GREATTHINKERDAIMA
JF-Expert Member
- Feb 26, 2014
- 232
- 46
UJENZI WA MAABARA SHULE ZA SEKONDARI NA KUKATWA MSHAHARA WA MWALIMU VINAHUSIANA VIPI?
Mwalimu nje ya shule ni mwananchi wa kawaida na anawajibika katika mambo yote ya kijamii kama wengine wanavyo wajibika. Hivyo kukata mshahara wa mwalimu kuchangia maabara ni kumbebesha mzigo usiokuwa wake na ni kinyume cha haki ya za binadamu na kosa kwa mujibu wa sheria ya kazi na mahusiano kazini.
Mchokozeni mwalimu kwa namna tofauti lakini sio kwenye mshahara wake. Kama kuna maslahi ya kisiasa nadhani aliyetoa wazo/kauli ni sawa na mkubwa aliyeachia ushuzi kisha wakasema amepumua badala ya kusema amejamba na huku wakiwa wameziba pua zao. Mimi nasema kauli hii inathibitisha kuwa ni mjambo wa hatari.
Wakurugenzi katika halmashauri mbali mbali wamekuwa wanafanya mambo nje ya utaratibu wa mamlaka yao; hii ni dalili ya kulewa madaraka au matumizi mabaya ya madaraka. Mbaya zaidi hata wanapoonekana wamepanga kutekeleza mipango yao isiyoshabihiana na kanuni ama taratibu zinazongoza utumishi wa UMMA; wamekuwa wakilindwa na mamlaka zilizowaweka na hiyo kutengeneza sumu kali kwa watumishi walio katika nafasi za chini, na hapa nazungumzia Walimu. Uanzishwaji wa kodi mpya ya maabara utawafanya walimu washughulike kutafuta namna ya kurudisha kile kilichokatwa na mwajiri kwa kutoroka kazini ana kutumia muda wa mwajiri kujipatia kipato na hivyo ufanisi wa kazi kutoweka.
Walimu daima hutumia hekima kufanya maamuzi yao katika masuala mengi ila katika hili moto wake mtauona ukilipuka. Walimu sio wanasiasa, walimu ni wanataaluma na hivyo wasiathiriwe na matamko yenye maslahi ya kisiasa. Hela ya kujenga maabara ingetosha sana kupunguza posho za wajumbe wa bunge la katiba pamoja na kupunguza matumizi ambayo si ya lazima kama michezo ya shimiwi n.k.
Waziri anayehusika, pia ikulu wamekana kuagiza hili kutekelezwa, basi ni vyema wachukue hatua kulifanyia kazi ili kurudisha imani kwa jamii ya walimu kuwa yaliyopangwa kutekelezwa na baadhi ya wakurugenzi katika halmashauri nchini si maagizo ya serikali au wizara husika bali ni maamuzi ya wakurugenzi katika halmashauri zao. Lakini kama wataishia kujibu kwenye vyombo vya habari bila kuwawajibisha hao wakoloni weusi basi jamii itaamini kuwa hayo yalikuwa maagizo toka juu.
Mwisho wa yote tujitoleeni kuleta maendeleo kwenye jamii zetu, lakini wanasiasa na watendaji kuweni makini wananchi wa sasa si wa kipindi kilichopita, wanajua kuhoji na kuchanganua mambo na umakini unapaswa kuwa kipaumbele. Tunapowaweka katika hali ya mashaka tunawarudisha nyuma kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
Mungu ibariki nchi yangu, Mungu ibariki Afrika