Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania: Disemba 11, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Kesi yafunguliwa dhidi ya IGP, DPP na ZCO kutaka Mwambe apewe Dhamana au afikishwe Mahakamani. Kusikilizwa Disemba 15

Wakili Hekima Mwasipu amefungua shauri la dharura Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camilius Wambura, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu, na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO) Faustine Mafwele, akitaka mteja wake, Godfrey Mwambe, aachiwe huru mara moja au afikishwe mahakamani.

Mwasipu anadai kuwa Mwambe, aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara na baadaye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), alikamatwa na kushikiliwa kinyume cha sheria tangu Desemba 7, katika Kituo cha Polisi Kigamboni bila dhamana wala kufikishwa mahakamani licha ya kushtakiwa kwa tuhuma za uchochezi, kosa ambalo linadhaminika.

Kwa mujibu wa hati ya maombi ya kesi namba 289778/2025, familia ya Mwambe ilipopeleka chakula kituoni ilielezwa kuwa hayupo tena kituoni hapo bila taarifa rasmi ya alipopelekwa. Wakili Mwasipu ameieleza mahakama kuwa hatua hizi za Jeshi la Polisi ni uvunjifu wa haki za msingi za mwombaji na kuomba maombi hayo yasikilizwe kwa dharura ili kuzuia ukiukwaji zaidi.

Awali, taarifa zilisambaa kupitia mitandao ya kijamii zikidai kuwa Mwambe amekamatwa na kushikiliwa kwa siku kadhaa katika eneo la Kigamboni jijini Dar, huku akihojiwa kwa tuhuma zinazohusu mahusiano ya Makamu wa Rais, Emmanuel Nchimbi na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kwenye kuchochea chuki ya wananchi dhidi ya Serikali.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Disemba 15 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu

Maoni ya wananchi:
Wananchi walio wengi wameendelea kukosoa utendaji wa Jeshi la Polisi kwa kutofuata sheria licha ya maagizo ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuwataka wafuate sheria. Wamesema licha ya tuhuma za mara kwa mara dhidi ya IGP Wambura na viongozi wengine wa Jeshi la Polisi kuhusishwa na matukio ya kikatili dhidi ya wananchi, bado wamesalia katika nafasi zao bila uwajibikaji wala uchunguzi dhidi yao kufanyika, huku utekaji ukiendelea na wananchi kuishi kwa hofu kubwa.

Aidha, wengine wamesema ikiwa sababu za kukamatwa kwake zinahusiana na TEC ni kweli, basi Serikali inakosea sana na inapaswa kujitafakari, kwasababu wanachochea chuki za kidini na kuwaadhibu watu wasio na hatia. Wapo waliosema hatua hizi zinazochukuliwa dhidi ya wanaoonyesha msimamo tofauti na Serikali, zinazidi kuongeza hasira kwa umma kuliko kumaliza tatizo.

Kampeni ya kuwatetea wasanii yaanza upya mtandaoni. Majizzo ajitokeza kuwaombea msamaha; mashabiki wao wakataa

Baada ya kipindi kirefu cha ukimya na mgawanyiko kati ya wasanii na mashabiki wao, hali iliyoibuka kufuatia uchaguzi mkuu wa 2025, upepo mpya umeanza kuvuma kwenye mitandao ya kijamii. Wasanii ambao kwa kiasi kikubwa waliwekwa pembeni na mashabiki wao kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ukimya wao Serikali inapokandamiza wananchi na katika matukio ya hivi karibuni, sasa wameanza kuibuka watu kuanza kuwatetea wasanii hao, wakiwemo watu mashuhuri nchini.

Mmoja wa watu waliozua mjadala mkubwa mtandaoni ni Mkurugenzi wa vituo vya EFM na TVE, Francis Ciza (Majizzo), aliyejitokeza kuwaomba mashabiki kuwasamehe wasanii kwa kauli zao ambazo zinaweza kuwa ziliwakera kwa namna moja au nyingine. Ameeleza kuwa kususia kazi za wasanii kumewaathiri wengi wao kiuchumi na kisaikolojia, hivyo ni muhimu mashabiki kuangalia tasnia kwa ujumla na kutambua kuwa wasanii bado ni sehemu ya jamii inayowategemea kufanikisha kazi zao. Pia, Majizzo amesisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa sababu ya kuharibu mustakabali wa sekta ya burudani, na amewaomba Watanzania kuwarudishia wasanii nafasi yao ili tasnia iweze kuendelea kukua.

Maoni ya wananchi:
Wananchi wengi wakiwemo baadhi ya wasanii kama Webiro Wassira (Wakazi) na Joseph Mbilinyi (Sugu), ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu CHADEMA na amewahi kuwa mbunge wa Mbeya Mjini - wamepingana na Majizzo wakisema hana uhalali wa kuwasemea wasanii kutokana na yeye kutumia vituo vyake vya redio na TV hasa kupitia mitandao ya kijamii, kuegemea upande wa CCM na Serikali ambao wananchi wanawakosoa kutokana na matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Pia, wamemkosoa kwa kutoongelea hoja ya msingi iliyofanya wananchi kususia kazi za wasanii; ambayo ni ukimya wa wasanii kwa ukandamizaji mkubwa unaofanywa na Serikali dhidi ya wananchi huku wasanii hao wakichagua upande wa CCM na Serikali.

Wengine wamesema, wasanii hao wapo hai na wanaona yote yanayotokea, kama wanataka kusamehewa wanatakiwa kutoka hadharani wao wenyewe na kuomba msahama huo kwa dhati vinginevyo inakuwa haina maana kwani inaonekana wanachojali ni hela wanazotengeneza tu na sio athari wanayoiacha kwenye jamii.

Aidha, wapo waliosema wataendelea kuwasusia wasanii pamoja na kazi zao sababu hata baada ya Majizzo kujitokeza kuwaombea msamaha baadhi wamejitokeza kwenye mitandao hiyo na kukejeli wananchi, kuwa hata kama wamenuna sasa, hawana nguvu za kutosikiliza kazi zao. Wameongeza kuwa jambo hili limefanywa ili wasanii waweze kuandaa matamasha ya mwisho wa mwaka kama kawaida bila kujali kuwa Watanzania wengi bado wapo kwenye maombolezo, hali inafanya wazidi kuona kuwa hawastahili kusamehewa.

CHADEMA: Tunataka serikali ya mpito ya kitaifa, Samia hana uhalali wa kuwa Rais wa Tanzania

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza msimamo wake na kusema uchaguzi wa Oktoba 29 ulikuwa batili, haukuendeshwa kwa njia halali kutokana na ukiukaji mkubwa wa sheria, haki za binadamu na misingi ya demokrasia. CHADEMA inataka matokeo yote yafutwe na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ivunjwe, kwa kuwa haikuthibitisha uhuru na uaminifu wa kusimamia uchaguzi wa kidemokrasia.

Taarifa hiyo pia imemtaja Samia Suluhu kuwa mtawala asiye halali, wakidai hakupata ridhaa ya wananchi na kwamba Serikali yake inategemea mabavu na ukandamizaji. CHADEMA imeeleza kuwepo kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Pia, kimeilalamikia Werikali na Vyombo vya Ulinzi kwa kuhusika moja kwa moja katika mauaji ya halaiki, utekaji, mateso na kupotezwa kwa raia, huku kikitaka uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu matukio hayo.

CHADEMA kinataka kuundwa kwa Serikali ya Mpito isiyoongozwa na Samia Suluhu, chini ya usimamizi wa taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa, AU na SADC.

Aidha, chama hicho kimetaka uwajibikaji kwa wote wanaodaiwa kuhusika katika ukiukaji wa haki za binadamu, wakiwemo viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, na kusisitiza mageuzi makubwa katika vyombo hivyo pamoja na fidia kwa familia zilizopoteza wapendwa wao pamoja na kwa waliojeruhiwa. CHADEMA inaunga mkono mchakato wa kupata Katiba Mpya pamoja na jitihada za vijana (Gen Z) na makundi yote yanayodai haki wakiwemo viongozi wa dini na wanaharakati.

Maoni ya mwananchi:
Wananchi wengi wameunga mkono tamko la CHADEMA wakieleza kuwa hawatambui Serikali ya Rais Samia na kuendelea kuituhumu kwa mauaji ya raia yaliyotokea wakati wa uchaguzi, na uminywaji wa sauti za wananchi hasa Vyombo vya Ulinzi kuzuia maandamno yaliyopangwa kufanyika Desemba 9, 2025.

Wengine wameendelea kuhoji ukimya Serikali kuhusu miili ya wapendwa wao waliouawa wakati wa uchaguzi, wakisema wanahitaji kufanya maziko ya heshima kwa wapendwa wao kama ilivyo desturi nchini.

Jenista Mhagama, Mbunge wa Peramiho na aliyekuwa Waziri wa Afya katika uongozi uliopita afariki dunia

Mbunge wa Peramiho, Jenista Joachim Mhagama, amefariki dunia leo asubuhi baada ya kuanguka ghafla na kupelekwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ambapo baadaye alithibitishwa kufariki. Mwili wake umepelekwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ajili ya taratibu na mipango ya mazishi.

Mhagama (58) amehudumu katika serikali ya Tanzania katika awamu mbalimbali, kabla ya Serikali mpya kuundwa alikuwa Waziri wa Afya, aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo baada ya Ummy Mwalimu kutenguliwa.

Maoni ya wananchi:
Katika hali isiyo ya kawaida, wananchi wengi wamefurahia taarifa hiyo, jambo ambalo limeonekana kuanza kuwa la kawaida pale ambapo viongozi au wafuasi wa CCM wanapofariki. Aidha, wengine wamerudia kauli aliyosema Rais Samia wakati wa msiba wa Ali Kibao, “Kifo ni Kifo” hivyo waache kuleta taharuki.

Baadhi wamehisi kifo chake kimechangiwa na msongo wa mawazo kutokana na kushindwa kupata nafasi katika Baraza la Mawaziri kwenye Serikali ya sasa, licha ya kuwa mstari wa mbele kumpigia debe Samia alipokuwa Rais na hata wakati wa kampeni za Uchaguzi wa 2025.

Waziri Mkuu: Mali za viongozi wa umma zichunguzwe, lazima mtu aogope mali ya umma

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba ameiagiza Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma ishirikiane na TAKUKURU kuanzisha kitengo maalum kuchunguza mali za viongozi wa umma kwa kuanza na wenye viashiria vya rushwa ili kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za umma pamoja na uwajibikaji kwa mujibu wa sheria. Ameongeza kuwa, kila kiongozi anatakiwa kujaza tamko la mali pamoja na madeni na kisha sekretarieti ichunguze kwa kulinganisha taarifa hizo na mapato halisi.

Akizungumza jijini Dodoma, Mwigulu amesema Serikali inaendelea kuimarisha maadili kwa watumishi wa umma kutokana na changamoto zilizopo, na kuwa maadili hayawezi kuwa kamilifu kwa asilimia mia moja hivyo yanahitaji kuangaliwa mara kwa mara. Alisisitiza kuwa lazima mtu aogope mali ya umma, akisema yule ambaye hataki kuwa na nidhamu binafsi – alazimishwe na Serikali kuogopa kugusa mali ya umma.

Maoni ya wananchi:
Wengi wameona agizo la Waziri Mkuu kama maigizo yanayotumika kuwaaminisha umma kuwa viongozi wa sasa wanachukia rushwa, wanapigania utawala bora na kutaka uawajibikaji lakini kiuhalisia hali haiku hivyo. Wametolea mfano wa kauli ya Mwigulu kusema ‘wasiokuwa na nidhamu binafsi kwenye mali ya umma Serikali itawalazimisha’, wakihoji kwanini waache watu ambao hawana nidhani na kuchezea fedha za umma kuendelea kubaki madarakani wakati kuna watu wengi waadilifu na wenye uwezo wa kushika nafasi hizo?

Wengine wamesema Rais Samia katika awamu iliyopita alisharuhusu rushwa kuendelea, alipowaambia viongozi “Wale kwa urefu wa kamba zao,” wakisema hakuna kitakachobadilika ikiwa walewale waliokuwa wala rushwa wakubwa kutoka awamu iliyopita ndio wanaendelea kuongoza sasa!

Baadhi wamesema ingekuwa kweli wanataka kuimarisha uwajibikaji kwa watumishi wa umma, basi wangeanza na kuwawajibisha wale wote waliohusika kwenye mauaji ya raia wakati wa uchaguzi, mbali na hapo wanawahadaa wananchi.

Wengi wamehoji kuwa mamlaka za maadili pamoja na TAKUKURU huwa zinasimamia nini hadi viongozi wanapotekeleza rushwa, wakionyesha kukwazwa na jinsi mifumo mibovu ya kusimamia utekelezaji na uwajibikaji inavyoendelea kulinda viongozi huku wananchi wakinyanyasika.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…