Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 3, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Serikali yawafutia mashtaka watuhumiwa 219 wa kesi ya uhaini wakiwemo Niffer na Mika

Jumla ya watuhumiwa 219 waliokamatwa kufuatia maandamano na vurugu za baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 wameachiwa huru leo nchini kote, baada ya Serikali kupitia ofisi ya DPP kuiarifu mahakama kuwa haitaki kuendelea na mashtaka yao chini ya kifungu cha 92 cha CPA. Kwa mujibu wa LHRC kupitia Wakili Maduhu William, walioachiwa ni pamoja na 53 Dar es Salaam, 105 Arusha, 34 Mafinga, 18 Dodoma na 9 Kahama.

Uamuzi wa ofisi ya DPP hauhitaji sababu na mara tu tamko linapotolewa, mashauri yanafutwa moja kwa moja. Hata hivyo, Dar es Salaam bado kuna watuhumiwa 10 wanaosubiri kurejea mahakamani Jumatatu ijayo, ambapo inatarajiwa hati ya mashtaka inaweza kubadilishwa na mashitaka makubwa kama uhaini kushushwa hadi yanayoruhusu dhamana.

Miongoni mwa waliokuwa wakifuatiliwa zaidi kwenye mashataka hayo ni Jeniffer Jovin (Niffer) na Mika Chavala, ambao nao pia wameachiwa huru. Baada ya kuachiwa, Niffer aliwashukuru waliomuombea ambapo muda mfupi baadaye aliongea na wanahabari akitoa wito wa amani, busara na kuwahimiza vijana kutambua athari za matendo yao. Pia, alimshukuru Rais kwa hatua iliyoruhusu arejee kwenye maisha yake bila vikwazo vya kisheria, akisema hana chama cha siasa na hajihusishi na siasa.

Maoni ya wananchi:
Mjadala mkubwa umetokea baada ya Niffer kumshuruku Rais Samia kwa kuagiza wafutiwe kesi pamoja na kutoa wito wa amani kwa vijana kutojihusisha na vurugu kwani uhuru ni wa thamani. Wananchi wanasema amepewa maagizo ya kutoa shukrani na wito huo ili kuwashawishi vijana kutoshiriki kwenye maandamano mengine.

Wengine wamesema watuhumiwa hao kuendelea kufutiwa kesi ni namna ya Serikali kuonyesha inataka maridhiano na amani irejee nchini, lakini haviwezi kutokea mpaka wale wote waliosababisha wananchi kuuawa kuwajibishwa pamoja na Serikali kuvunjwa ili kupisha uchaguzi mwingine ufanyike, wakisema hawakuwachagua.

Serikali yamfungulia mashtaka ya Uhujumu Uchumi Mwanaharakati Mange Kimambi

Mwanaharakati maarufu kupitia mitandao ya kijamii, Mange Kimambi, ambaye anaishi Marekani, amefunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi, akidaiwa kujihusisha na utakatishaji wa fedha kiasi cha Tsh. Milioni 138.5. Kesi ya jinai namba 000021172 ya mwaka 2025 ilifunguliwa Agosti 28, 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, na imepangwa kutajwa Desemba 4, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Mange anadaiwa kujipatia fedha hizo kati ya Machi 1 na 31, 2022, akifahamu kuwa ni zao la uhalifu. Aidha imeelezwa kuwa alizipata kwa kufanya kazi ya uandishi wa habari bila kibali pamoja na kuzidai kwa vitisho. Shtaka linatokana na kifungu 12(1)(d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha Sura ya 423 ya mwaka 2019, likisomwa sambamba na Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Disemba 2 Mange alitoa taarifa kupitia mtandao wa kijamii akithibitisha kupokea taarifa za kufunguliwa kwa kesi hiyo, akidai kuwa Serikali ya Tanzania imedhamiria kumrejesha nchini na kumfunga kutokana na kuikosoa serikali pamoja na kuibua ufisadi unaofanywa nchini.

Ikumbukwe, Novemba 5 Mwanasheria Mkuu Mpya wa Serikali, Hamza Johari, alisema ofisi yake inatazama namna ya kumchukulia hatua Mange kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano, akisema Serikali ingetumia mikataba ya ushirikiano na Marekani kutathmini uwezekano wa kumrejesha mtuhumiwa nchini. Johari aliongeza kuwa hawawezi kumwacha Mange ‘atambe’ kwa kuhamasisha Watanzania kufanya maandamao bila ya wao kuchukua hatua yoyote, akieleza kuwa ameagizwa kufanya hivyo baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo!

Pamoja na hayo kutokea, kurasa za mitandao ya kijamii (Instagram) ya mwanaharakati huyo zimefungwa na META huku ukurasa wa mwanaharakati mwingine, Maria Sarungi zikizuiwa kuonekana nchini Tanzania baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwasilisha matakwa ya kisheria kwa META.

Maoni ya wananchi:
Wengi wamekosoa jaribio hilo la Serikali wakisema ni kupoteza muda na rasilimali za nchi ambazo zingeweza kutumika kufanya mambo mengine ya msingi. Wameongeza kuwa, badala ya kuwasumbua wanaharakati pamoja na wananchi wanaoikosoa Serikali, kuwateka na/au kuwaua; wanatakiwa kuwajibika kutokana na matendo yao pamoja na kuhakikisha mwananchi anapata huduma bora kwani hiyo ndio njia pekee ya kuleta haki na watu wakaishi kwa amani.

Aidha, wengine wanasema Serikali inazidi kuharibu mahusiano ya kidiplomasia na nchi nyingine pamoja na kuongeza hasira kwa wananchi jambo ambalo linaendelea kutishia hali ya kiuchumi pamoja na ustawi wa nchi.

Kuhusu kurasa za mitandao ya kijamii za wanaharakati hao kufungwa na kuzuiwa kupatikana nchini, baadhi wameieleza Serikali ya Tanzania kuwa hawawezi kushindana na teknolojia na kwamba kadri wanavyozidi kuzuia uhuru wa maoni ndivyo wananchi wanavyopata nguvu ya kuongea zaidi na kudai haki zao. Wamesisitiza, wataendelea na msimamo wao mpaka pale wale wote waliohusika na mauaji kuwajibishwa na madai yao yote kufanyiwa kazi.

Polisi: Wakataeni wanaotaka kuturudisha kwenye machungu na madhara tuliyopata Oktoba 29, hatuhitaji tena vurugu

Jeshi la Polisi nchini limetoa onyo kuhusu ongezeko la ‘uhalifu wa kimtandao’ na taarifa za kupanga ‘vurugu’ zinazodaiwa kuenezwa kupitia mitandao ya kijamii kuelekea Desemba 9. Katika taarifa iliyotolewa Desemba 3 na Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, DCP David Misime, amesema Jeshi hilo linaendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaohamasisha uhalifu mtandaoni, ikiwemo makundi yanayotangaza kile wanachokiita “Maandamano ya amani yasiyo na kikomo”.

Kwa mujibu wa Polisi, baadhi ya wafuasi wa makundi hayo wanadaiwa kutoa maelekezo hatarishi kama; kuwataka waliofunzwa kutumia silaha kushika majukumu maalum siku hiyo, kutaka shughuli zote nchini zisimame, kuharibu na kuchoma minara ya mawasiliano ili Taifa likose huduma za mawasiliano, kufunga barabara zinazoingia na kutoka bandarini Dar es Salaam, kufunga mipaka ya nchi, kupora mali za wananchi kwa kisingizio cha njaa, kuzuia huduma hospitalini, na kuwadhuru watumishi wa Serikali.

Polisi imesema mipango hiyo ni tishio kwa usalama wa wananchi, uchumi wa nchi na utulivu wa kijamii, na imewataka wananchi kuikataa na kutoshiriki katika wito huo. Polisi imewaomba Watanzania kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudumisha amani na kuepusha kurudia machungu ya vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi, Oktoba 29.

Maoni ya wananchi:
Wengi wameonyesha kuchukizwa na tamko la Polisi wakisisitiza kuwa wasithubutu kuzuia maandamano yanayopangwa kufanyika Desemba 9, kwani ni haki ya kikatiba kama inavyoelezwa na Katiba kupitia Ibara ya 20(1); wameongeza kuwa, kuzuia haki hiyo ni kukandamiza uhuru wa raia na matumizi mabaya ya madaraka.

Kadhalika, baadhi ya wananchi wamesema kuwa kama kweli Polisi wana taarifa za watu kutumia silaha siku hiyo, basi hatua zichukuliwe mapema dhidi ya wahusika kama sheria inavyotaka, badala ya kulalamika na kusubiri hadi siku ya maandamano ili wapate uhalali wa kuua wananchi kama ilivyotokea Oktoba 29.

Aidha, wengine wamesema matamko pamoja na doria za Jeshi hilo wakati huu ni mbinu ya kuwatisha wananchi ili wasitoke kuandamana, wakiwasihi wenzao kutokubali kutishika na badala yake kujitokeza kwa wingi ili kurudisha utawala wa sheria na kukomesha vitendo vinavyokiuka haki za binadamu nchini.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…