SoC04 Mtaala bora wa elimu hujenga taifa imara

SoC04 Mtaala bora wa elimu hujenga taifa imara

Tanzania Tuitakayo competition threads

Frajoo

Member
Joined
May 28, 2024
Posts
12
Reaction score
3
MTAALA BORA WA ELIMU HUJENGA TAIFA IMARA.


DIBAJI.


Katika taifa letu kuna ongezeko kubwa la vijana wasio na kazi, wengi wakiitupia lawama serikali kwa uchache wa nafasi za ajira rasmi zinazotolewa,hasa tukilinganisha na idadi ya wahitimu wa elimu ya juu na kati kwa kila mwaka.Hio imepelekea kwenda mbali zaidi ,vijana wanalaumu Serikali ya chama tawala kwamba imeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa wahitimu ambao kimsingi wangezalisha ajira zisizo rasmi kwa vijana wenzao wasiofikia kiwango hicho cha elimu.

UTANGULIZI.


Kuna mijadala kwenye majukwaa mbali mbali inayoendeshwa na serikali na wadau wa maendeleo endelevu kutoka nje na ndani ya nchi , wakisisitiza vijana wachangamkie fursa zilizopo katika jamii zao na kuchukua hatua za makusudi ili kujitengenezea ajira binafsi na baadae watatimiza azma ya kuajiri wengine pia.Huku sekta ya kilimo ikiongoza kuorodheshwa kama moja ya maeneo yenye fursa kubwa,ikiwa pamoja na ujasiriamali ambao kimkakati lazima uhusike katika kila eneo ,yaani hata Kilimo wakulima wadogo wanahamasishwa kuacha kulima kilimo cha mazoea (Substance agriculture.) na kuchangamkia kilimo biashara (Agri-business.) kwa maana ya kujikita zaidi kwenye mazao ya kibiashara (Cash crops) ,eneo lingine linatajwa sana ni eneo la teknolojia ambalo nalo ni mtambuka pia, kila ambacho vijana watachagua kufanya ni lazima wahusishe teknolojia,mathalani wanachagua kilimo ni lazima kutumia mitandao ya jamii kupata taarifa za uhakika zenye tija, lakini pia kutafuta masoko kupitia mitandao, aidha wanaweza pia kujifunza namna ya kuziongezea thamani bidhaa zao ili kukusanya mapato zaidi ya kawaida,aidha kuna msisitizo wa kuthubutu kuanzisha viwanda vidogo ,ili kuitikia wito wa kuwepo kwa bidhaa nyingi zinazozalishwa ndani ya nchi (Made in Tanzania.)tuzidi kukuza pato la taifa .Hata Ubunifu haupo nyuma kwenye taifa linalotaka kujikwamua kiuchumi na kufanya ushindani wa kweli kwenye nyanja tofauti yaani Sanaa na michezo,utamaduni hadi teknolojia, na sasa kuna hili la Akili bandia ( Artificial Intelligence.)ambalo kimsingi bado kuna nafasi ya kubuni ili iweze kusaidia katika kuboresha zaidi kwenye sekta zote .

Hayo yamekuwa ni masisitizo-tija kutoka kwa wataalamu wa kimaendeleo kwa muda mrefu sasa.

HALI ILIVYO KWA UHALISIA.


Katika jamii zetu kuna wimbi kubwa la wasomi ambao hawana uwezo wa kufanya kazi zozote mbadala wa ajira rasmi.Kwani hata yale maeneo yote ambayo wataalamu wanayaorodhesha kwamba kuna fursa za kujikwamua kiuchumi, kadhalika nayo yanahitaji utaalamu kuliko hata utaaluma wenyewe, hii inamaana kwamba mfumo wa elimu yetu umejikita zaidi kwenye masomo ya nadharia kuliko mafunzo kwa vitendo.Ndio sababu leo hii kijana aliemaliza VETA anauhakika wa kujiingizia kipato, lakini mhitimu wa Chuo kikuu anateseka mtaani kwa kusubiri kuajiriwa.Mbaya zaidi hata wale waliohitimu masomo ya uchumi,biashara, ujasiriamali na masoko pia ni wahanga.

Binafsi nimekuzwa sana kifikra na wazungumzaji wasomi na wenye uzoefu wa maisha, (Motivational Speakers.)nami huwa nazingatia sana mashauri mema hususani yenye mlengo wa kujenga taifa linalowajibika kwenye mchakato wa maendeleo endelevu.Wanasema kwamba siku zote tutafute suluhisho katika kila changamoto na ni vizuri zaidi kutumia rasilimali zilizopo, yaani rasilimali watu,fedha na Mali asili.Pia wengine walisisitiza kwamba katika kila changamoto tujizoeshe tabia ya kujiuliza “Kwanini Kwanini Kwanini?”hapo tutapata uelekeo wa kufikia Suluhu ya changamoto zetu. Sasa basi nina maoni yangu kuhusu shida ya ongezeko la vijana wasio na kazi (Sio kukosa ajira pekee bali kukosa kazi kabisa.) na wapo hata wale waliofanyia kazi ushauri wa wataalamu lakini mwishowe juhudi zikagonga mwamba.Katika kujiuliza sababu ili kupata Suluhu nilipata majibu ambayo kimsingi ninaamini yakizingatiwa basi baada ya miaka 5 au 25 kabisa Tanzania itakuwa nchi yetu ya ahadi.

WAZO LANGU TUNDUIZI.

Tunahitaji kuongeza somo moja la vitendo kwenye mitaala ya elimu ya msingi hadi chuo kikuu. Somo hili pengine tukaliita “Fani” ambalo litatengewa siku yake maalumu hasa Ijumaa ili lisiingiliane na yale ya kawaida.Kila mwanafunzi kwa ushirikiano na mlezi atachagua fani aipendayo ili kupato mafunzo yake kwa vitendo mpaka atakapohitimu.Hivyo siku hio watatembelea eneo husika au watatembelewa na wataalamu hapo shuleni (Nadhani ni nzuri zaidi ili kuepusha usumbufu)
Somo hili likiandaliwa vizuri basi mwendelezo wake unakua ni kujiunga na VETA kwa wale wasiopata bahati ya kuendelea na elimu ya sekondari,elimu ya kati na ya juu.Hivyo basi somo hili litakuwa kama elimu msingi wa fani .Kwa wale watakaochagua fani kama udaktari,uinjinia, na fani nyingine ambao kimsingi zinahitaji muendelezo wa vyuo maalumu basi huu utakua ni msaada mkubwa kwao kwani watakuwa wameshajengewa msingi imara.

Ukifatilia miaka ya nyuma kulikua na mfumo wa shule za msingi za mazoezi , ambazo zilitoa mafunzo kwa vitendo kwenye fani mbalimbali zenye tija kama useremala,uashi,umeme na mengineyo,hakika ulikua ni mfumo wenye tija sana kwa wanafunzi mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi , mafunzo yalisaidia sana wasiofaulu hawakukosa kazi ya kufanya ili kuwaingizia kipato.

UMUHIMU WAKE.

Kama ambavyo nimeainisha hapo juu baadhi ya faida ya uwepo wa somo hili,ni pamoja na kujenga msingi wa taifa la wachapa kazi,litachochea ubunifu,litawarahisishia wanafunzi kuchagua kada wanazomudu,elimu ya Tanzania itakua imeongezewa thamani,kwakuwa wanayojifunza kinadharia wanafunzi watayaelewa vizuri kwa vitendo, kuongezeka kwa ajira binafsi,utekelezaji wa dira ya maendeleo endelevu kwa taifa letu, itachochea uwajibikaji wa viongozi na utekelezaji wa mipango-mikakati ya serikali,kutakuwa na uwezekano wa vijana kuwa na ujuzi wa fani zaidi ya moja ,itapunguza utoro mashuleni kwavile watoto na vijana huvutiwa kufanya yale wanayoyapenda zaidi ,lakini pia itapunguza ushiriki wa matendo maovu au uvunjifu wa maadili ,ni mrobaini wa ukosefu wa ajira kwa vijana wenye fani tofauti tofauti waliopo kwenye jamii kwakuwa watapata fursa ya kutoa mafunzo,itapelekea kujidhatiti kama taifa ili kushiriki kwenye ushindani wa kimataifa kwenye maeneo mbalimbali,(Kumbuka kuhusu Ramadhani Brothers na ushiriki wao kwenye mashindano yenye hadhi ya kidunia ya kutafuta vipaji mbalimbali hadi wakaibuka na ushindi ambao ni sifa kwa taifa letu .) pia mfumo huu utairahisishia Serikali na wadau wa maendeleo katika mchakato wa kuendeleza vipaji mbalimbali.Na mwisho tutafikia dhamiri yetu ya kutatua tatizo la ukosefu wa kazi kwa vijana hasa wasomi kwa asilimia kubwa.

WAZO PACHA.

Sambamba na hilo kwenye utekelezaji wake nadhani kuna umuhimu wa kuunganisha VETA na vyuo vinavyotoa fani husika kwenye orodha ya machaguo pale wanafunzi wanapohitimu elimu ya msingi na sekondari.Kiuhalisia wahitimu wa shule za msingi wapo wanaofikia wastani wa ufaulu unaowaruhusu kujiunga na elimu ya sekondari ,pia wapo wasiofikia wastani wa ufaulu ambao nadhani ni uamuzi wenye siha kwa maendeleo ya kundi hili, kuwekewa chaguo la kujiunga na VETA au chuo chochote kulingana na fani alioichagua shule ya msingi ,lengo likawa lilelile la kumuondoa kijana mtaani .Umuhimu wa hili ni kuwasaidia wale ambao wanakosa nafasi za kujiunga na sekondari.

UTEKELEZAJI WAKE.

Katika kutekeleza jambo hili ni lazima iandaliwe mipango saidizi ambayo haitaathiri maendeleo ya elimu nadharia ambayo kimsingi ndio msingi wa ufahamu,pia wazazi na serikali wafikie muafaka mzuri kupitia ushirikishwaji wa wananchi (Participatory approach.) ili kukubaliana kuhusu kuwapa muda wanafunzi kwaajili ya somo hilo la mafunzo kwa vitendo na gharama za kuwalipa posho wataalamu ambao watakuwa ndio waalimu mpaka pale wanafunzi watakapohitimu elimu yao aidha ya msingi au sekondari.

Pia kwa wale watakaoendelea na elimu ya sekondari somo hili litakua na muendelezo pamoja na kutumia lugha ya kingereza kama ilivyo kawaid kwa masomo yote yanayotolewa shule za sekondari.

MIFANO BORA YA KUJIFUNZA.

Katika muktadha huu napenda kuiangalia nchi ya China kama mfano bora wa kuigwa katika mpango mkakati wa kukuza uchumi ,wakati raia wake kwa asilimia kubwa wakichangia kwenye ukuaji wa uchumi.Silaha yao kubwa ni mafunzo kwa vitendo dhidi ya nadharia. Leo hii China inazalisha wataalamu wengi karibu kwenye kila kada ,nadhani mifano ipo wazi tunaona wakandarasi kutoka China wanavyochukua tenda za madaraja na barabara pamoja na miundombinu kwa ujumla hapa nchini,pia kwenye sekta ya viwanda China inazalisha wabobezi wengi.

Ikumbukwe kwamba miaka ya utawala wa Hayati Julius Kambarage Nyerere ,Rais wetu wa kwanza ,Tanzania na China hazikuachana sana kiwango cha uchumi,lakini leo hii China inatoa mchango wa ongezeko la pato la dunia kwa asilimia 30.

Kwa msisitizo huu nazidi kukoleza wino kwamba mrobaini wa changamoto ya ukosefu wa kazi kwa vijana na kudorora kwa pato la taifa ni kuongeza somo hili la “Fani” ikiwa ni mafunzo ya fani kwa vitendo iliyojikita kuzalisha wataalamu kwenye kada mbalimbali nchini.

Haya ni maoni yangu katika namna ya utekelezaji wa mpango huu,lakini Wizara ya elimu,wadau wa elimu pamoja na watunga sera kwa ushirikiano na wananchi watapata namna bora zaidi kulingana na uhalisia,sheria,taratibu na kanuni.

HITIMISHO.

Natamani kuona bidhaa kutoka Tanzania zinaongezeka kwenye soko la dunia,pia natamani kuona Tanzania ikizalisha wabunifu na wataalamu wenye kukidhi vigezo vya kimataifa.Ni faraja ilioje kuona ramani za majiji zikisanifiwa na wazawa,wakandarasi wazawa,wajasiriamali wakizipamba meza kwa bidhaa bora zenye upekee kwenye masoko na mikutano ya kitaifa na kimataifa,natamani kuona kuna mashine nyingi zinabuniwa zitazotumia gesi yetu asilia, natamani kuona changamoto za maji na Umeme zinatatuliwa na vijana kwa kutumia rasilimali tulizonazo,natamani kuiona Tanzania ikiwa na kiwanda cha magari kama ambavyo watu kama Masoud Kipanya walivyoonesha mifano, natamani kuona sekta ya kilimo inaboreshwa na vijana kwa kulima kisasa na ubunifu wa kuongeza thamani mazao kuwa bidhaa zenye tija, natamani kuona watu wanatatua changamoto za magonjwa ya Typhoid ,Kipindupindu na homa za matumbo kwa ujumla wake kwa kuja na Chujio za maji yule aliyebuni Nano Filter lakini pengine zikabuniwa zisizo na kemikali ili kuwasaidia watu waishio vijijini, natamani kuona kwenye teknolojia watanzania wanakuja na ubunifu kama Given Edward alivyokuja kuboresha upande wa elimu kwa Application yake, ya Mtabe Education au Benjamin Fernandez na ubunifu wake wa Application ya NALA kwenye huduma ya miamala .Wanahitajika vijana wengi zaidi ya hawa ambao kimsingi wanachonga barabara ili kizazi kijacho kiweze kufika nchi ya ahadi.

Asante kwa muda wenu.
Nawasilisha.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom