Mwanahabari mkongwe na mashuhuri wa kimataifa na mtangazaji mkuu wa habari za kimataifa wa CNN, Christiane Amanpour, ametangaza kuwa ataondoka katika mtandao huo Juni 2027, akihitimisha safari ya miaka 43. Amanpour, mwenye umri wa miaka 68, ametangaza uamuzi huo Jumatatu, Oktoba 19, 2026, baada ya miezi kadhaa ya kutafakari kuhusu mustakabali wake wa kitaaluma.
Katika taarifa yake, Amanpour amesema anatarajia kuanza miradi mipya baada ya kuondoka CNN, huku akiahidi kuendelea kuunga mkono mtandao huo na kutetea uandishi wa habari huru. Amesisitiza falsafa yake ya uandishi wa habari kwa kauli: “Daima sema ukweli, si kuwa upande wowote,” akieleza msimamo wake kuhusu umuhimu wa ukweli katika taaluma hiyo.
Amanpour alijiunga na CNN mwaka 1983 akiwa msaidizi katika dawati la habari za kimataifa, kabla ya kuwa mmoja wa wanahabari mashuhuri duniani. Alipata umaarufu kupitia taarifa zake kutoka maeneo yenye migogoro, yakiwemo Vita vya Ghuba, Bosnia, Rwanda, Afghanistan, Ukraine na Iran, pamoja na mahojiano yake na viongozi wakuu wa dunia.
Tangu mwaka 2009, Amanpour amekuwa akiendesha kipindi chake cha mahojiano, Amanpour, kupitia CNN International. Kuanzia Januari 2027, kipindi hicho kinatarajiwa kurushwa mara moja kwa wiki hadi mwisho wa Mei, huku akiendelea na majukumu mengine ya kuripoti kwa CNN hadi Juni 2027. Kipindi chake cha Amanpour & Company kupitia PBS kinatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka 2026.
Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa CNN, Mark Thompson, amesema amekuwa akijadiliana na Amanpour kuhusu uamuzi huo kwa miezi kadhaa. Amesema anasikitishwa na kuondoka kwake, lakini anakubali kuwa wakati umefika kwa mwanahabari huyo kuanza hatua mpya katika maisha yake binafsi na kitaaluma, akimtaja kuwa mmoja wa wanahabari wanaoaminika na kupendwa zaidi.
Kuondoka kwa Amanpour kunahitimisha zaidi ya miongo minne ya kazi katika CNN, akiripoti matukio makubwa ya kimataifa na kufanya mahojiano yaliyomjengea heshima katika tasnia ya habari. Hata hivyo, hakutaja mabadiliko ya umiliki wa kampuni mama ya CNN kama sababu ya uamuzi wake, akieleza kuwa anatarajia fursa mpya katika hatua inayofuata ya maisha yake.