SoC01 Msibani mavazi ya heshima Kanisani ovyo

SoC01 Msibani mavazi ya heshima Kanisani ovyo

Stories of Change - 2021 Competition

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Joined
Sep 20, 2021
Posts
3,211
Reaction score
3,611
Nyanja: Maendeleo ya Jamii
OIP.O-7ntes5CUOQPSx6NPRakQHaEI

Suala la nidhamu ya mavazi katika ibada takatifu ya Mungu limekuwa sugu na kujipatia uhalali ambao haupo hata kwenye taratibu za mifumo halali ya ibada duniani. Suala hili limeleta mpasuko kufuatia mitizamo na mikondo ya uelewa wa jambo hili na Kanisa la leo (siyo lile Yesu alilowakabidhi wanafunzi wake) limebaki bila majibu/msimamo maridhawa kuhusu nidhamu ya ibada zaidi tu ya kusoma kwenye vyombo vya habari kuwa Kanisa fulani limetenga baadhi ya waumini wake, Kanisa fulani limezuia baadhi ya waumini wake kuingia ibadani kwa utovu wa mavazi au hata Kanisa fulani limevunja kwaya kwa kupotoka kimaadili ya mavazi au Kanisa fulani limewavisha khanga waumini wake walioingia ibadani wakiwa nusu utupu. Nachelea kuamini kuwa hata baada ya Yesu Kristo kumaliza kazi duniani zaidi ya miaka 2000 iliyopita na baada ya Injili ya gharama kubwa za jasho, damu na roho iliyohubiriwa na wanafunzi wa Yesu bado makanisa ya Efeso, Korintho, Galatia, Kolosai yangalipo nasi hata leo?! Inashangaza na kusikitisha sana.

Katika ibada ya Kiislamu nidhamu ya mavazi imebaki kuwa moja ya nguzo kuu za imani hiyo huku hali ikiwa tofauti kabisa na ya kukatisha tamaa kabisa kwa ibada ile ya Kikristo. Ukristo ambao uliingia Afrika kutokea Mashariki ya Kati ambako huko umeendelea kuenzi desturi na itifaki ya mavazi na hasa ibadani. Israel ambako ndiko Ukristo ulishukia kutokea Mbinguni (asili ya Ukristo siyo duniani bali Mbinguni kwa sababu Ukristo siyo dini bali imani na imani asili yake ni Mbinguni na dini asili yake ni duniani) kuna dini kuu ya taifa ya Judaism, dini zingine ni Jewish, Ukristo (hii ni imani siyo dini), Uislamu, Druze, Kurd, Armenia, Aramean na Bahai huku Palestina kukiwa na Uislamu, Ukristo na Druze, wafuasi wote wa dini hizi huvalia mavazi maalum ya ibada, sasa kama sisi tumefuata dini/imani zao iweje tukengeuke na kuhalalisha mavazi yasiyo ya staha ibadani? Tunasimamia maandiko yapi yanayohalalisha kila mtu kuvaa anavyotaka na kukosekana viwango/standards za uvaaji? Hata Wapakwa mafuta wetu wameendelea kuenzi nidhamu na staili ya mavazi ya ibada toka Mashariki ya Kati ambako ndiko imani/dini zilitokea kuja Afrika kupitia Ulaya.

Nini maana ya vazi kibiblia. Kibiblia na hata kimila na desturi za makabila ya wanadamu, vazi maana yake ni mamlaka, ndiyo maana watu wa nyakati za Biblia waligombea vazi la Yesu, wengine walishika pindo lake na wakapokea miujiza yao waliyoitamani kwa muda mrefu Mt.14:36; Mk.6:56, huku wengine wakipigana vikumbo kugusa vazi la Mtume Paulo na waliposhindwa walishindana walau kugusa hata kivuli chake tu. Nabii Elisha alipata mamlaka ya Kinabii baada ya kumiliki vazi la Nabii Eliya ili apate mamlaka na nguvu kama za Eliya za kutenda miujiza, yaani Elisha anarithi roho wa Eliya na kitendo hicho cha kimamlaka ya Kinabii kinadhihirishwa kwa vazi 2Fal.2 yote (hasa mistari ya 13 na 14).

Kimila mtu anapovikwa mgolole (vazi la kimila) maana yake anatawazwa kuwa kiongozi na kiongozi hawezi kuwa kiongozi pasina kuwa na mamlaka. Unapovaa bila kufuata itifaki, maana yake unapoteza mamlaka hata kama ni kiongozi mkuu, mfano Askofu, Mchungaji, Mwinjilisti, Mtendakazi au Mzee wa Kanisa akiingia ibadani akiwa amevalia mlegezo, kaptula, taiti, kitovu nje, maziwa nje, mapaja nje kwa madai mepesi tu ambayo watovu hawa wa nidhamu ya mavazi wamekuwa wakisisitiza ili kutetea utovu wao huo kuwa Mungu haangalii mavazi bali anaangalia roho; naamini watu wote watahama Kanisa hilo wakiwamo waumini hao wanaovaa kwa jinsi hiyo ya utovu wa nidhamu, watu watafasiri kwamba hilo silo Kanisa.

Kuthibitisha kuwa vazi ni mamlaka ni kwamba askari hawezi kushika zamu yake mfano kumkamata mhalifu kama hajavaa crown/kofia yenye nembo ya jeshi, vilevile hakimu hawezi kuendesha shauri kama hajavaa suti, halikadhalika jaji hawezi kuendesha shauri kama hajavaa suti na zaidi anapotaka kutoa hukumu ya kunyonga lazima avalie vazi maalum tofauti na suti ya kawaida ya kuendeshea kesi na lazima desturi au itifaki zingine zifanyike kama dua, kengele maalum igongwe, utulivu lazima utande kwenye eneo la hukumu ya kifo, ulinzi mkali wa askari lazima utande kwenye eneo husika, yote hiyo ni kwa sababu kutoa hukumu ya kukatisha uhai lazima itifaki zake zizingatiwe, lengo kuu likiwa ni kuheshimu mamlaka ambayo moja ya vigezo na masharti ya kuzingatia mamlaka hayo ni kuwa ndani ya vazi maalum lenye kuashiria mamlaka hayo kutenda kazi kwa wakati huo husika.

Wakili aliyesajiliwa haruhusiwi kuendesha kesi kama hana suti na kola maalum ya kiuwakili. Wakili huyuhuyu hupewa kola hiyo ambayo huitumia tu pale anapoendesha kesi mahakama za juu kama mahakama kuu na mahakama ya rufani na awapo katika kutenda kazi zake za uwakili katika mahakama za chini haruhusiwi kuvaa kola hiyo ilhali lazima avae suti tena nyeusi na shati jeupe pyee.

Lakini zaidi vazi ni kitambulisho, ndiyo maana wanafunzi wa Yesu walitambuliwa hata na watu wa mataifa pale walipopita katikati yao; kuwa ni wafuasi wa Yesu kwa sababu walivaa na kuenenda kama Yesu. Vivyo hivyo huhitaji kufundishwa kuwatambua wafuatao kwa taaluma/fani au kazi zao: Mchungaji, Askofu, nesi, tabibu, mlozi, mwanafunzi, askari, mwanasheria, kichaa/chizi, mfungwa, fundi, mfuasi wa timu ya mpira wa soka, kondakta, dereva, rubani, nahodha, mfanyakazi wa hoteli, mpishi/chef, muuza nyama buchani, mchunga ng’ombe, dadapoa, bradhameni, msela nk.

Mpenzi msomaji wa mafundisho haya, wewe uvaaji wako ibadani unakutambulisha kama nani? Dadapoa?! Buzi?! Mvuta bangi?! Fundi gereji?! Muumini mzuri?! Chizi?! Kondakta?! Mchunga ng’ombe?! Mlozi?! Hivi wewe umewahi kujiuliza kuwa utatoa hesabu gani Yesu anaporudi kulinyakua Kanisa? Farao aliulizwa kwamba yeye afanana na nani katika ukuu wake? Eze.31:2. Wewe msomaji wafanana na nani katika uchaji wako? Labda Herodia aliyemtamani Yohana! Labda Daudi aliyemtamani mke wa Uria! Utovu huu wa Daudi ulimchukiza Bwana 2Sam.11:27. Mathayo katika sura ile ya 6:8 anawaonya watakatifu wasifanane na mataifa. Ni unafiki kuvaa kwa hila (kwa agenda ya siri ya kunajisi ibada takatifu) na wanafiki Injili imewafananisha na makaburi Mt.23:27; Lk.11:44. Ukristo wako unasomekaje kwa mataifa? Mataifa waige lipi lililo jema toka kwako?

Wengi wanaamini jinsi ulivyo nje ndivyo ulivyo ndani haijalishi ndani uko vizuri. Na wengi wanatumia vigezo vyako vya nje (yakiwemo mavazi) kujenga mahusiano ya kidugu, kirafiki, uchumba nk, hakuna awezaye kuwa na urafiki wala kuoa chizi kwa sababu mojawapo ya viashiria vya chizi ni mavazi yake. Pia hata kwenye usaili wa kazi huwa mavazi (dress code) ni moja ya vigezo vya msingi sana vinavyozingatiwa kwenye usaili wa kazi za jumla au kazi za kitaaluma/kitaalamu hata kama kigezo hicho hakikuorodheshwa kwenye tangazo la kazi, mfano huwezi kuvaa nguo za gereji au za gari ya mkaa au za kuzibulia vyoo/maji taka au za gari la taka au za ulozi alafu ukaenda kufanya usaili wa kazi ya mhudumu wa ndege au nafasi ya ukurugenzi au ukaingia wodini kutibu wagonjwa au ukauza nyama buchani au ukauza kwenye duka la dawa au ukafanya kazi ya vipimo maabara, haijalishi kwenye usaili wa mtihani wa kuandika (written interview) umeongoza kwa kupata alama hata 100 zote.

Vilevile dadapoa hawezi kuvalia nguo za muuza mkaa au mzibua vyoo alafu akaenda viwanja (magot) kujiuza akategemea kupata mauzo/mteja siku hiyo. Kwanza nguo ya mkaa inawezaje kuonekana gizani ambapo ndiyo muda wa biashara hiyo? Je, muuza mkaa au mzibua vyoo hata kama ni tajiri kiasi gani aweza kulipa nauli ya ndege na akasafiri akiwa na mavazi ya kuuzia mkaa au kuzibulia choo wakamkubali? Je, madhabahu ya Mungu si ni zaidi ya ndege? Je, waweza kwenda kuposa binti ukali katika vazi la gereji au la kuzibulia choo au la kuuzia mkaa, au la kuuzia nyama buchani (likiwa na madoadoa ya damu ya nyama) posa yako ikakubalika? Iweje ibadani turuhusu mavazi ambayo ni kinyume na maadili, desturi na itifaki za ibada?

Wawezaje kuingia ibadani ukali ndani ya mavazi ya ufuasi au ya ushabiki wa timu ya mpira alafu utegemee kupokea hitaji lako?! Baadhi ya vijana ambao ndiyo Kanisa la kesho wanaingia ibadani wakiwa na fulana za Manchester United, Arsenal, Real Madrid, Barcelona, Liverpool, AC Milan, Chelsea, Yanga, Simba, Azam FC kama vile wakati wote (siku 7 za wiki ni mpira tu) au kama vile Kanisa ni uwanja wa soka. Unaonaje kama Jumapili moja umedamka kwa hamu kubwa kwenda ibadani kuiombea timu yako ambayo imeingia fainali na Red Devils ili ishinde (tena umeweka rehani gari, pikipiki au nyumba yako kabisa kwamba timu yako ikishindwa basi rehani hiyo ichukuliwe) na unaenda kuomba Kanisani ukiamini kabisa sawa na Lk.1:37 kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu, alafu unasubiri kwenye viti Mchungaji aingize ibada, ndiposa unamwona Mchungaji ameacha joho akavalia fulana ya Red Devils (mashetani wekundu). Anapanda mimbarini kuhubiri huku fulana yake imeandikwa Red Devils (mashetani wekundu), mara wakati wa maombezi unawadia baada ya mahubiri na hiki ndicho kipindi ulichokuwa unakisubiria kwa hamu uombewe ili rehani zako zisipotee, na sasa Mchungaji anawaita mbele wote wanaotaka kuombewa, mara anakustukia umevalia fulana ya timu yako ambayo ndiyo hiyo imeingia fainali na Red Devils ya Mchungaji, mara anakuuliza hitaji lako ni nini? Unamjibu kuwa nataka uniombee timu yangu ishinde ili rehani (nyumba, gari, bodaboda) zangu zisalimike.

Naomba kura yako.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom