Msaada wa Ushauri

ALF

JF-Expert Member
Joined
Apr 17, 2011
Posts
207
Reaction score
137
Habari zenu ndugu, nimekuwa nikivutiwa sana na ushauri mnaotoa juu ya mambo mbalimbali. Ushauri unaotolewa huwa unanipa moyo sana.

Mimi ni muajiliwa kwa miaka 13 sasa katika sekta binasfi nimebahatika kununua shamba lenye heka 12 maeneo ya kijiji cha mlanzi wilaya ya rufiji, mwaka jana nilibahatika kuchimba kisima, nimefunga pump na baada ya kujidunduliza nimeweza kupata Generator Used ambalo nategemea kuanza kupandisha maji kwajiri ya umwagiliaji tatizo linalonikabili mpaka sasa ni madeni niliopata baada ya kuanza project hii, naomba ushauri wako je ni mazao gani naweza kulima ambayo yatanisaidia kupata pesa nyingi ili niweze kulipa madeni hayo na kuingia moja kwa moja kwenye ujasiliamali na kuachana na utumwa wa kuajiliwa?.

Changamoto kubwa ya huko ni nguruwe wa porini, pia naomba ushauri namna ya kuwazibiti.
Naomba kuwasilisha.
 
Eka moja Lima nyanya nyingine passion na ya tatu midizi .

Njia bora ya kudhibiti nguruwe pori kama wewe si muisilamu ni kuwatafuna .
Kama utaamua kuwatafuna uwe mwangalifu jamaa wa huko wasije wakakutafuna wewe.
 
Nashukuru kwa ushauri wako ndugu yangu.
 

PART ONE

Mkuu ALF nimeamua nikujibu hapa jukwaani baada ya kuona hii thread yako ambayo umeulizia kitu kile kile ulichoniulizia kwenye PM. Nimeona nitakuwa nimetumia vizuri muda na nguvu ya kuandaa jibu lako iwapo litawafikia na wengine wenye mazingira yanayofanana na wewe.

Kwanza ninaomba nikupe angalizo mapema kuwa kwa eneo lako kubwa hilo unaweza kujikuta umeshawishika kuzalisha utitiri wa aina nyingi ya mazao na mifugo ukiwamo ufugaji wa samaki. Jitahidi ujikite kwenye mazao machache na mifugo michache ili uweze kuhudumia kwa umakini na ufanisi. Kwa ufafanuzi zaidi rejea nyuma usome thread ya mdau Bwegebwege: Naomba ushauri wa mawazo kwenye Kilimo na ufugaji

Ufugaji wa samaki kwenye eneo lako unaweza kutumia maji mengi, inapaswa uwe una uhakika juu ya akiba ya maji yaliyopo kwenye eneo lako! Kumbuka ufugaji wa samaki unaweza kuleta ushindani wa matumizi ya maji na mazao mengine! Nina wasiwasi ufugaji wa samaki unaweza kukausha haraka maji kwenye kisima chako labda tu kama una uhakika na kiasi cha akiba ya maji iliyoko ardhini.

Kwa kuwa unandoto za kuachana na ajira, ni vema ukaingia kwanza kwenye kipindi cha mpito kujiandaa tayari kuingia kwenye ile tunaita “you eat only what you kill”! Kipindi hiki cha mpito kama utakuwa uko kazini ni vigumu kusimamia vizuri baadhi ya mazao au mifugo huko shambani! Sina uhakika unaishi karibu na shamba lako au la. Ukiwa bado kazini huwezi kulima kwa ufanisi mazao kama ya bustani ambayo ndiyo yana kipato kikubwa sana na ndiyo yanayoweza kukulinda kukupatia kipato cha mara kwa mara kwa mwaka mzima na kukusaidia kulipa deni. Lakini si rahisi iwapo unaishi mbali na shamba lako!

Kwa kipindi cha mpito kama uko mbali na shamba jizatiti zaidi kupanua kilimo chako cha mihongo na mananasi! Utaendelea kupanua zaidi moja ya mazao haya kutegemea na hali itakavyokuvutia ukizingatia mazingira na soko lilivyo. Huenda unaweza gundua kuwa moja ya mazao hayo halishambuliwi sana na nguruwe au linakulinda sana kwa kipato chake. Hilo ndiyo utalipanua zaidi! INAENDELEA………
 
PART 2

Mkuu ALF, baada ya kipindi cha mpito ukishajiridhisha kuwa sasa shamba lako linajiendesha lenyewe hapo itabidi ufuate mwongozo ufuatao:
Shambani uwe na mazao kwa makundi aina tatu, mazao ya muda mfupi, mazao ya muda wa mrefu na mazao ya kudumu.

Mazao ya muda mfupi

Haya mazao yatakusaidia kukuingizia pesa kidogo kidogo kuweza kukufanya uweze kupata mahitaji yako ya kila siku na lakini pia yanaweza hata kumudu kulipa madeni yako. Haya ni mazao ya bustani. Kwa vile tayari unayo pampu na kisima cha uhakika, mazao haya ya bustani yanaweza hata yakawa ndiyo moyo wa shamba lako kulingana na mipango yako na utashi wako. Inawezekana eka zako zote 12 zikawa ni mazao tupu ya bustani kulingana na soko na juhudi yako. Mazao ambayo nashauri kwa eneo lako huko Rufiji ni Hoho, nyanya chungu na pili pili mbuzi! Haya ni mazao rafiki kwa anaenza shughuri hizi kwa mara ya kwanza. Unaweza kwa kuanzia ukalima nusu au ekari moja kwa kila zao kisha ukaendelea kujipanua kadri unavyoendelea kumudu changamoto zake. Kadri utakavyokuja kuwa na nguvu zaidi ya kipesa unaweza kwenda hatua nyingine zaidi ya kulima mazao yenye kulipa zaidi kama nyanya maji, matikiti na vitunguu! Maana haya mazao (nyanya maji, matikiti maji na vitunguu) ukiyaendea kichwa kichwa utatupwa chali asubuhi tu, yana faida kubwa sana na mieleka yake ni spectacular!!.


Pia usiache kulima mboga za majani japo nusu eka au ekari moja kwa ajili ya kupata pesa za kujikimu, soma thread ya mdau Kig :”Naombeni ushauri kuhusu biashara na kilimo cha bustani ya mboga mboga”. Itafute hii thread huko nyuma na uisome ushauri aliopewa huyu mdau.


Mazao ya muda mrefu

Haya mazao tayari unayo. Hivi sasa una ekari 1 ya mihongo na ekari 3 za mananasi ni hatua kubwa hii, bahati nzuri mazao yote haya hayana mahitaji makubwa ya umwagiliaji. Ninashauri upanue zaidi kilimo cha mihogo na mananasi ili haya mazao ya muda mrefu yachukue eneo kubwa zaidi kipindi ambacho hujajipanua sana kwenye mazao mengine!


Uzingatie kuwa hutahitaji kununua mbegu za mihogo na mananasi tena kitu ambacho ni hazina kubwa ambayo tayari unayo! Haya mazao yatakuwa yakikupa pesa za msimu za mkupuo. Pesa nyingi za mkupuo ndiyo zinaweza kukufanya ukafanya uwekezaji mwingine zaidi kadri ya unavyotaka kutimiza ndoto zako.
 
PART 3

Mkuu ALF

Mazao ya kudumu.

Kabla hujaamua kupanda mazao ya kudumu angalia mbali! Huenda kuna wakati unaweza kuwa na nguvu ya kulima shamba lote vitunguu au mboga mboga au Mananasi! Maana tatizo ukipanda zao la kudumu huwa si rahisi kuchukua uamuzi wa kuling'oa. Inahitaji maamuzi magumu kung'oa mazao ya kudumu. Kwa kuwa ni muhimu kuwa na zao la kudumu tenga ekari 3 hadi 5 kwa ajili ya zao la miembe! Hii ndiyo itakuwa BIMA na pensheni yako ya uzeeni kipindi nguvu zimekuishia. Kuna thread za zao la embe humu ukipendezwa zitafute uzisome.


Mwisho, wakati ukiendelea na uzalishaji ujiandae kifikra na kimikakati kujenga Green House siku za mbeleni. Huenda usipate fursa ya kununua shamba linguine tena. Ukiwa na mawazo ya kuwa na green house mbeleni huwezi kulazimika kupanua shamba lako kwa kununua ardhi nyingine, bali ni kuwekeza zaidi kwenye hii technolojia ambako ndiyo huko ambako zama hizi za DIGITALI tunakopaswa kujielekeza. Unakuwa na eneo dogo, nguvu kidogo, mazao kibao na kwa uhakika zaidi. Kuna green house za bei nafuu kwa kutumia mbao. Green house za Balton zinahitaji mtaji mkubwa, unaweza kujenga green house kwa nusu ya gharama ya green house za Balton kwa kutumia mbao na miti badala ya vyuma na mabomba ya chuma.


Kwa hiyo ni budi ukawa na malengo ya muda mfupi (Mazao ya muda mfupi), malengo ya muda wa kati (Mazao ya muda mrefu, mihogo na mananasi) na malengo ya muda mrefu (Mazao ya kudumu kama miembe na ujenzi wa Green house).


Kuhusu kuwa na mifugo muhimu kuwa makini sana kwenye kuamua wingi wa mifugo hii kwani tahadhari yangu inarudi pale pale kwamba jihadhari usiwe na vitengo vingi sana vya uzalishaji kwani ufanisi unaweza kushuka na kushindwa kumudu kuliendesha shamba kwa faida.


Kudhibiti nguruwe pori unaweza kuzungushia shamba kwa kupanda wigo wa mikonge mistari miwili (double rows), pia tumia utaalamu asilia wa wakazi wa eneo husika lazima watakuwa wanajua jinsi ya kukabiliana na nguruwe!


Ninaimaini kwa ushauri huu utapata angalau pa kuanzia!
THE END !!
 
Mkuu ALF, pamoja na majibu mazuri ya Mkuu Kubota, nami napenda kukupa ushauri ufuatao: Tafuta vitabu hivi na kuvisoma kwa kuanzia, mapema iwezekanavyo THE CASHFLOW QUADRANT, THE BUSINESS SCHOOL & THE BUSINESS OF THE 21ST CENTURY vyote vikiwa vimeandikwa na Robert T. Kiyosaki. Vinapatikana kwenye maduka yafuatayo: Scholastic Bookshop (Mlimani City & Posta), Dar es Salaam Printers, Saramanda, n.k. Pia, kwa wauza vitabu stand ya mabasi ubungo vinapatikana.
Vitabu hivi vitakusaidia kukupa mwanga zaidi juu ya biashara na ujasiriamali katika karne hii ya 21, hasa kwa watu ambao tunakumbwa na changamoto za Usimamizi, Mitaji, na Ofisi/Eneo (premisis) la kufanyia biashara. Zaidi, vitakupa muongozo mzuri namna unavyoweza kuutumia muda wako wa ziada (part time) kujenga TIMU ya watu watakaokuwa wanakufanyia kazi (SYSTEM/ NETWORK) kama ambavyo Bakheresa, Mengi, n.k walivyo na wanavyoendelea kufanya.

Kwa mawasiliano zaidi, piga 0713 366 473 au 0767 277 223.

KILA LA KHERI MKUU.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…