Mtoto wa kike asibaguliwe kielimu

Mtoto wa kike asibaguliwe kielimu

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363

Wakati leo dunia ikiadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike, bado kuna baadhi ya jamii za Tanzania na Afrika kwa ujumla, hazijampa mtoto wa kike fursa zote muhimu ikiwamo elimu.

Mila na desturi za baadhi ya jamii hapa nchini, zimekuwa zikimbagua kwa kiasi kikubwa mtoto wa kike kupata haki yake ya elimu.

Jamii nyingi humchukulia mtoto wa kike kama asiyestahili kusomeshwa na hata wale wachache wanaobahatika, hukabiliwa na changamoto nyingi ambazo hatma yake hujikuta wakikwama kupata elimu stahiki.

Mbali ya kubaguliwa kielimu, watoto wa kike pia wanakabiliwa na changamoto za ndoa za utotoni.

Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, imekuwa kikwazo kikubwa kwa mtoto wa kike hapa nchini Tanzania kumfikisha katika matarajio na ndoto zake za elimu.
Pamoja na mambo mengine, sheria hii inaruhusu mtoto wa miaka 14 au 15, kuolewa kwa ridhaa ya wazazi.

Huu ni ukandamizaji mkubwa kwa mtoto wa kike kwa kuwa umri huo ndiyo mwafaka kwa kusoma.

Hata hivyo, tunashukuru kuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, leo jijini Dar es Salaam atakuwa ni miongoni mwa washiriki wa mjadala mpana kuhusu kumaliza tatizo la ndoa hizi za utotoni.

Mjadala huu wa leo ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), Kikundi cha Mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania yanayoshughulikia jinsia, kwa kushirikiana na Jukwaa la Graca Machel, una umuhimu wa kipekee kwa hatma ya mtoto wa kike hapa nchini. Aidha, mjadala huu ambao ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, utatoa taswira ya nini kifanyike kumsaidia mtoto wa kike ili haki zake za msingi zisiendelee kukiukwa.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Kuwawezesha wasichana, kuhakikisha haki zao za binadamu na kushughulikia ubaguzi na unyanyasaji yao dhidi ni muhimu kwa maendeleo kwa ajili ya familia nzima ya wanadamu.”

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya ndoa za utotoni duniani.

Ndoa za utotoni ni miongoni mwa mambo yanayomkwaza mtoto wa kike nchini pamoja na mambo mengine, ashindwe kupata elimu ambayo ndiyo msingi wa maisha. Takwimu zinaeleza kuwa kwa wastani, watoto wawili kati ya watano huolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.

Kwa msingi huo, sisi tunaamini kwamba mjadala huu wa leo utachochea zaidi ushirikiano ulioundwa kwa ajili ya matokeo bora kwa watoto wa kike hapa nchini kwetu. Hali kadhalika, tunaamini kwamba mjadala huu utajadili kwa kina na kutafutia ufumbuzi suala la ndoa za utotoni hapa nchini Tanzania.

Wakati wa mjadala huu, tumeelezwa kwamba Mama Graca Machelm mjane wa Rais wa kwanza wa Msumbiji, atawasalimia washiriki kwa njia ya video ambapo washiriki wote watakuwa na nafasi ya kuuliza maswali jopo la wazungumzaji na pia kushiriki mjadala kwa kuchangia mada kwa kutumia utaalam na ufahamu.

Ni faraja kubwa kwetu Watanzania kupata fursa ya mjadala kama huu ambao kwa hakika tunaamini kwamba utawafumbua macho wadau wote na hivyo kusimamia kwa umakini haki za mtoto wa kike.

Na kwa msingi huo, tunashauri kwamba wakati umefika sasa kwa serikali kuiangalia upya kwa lengo la kuifanyia mabadiliko Sheria hii ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu mtoto mwenye umri wa miaka 14 ama 15 kuolewa eti kwa ridhaa ya wazazi.

Kimsingi, kumruhusu mtoto mwenye umri huo kuolewa, ni kumkandamiza na kumnyima haki zake za hasa za kupata elimu.
Si hivyo, umri huo ni kumsababishia mtoto wa kike matatizo yanayotokana na uzazi.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya vifo vinavyotokana na uzazi, huwapata wasichana wanaoolewa katika umri mdogo.
Ni kutokana na sababu hizi na nyingine nyingi, sisi tunaposisitiza kuwa mtoto wa kike ana haki zote za kuthaminiwa kama ilivyo kwa mtoto wa kiume, hivyo apewe mambo yote ya msingi ikiwamo elimu.

Kwa bahati nzuri, baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yameungana kufanya kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake ukiwamo wa ndoa za utotoni.

Kuna mradi wa GEWE II unaoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kikishirikiana na mashirika mengine manne watetezi wa haki za binadamu hasa wanawake na watoto yakiwamo, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Kituo cha Usuluhishi cha TAMWA (CRC). Bila shaka kupitia harakati hizo unyanyasaji wa kijinsia zikiwamo ndoa za utotoni utapungua ama utatokomezwa kabisa.




CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom