Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 13, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Mhadhiri wa UDOM akamatwa na Polisi baada ya kurekodiwa akijadili maandamano ya Desemba 9 darasani, aachiwa kwa dhamana

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (ambaye hajatajwa jina) anadaiwa kukamatwa na Polisi baada ya nyumba yake kufanyiwa upekuzi na kuhojiwa kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

Mhadhiri huyo anatuhumiwa kujadili maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Disemba 9, siku ya Desemba 8 kuanzia saa 4:30 asubuhi hadi saa 7:30 mchana alipokuwa katika kipindi darasani, akidawia ‘kuwachochea’ wanafunzi kushiriki katika maandamano.

Kauli zake zinadaiwa kurekodiwa kwa siri na mtu aliyedaiwa kuwa mpelelezi na baadaye kuwasilishwa kwa mamlaka za juu, hatua iliyopelekea kutolewa kwa agizo la kukamatwa kwake.

Taarifa iliyotolewa Desemba 12 na chuo, iliwasisitiza Wahadhiri na watendaji wengine chuoni hapo kuwa makini wawapo darasani kutokana na tukio hili kuonyesha kuwa wanafuatiliwa, huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea ili kubaini hatua hatua stahiki zitakazochukuliwa.

Maoni ya Wananchi:
Wananchi wamekosoa hatua hiyo wakisema inaenda kuua elimu ya vyuo vikuu nchini kwa kufanya walimu waache kufanya majadiliano na uchambuzi kwa uwazi kwa kuhofia maisha yao na hivyo kuzalisha vijana waliojaa uoga na wanaowaza kusifia ili wateuliwe kwenye nafasi mbalimbali za uongozi na si wataalamu wanaoweza kufikiri na kujenga hoja kwenye mijadala mbalimbali, kuchochea ubunifu, kukosoa na kushauri mabadiliko chanya.

Aidha, wengine wamesema suala la kuingilia uhuru wa maoni halikubaliki iwe vyuoni, sehemu nyingine za kazi au mitaani, vinginevyo nchi itaanguka sababu watu hawatajali tena kushauri mabadiliko, wataacha Serikali ifanye itakavyo na ikifikia hatua hiyo hakutakuwa na taifa la kuongoza!

BASATA yatangaza kuahirisha utoaji wa tuzo za muziki (TMA) zilizokuwa zitolewe Desemba 13, 2025. Kampeni ya kuwasusia wasanii yaendelea

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetangaza kuahirishwa kwa hafla ya utoaji wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2025, ambayo awali ilikuwa imepangwa kufanyika Desemba 13, 2025 mpaka pale tarehe nyingine itakapotangazwa.

Uamuzi huu unakuja wakati vuguvugu la wananchi la kususia kazi za wasanii likiendelea kushika kasi, kufuatia baadhi ya wasanii kujitenga na masuala ya kijamii na kuunga mkono shughuli za watawala.

Mjumbe wa Kamati Kuu CHADEMA, Godbless Lema kupitia mitandao ya kijamii ametoa wito kwa vijana na Watanzania kwa ujumla kutoshiriki katika jambo lolote linalowahusu wasanii ‘chawa’, mfano kwa kutohudhuria kwenye matamasha, kutoangalia video zao kupitia majukwaa mbalimbali ya muziki au kutowapigia kura wanapochaguliwa kuwania tuzo, akisema wanatakiwa wawape “Ban”

Maoni ya Wananchi:
Wananchi wamepokea taarifa hiyo kwa furaha, wakieleza kuwa ni ushindi kwa mashabiki na Watanzania ambao wameamua kutounga mkono kazi, biashara, au shughuli yoyote inayohusiana na sanaa mpaka wasanii hao watakapojirekebisha na kuanza kushirikiana na wananchi kukataa ukandamizaji unaofanywa na Serikali.

Wengine wameupokea wito wa Lema kwa mikono miwili wakisema wataendelea kutounga mkono masuala yoyote yanayowahusu wasanii nchini na kufanya hilo kuwa sehemu ya maandamano yasiyo na kikomo mpaka pale haki itakapopatikana kwa watu waliouliwa wakati wa uchaguzi na matukio ya utekaji na ukiukwaji wa haki za binadamu vitakapokomeshwa.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…