri kama Mpendazoe na Mashishanga, sekretarieti ilituma ujumbe kumwomba agombee jimbo la Kinondoni na amekubali kufanya hivyo, alisema Kimath.
Alisema ujumbe ulioonana na Mpendazoe ni pamoja na Mwenyekiti wa jimbo hilo, Michael Sebugabo, Katibu Fred Kimath, Mweka Hazina, Edgar Njwaba, Katibu Mwenezi Moses Raymond, Katibu wa Mkoa wa Kinondoni, Henry Kilewo.
Kimath, alisema sekretarieti imeitisha kikao cha kamati ya utendaji kwa ajili ya kuwasilisha mapendekezo yake kabla ya mkutano wa kura za maoni na uteuzi kwa kuzingatia Katiba na kanuni za chama.
Sekretarieti inamshukuru Mpendazoe kwa kukubali wito huu wa kuwatumikia Watanzania ikiamini Mpendazoe ni Mbunge wa Taifa ambaye m chango wake unahitajika kuingoa CCM, alisema Kimath.
Mpendazoe alikihama Chama cha Mapinduzi CCM mapema mwaka huu, akidai kuwa kimepoteza mwelekeo na kuhamia Chama cha Jamii (CCJ).
Baada ya chama hicho kukosa usajili wa kudumu hivyo kukosa sifa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Mpendazoe aliamua kuhamia Chadema.
NIPASHE
Mpendazoe aibukia ubunge Kinondoni