muhogo mtamu

muhogo mtamu

Swahilian

JF-Expert Member
Joined
Apr 28, 2009
Posts
591
Reaction score
69
MUHOGO MTAMU


Tule muhogo jamani, chakula cha wananchi.
Wala tusione soni, tafuna ilo mibichi.
Ifuateni sokoni, hamsini tu jisachi.
Chakula cha watu wote, yupi asema ukata.

Wakulima jitumeni, muwalishe wa mijini.
Machweo u' kaangoni, watu haweshi foleni.
Yajaza mate kinywani, kwa chachandu ndo nyumbani.
Waloidharau dume, watafuna kwa aibu.

Muhogo acheni nyie, mlo wa watu wa kale.
Magandaye ubandue, chemsha mtoto ale.
Weka pahala upowe, uchambue kwa upole.
Ipo dhana ufukara, sintoiacha asili.

Mwanzo nalidhani kweli, kripsi si muhogo.
Kumbe duara pingili, vifuko vidogo vidogo.
Meno yapata shughuli, ati aponda muhogo!
Nimewaona kwa macho, wakimung’unya vigogo.

Nirudi kwetu bandani, zogo limejaa tele.
Juma ataka sahani, jasho zamtoka Sele.
Nala muhogo jamani, sina hamu na mchele.
Acheni kutushangaa, ingia mwone uhondo.

Rangi yake ni nyeupe, japo yachimbwa topeni.
Unga wake ukauke, unga wake ni shani.
Walo wagonjwa wapike, iwe afya mwilini.
Muhogo hana maringo, aishi palo ukame.

Ramadhani ndo futari, shuleni wana wakena.
Palo dhiki yasitiri, wanunuzi wang’ang’ana.
Masikini kwa tajiri, muhogo kwao dhamana.
Aina yake ni wanga, nguvu na joto mupate.

Tamatini napepea, utamu wanizidia.
Sintoacha kutetea, nitajaza sufuria.
Watasema nimefulia, sijayaona madhila.
Waungwana jilieni, muhogo chakula bora.
 
umenikumbusha kuna mtu kijijini kwetu anaitwa muhogo mchungu, yaani hauliki hata kwa ndimu na pilipili
 
Back
Top Bottom