GeoMex
JF-Expert Member
- Jan 10, 2014
- 5,431
- 19,913
Dar Es Salaam. Mshatakiwa wa kwanza katika kesi ya kufanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu, kukwepa kodi na kuisababishia hasara ya Sh31milioni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Sadikiely Meta(71) amefariki dunia katika Hospitali ya Temeke alikokuwa akipatiwa matibabu.
Meta na wenzake 14 wanakabiliwa na kesi uhujumu uchumi namba 2/2021 yenye mashtaka 41 yakiwemo ya kusafirisha na kutumikisha walemavu katika biashara ya kuomba barabarani inayosikilizwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu.
Robert Langeni ambaye ni wakili wa Meta ameeleza hayo mahakamani leo Jumanne Februari 9, 2020 mbele ya hakimu mkazi mkuu, Kassian Matembele wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Langeni amesema Meta aliugua akiwa gerezani na kupelekwa katika hospitali ya Temeke kwa matibabu lakini Januari 28, 2021 alifariki dunia.
"Meta alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na tayari mazishi yamefanyika wiki iliyopita huko Moshi mkoani Kilimanjaro," amesema Langeni.
Awali, wakili wa Serikali, Kija Luzungana ameieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Matembele baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 23, 2020 itakapo tajwa.
Kesi hiyo imeendeshwa kwa njia ya video, huku washtakiwa14, wakiwa gerezani kutokana na mashtaka yanayowakabili likiwemo la kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Mbali na Meta washtakiwa wengine ni Yusuph Mbuani (35), Joseph Magafu (20), Emmanuel Salu, Gogad Mayenga(18), Samson Akunahai (26), Husein John(18).
Wengine ni Zacharias Paul( 18) Dotto Shigula(19), Petro Simon(21), Emmanuel Sahani(38), Joseph Mathias (20), Massanja Paul (21), Aminiel Sangu (21) na Emmanuel Lusinge(25) maarufu Salimu.
Chanzo: Mwananchi