Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 14, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Kiliba: Tumtii na kumuombea Rais Samia

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 14, 2025, Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba, amewasihi Watanzania kumuunga mkono Rais Samia, pamoja na viongozi wengine wa nchi, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kiraia na pia ni agizo la maandiko matakatifu. Amesema kwa mujibu wa imani ya Kikristo, kutii mamlaka ni agizo la Mungu na ni msingi wa kudumisha amani, ustawi na maendeleo ya taifa.

Ameongeza kuwa shughuli za uanaharakati mitandaoni na nje ya mitandao zinapaswa kuzingatia misingi ya amani, upendo na umoja wa taifa. Amesisitiza kuwa uanaharakati usiotumia misingi hiyo hujenga hofu, chuki na kulitenganisha taifa badala ya kulijenga.

Kuhusu matukio ya Oktoba 29 na siku zilizofuata, Kiliba amehoji kama mikakati na mbinu zilizotumiwa na wanaharakati zilitoa suluhu ya changamoto za wananchi au ziliongeza matatizo zaidi. Ameshauri umma uwajue na kuwataja waanzilishi wa mikakati hiyo aliyodai ilisababisha vifo vya raia, hasara kubwa na kugawanya wananchi kwa misingi ya dini na itikadi za kisiasa.

Maoni ya wananchi:
Wengi wamesema wanaona matamko yanayotolewa na watu maarufu wakiwemo wanasiasa hasa kutoka CCM ni mbinu za kuwaangushia lawama wanaharakati kutokana na matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi na kuisafisha Serikali ambayo ndio hasa inapaswa kuwajibika. Wananchi wamesema hawadanganyiki kirahisi, kwasababu walishuhudia yote yaliyofanyika, na kuwa waliandamana kupinga matukio ya ukandamizaji wa haki za binadamu na hawakulipwa kama inavyodaiwa.

Aidha, wengine wamesema hakuna raia anayeweza kutii mamlaka inayoua raia wake na Serikali nayokimbia uwajibikaji pale inapokosea.

Rais Samia atuma ujumbe kwa Katibu Mkuu wa UN, António Guterres

Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Kombo imewasilisha ujumbe wa Rais Samia kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), António Guterres.

Taarifa hiyo iliyotolewa leo Desemba 14, 2025 imeeza kuwa, wakati wa kupokea ujumbe huo Guterres alisisitiza kuwa ‘Tanzania inaendelea kuwa kielelezo cha amani na mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani kwa ujumla’. Aidha, Serikali imesema kuwa Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa sifa hiyo ilijaribiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, na akaipongeza nchi kwa uimara wake katika kudumisha umoja wa kitaifa na utulivu.

Guterres anadaiwa kueleza dhamira ya UN kuona Tanzania ikiendelea kubaki na umoja wake na kuwa mfano bora kwa mataifa mengine. Taarifa ya Serikali inasema kuwa amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mazungumzo ya kitaifa jumuishi na yenye tija, yenye lengo la kushughulikia chanzo cha matukio ya vurugu yaliyotokea wakati wa uchaguzi, pamoja na kuweka mikakati ya kuyazuia yasijirudie.

Vilevile, inaelezwa kuwa Guterres alithibitisha kuendelea kwa ushirikiano na msaada kamili wa Umoja wa Mataifa kwa juhudi zinazoendelea za Serikali ya Tanzania, ikiwemo msaada wakati na baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa jukumu la Tume ya Uchunguzi iliyoundwa.

Maoni ya wananchi:
Wengi wamebeza hatua hiyo ya Serikali kutuma ujumbe UN wakihisi ni propaganda za kujisafisha kutoka kwenye tuhuma zote za matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi.

Wengine wamehoji uhalisia wa kauili za Guterres, wakisema hawaamini kuwa amesema maneno hayo mpaka watakapoona video akiwa akiyazungumza, kwani wanadhani ni mbinu ya Serikali kujisafisha na kujionyesha kuwa inakubalika na mataifa pamoja na taasisi za kimataifa.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…