jumanne, 11 Machi 2008
CUF yatoa kauli
na Saada Said, Zanzibar
SIKU chache baada ya kuibuka kwa taarifa kuwa Rais Amani Abeid Karume, amekataa mapendekezo ya kuundwa kwa serikali ya pamoja visiwani humo, iliyotolewa na kamati inayosimamia mazungumzo ya kusaka muafaka wa kisiasa, Chama cha Wananchi (CUF) kimetoa kauli rasmi kumpinga Rais Karume.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya chama hicho iliyokutana kisiwani hapa jana, na kujadili ripoti ya maendeleo ya mazungumzo ya muafakaa, ilisema baada ya kikao chake kuwa iwapo ni mstaarabu, Rais Karume anapaswa kukubaliana na mapendekezo ya kamati ya muafaka.
Hata hivyo, kamati hiyo ilikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa hata kama atakataa, Rais Karume anapaswa kutambua kuwa yeye si mmoja wa wajumbe wa kamati ya muafaka, hivyo hana uwezo wowote wa kukwamisha mazungumzo yanayoendelea kati ya chama hicho na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Mazsons mjini hapa, Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali, alisema mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa kisiasa uliopo Zanzibar ni ya Watanzania wote na si ya CUF wala ya CCM.
Alisema kwa maana hiyo, mazungumzo hayo yanamgusa kila Mtanzania.
Kama Rais Karume atakuwa mstaarabu, basi atakubaliana na maamuzi, kwa sababu wajumbe wote watakuwa wameamua na wengine wanatoka ndani ya chama chake
ni maamuzi ya pamoja kwa manufaa ya taifa, alisema Machano ambaye alikaimu Uenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya CUF kutokana na kutokuwepo kwa Ibrahim Lipumba, ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo na chama hicho.
Alimkumbusha Rais Karume kuwa uamuzi wa kukaa katika meza ya mazungumzo ni wa busara na ni ustaarabu unaofuatwa na nchi nyingi dunaini zinazotatua matatizo yao kidiplomasia.
Alisema machafuko yaliyotokea Kenya ni tofauti na ya Zanzibar, kwa kuwa Kenya ilifikia hatua ya mauaji kabla hawajakaa kuzungumza, wakati Zanzibar wameamua kuanza mazungumzo kabla hali haijawa mbaya, ingawa kinachozungumzwa kimekuwa kikijirudia kila mara.
Alisema kwa kukubali kukaa mezani na kuzungumza, CUF haijashindwa katika harakati za kusaka haki, bali ni ustaarabu utakaosaidia kumaliza uhasama na migogoro iliyopo kwa njia ya mazungumzo bila ya kupigana na kumwaga damu kama inavyofanyika nchi nyingine.
Akizungumzia hatua iliyofikiwa, alisema kuwa hakutakuwa na haja tena na kuendeleza mazungumzo baada ya maafikiano, bali utekelezaji wa kile kilichoafikiwa katika vikao.
Katika mazungumzo sasa tumefikia tamati, kilichobaki ni utekelezaji wa makubaliano, hivi sasa tunataka Baraza Kuu la Uongozi litoe maamuzi ya mwisho kwa upande wa CUF, alisema Machano.
Alisema CUF wameamua kuitisha kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama, ili kupata ufafanuzi juu ya mwenendo mzima wa mazungumzo yalipofikiwa, ikizingatiwa kwamba sasa ni miezi 14 tangu kuanza kwa mazungumzo hayo.
Sisi tumeridhika na mazungumzo, tunahitaji kuyabainisha yale tuliyokubaliana, ila tu la msingi tunahimiza subira na kuwaomba wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki kifupi kilichobakia kabla ya kupokea taarifa ya mwisho ya mazungumzo haya, alifafanua.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Taifa ya CUF imeagiza rasmi kwamba taarifa hiyo kamili ya mazungumzo ifikishwe mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa katika kikao chake cha Machi 17 mwaka huu, ili kupata maamuzi ya mwisho ya chama hicho.
Hatua hii ya sasa inakuja baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama kuibana Kamati ya Kutafuta Muafaka ya chama, kubainisha kile kilichoafikiwa katika mazungumzo hayo.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad, alisema Rais Kikwete alikuwa karibu na mazungumzo ya muafaka baada ya kuombwa na chama chake kutokana na kusuasua kwa mazungumzo hayo.
Maalim Seif alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa na waandishi wa habari kubainisha ushiriki wa Rais Kikwete katika mazungumzo hayo, hasa baada ya kufanikiwa kwa juhudi zake za kupatanisha mahasimu nchini Kenya.
Rais Kikwete alikuwa karibu kwa kiasi fulani na ndiyo maana tukafikia hapa tulipofikia, kweli tulimuomba awe karibu yetu na amekuwa karibu kwa kupitia kwa wajumbe wa chama chake kumuarifu kila kinachojadiliwa katika mazungumzo, alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alisema ni kweli walilazimika kumuomba Rais Kikwete baada ya kuona mazungumzo hayo yanasita sita. Hata hivyo, hali hiyo ilisababishwa na uchaguzi ndani ya CCM, kwani kuna masuala ambayo yalihitaji maamuzi ya kisiasa kutoka ngazi za juu, hivyo CCM waliomba wapewe muda kupisha uchaguzi wao.
Kati ya mambo yaliyojadiliwa katika mazungumzo hayo ni pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005 na tathmini zake, usawa na haki katika uendeshaji wa siasa, utawala wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, njia za kuimarisha mazingira ya maelewano na uendeshaji wa uchaguzi huru na wa haki Zanzibar, pamoja na utaratibu wa utekelezaji na programu ya utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya CUF imearifu kupokea na kuridhishwa na taarifa ya mazungumzo kati ya CCM na CUF, ikihusu ajenda hizo tano za msingi. Wakati huo huo, Kamati Kuu ya CCM imepanga kukutana leo jijini Dar es Salaam na inaaminika kuwa moja kati ya mambo yatakayojadiliwa ni maendeleo ya mazungumzo hayo ya muafaka.