Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 4, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Kesi ya Mange yaahirishwa hadi Januari 28, 2026, Upelelezi haujakamilika

Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 000021172 ya mwaka 2025 inayomkabili mwanaharakati Mange Kimambi imeahirishwa hadi Januari 28, 2026, baada ya upande wa Jamhuri kuiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hassan Makube kuwa upelelezi bado haujakamilika. Shauri hilo liliitwa leo Desemba 4, 2025, ambapo upande wa utetezi haukuwa na wakili, na mahakama ikaelekeza kwamba taratibu zote zikamilishwe kabla ya tarehe mpya ya usikilizwaji.

Mange anakabiliwa na shtaka la utakatishaji wa fedha kiasi cha TSh138.5 milioni, akidaiwa kujipatia fedha hizo kati ya Machi 1–31, 2022 jijini Dar es Salaam kwa kufanya kazi ya uandishi wa habari bila kibali pamoja na kuzidai kwa vitisho, kinyume na Sheria ya Utakatishaji Fedha na Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Maoni ya wananchi:
Wengi wameonyesha kejeli, wakisema Serikali ilishazoea kuwaonea Watanzania na kuwaumiza kwa kutumia mahakama kutokana na mamlaka ya Rais kuwa makubwa, na kwamba sasa wanahaha sababu wamefika sehemu ambayo utawala wa sheria unasimamiwa kukiwa hakuna ubabaishaji wa kuwaonea wapinzani au wanaharakati kwa kuikosoa Serikali.

Aidha, wapo walioendelea kukosoa Jamhuri kufungua kesi hiyo wakisema inafanya matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kesi za kisiasa ambazo hazina msingi, badala ya kuelekeza nguvu kwenye masuala muhimu ya wananchi.

Marekani kutathmini upya uhusiano wake na Tanzania. Wataalamu wa UN walaani yaliyotokea

Marekani imetangaza kuanza kufanya tathmini upya ya uhusiano wake wa kibalozi na Tanzania, ikieleza kuwa matukio ya hivi karibuni nchini yamezua wasiwasi kuhusu usalama, demokrasia na mazingira ya uwekezaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya Naibu Msemaji Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tommy Pigott, hatua mbalimbali za Serikali ya Tanzania, zikiwemo tuhuma za kukandamiza uhuru wa dini na uhuru wa kujieleza pamoja na vikwazo vinavyowakumba wawekezaji wa Marekani, zimeifanya Washington kuanza kupitia upya mustakabali wa ushirikiano huo.

Pigott amesema matukio ya ukatili dhidi ya raia kabla na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29 yameongeza wasiwasi kuhusu kuaminika kwa Serikali ya Tanzania kama mbia wa muda mrefu. Marekani imeonya kuwa vitendo hivyo vinaweka hatarini raia wake, watalii na maslahi yake ndani ya Tanzania, na kusisitiza kuwa mustakabali wa uhusiano wa kibalozi utategemea hatua zitakazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kipindi kijacho.

Wakati huohuo, Wataalamu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa wameilaumu Tanzania kwa kile wanachosema ni kuongezeka kwa ukiukwaji wa haki za binadamu baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, wakiripoti madai ya mauaji ya kiholela, kupotezwa kwa lazima, na ukamataji kwa wingi dhidi ya waandamanaji, viongozi wa upinzani na asasi za kiraia. Wamesema Serikali inapaswa kutoa taarifa kuhusu watu waliopotea, kuondoa vizuizi vya habari vinavyodaiwa kuwepo, na kuanzisha uchunguzi huru na wa kina kuhusu matukio hayo.

Maoni ya wananchi:
Wengi wamesema haya ni matokeo ya hotuba ya Rais Samia katika kutano na wazee wa Dar es Salaam uliofanyika Desemba 2, aliposema kuwa Tanzania haiwezi kupelekeshwa wala kupangiwa la kufanya na mataifa ya nje kwani siyo koloni lao tena, akisema kuwa misaada wanayotoa ni kidogo na wakati huu haipo, akihoji kwa namna iliyotafsiriwa kuwa ni kejeli na kiburi, “Who are you? Kutokana na tamko hilo wengi wanaona hali ya uchumi wa Tanzania itazidi kudorora wakisema Marekani wanaweza kufungua milango kwa nchi nyingine zaidi kuiwekea vikwazo Tanzania.

Wengine wameendelea kupongeza taasisi za kimataifa pamoja na nchi za Magharibi kuonyesha kuchukizwa na yaliyotokea wakati wa uchaguzi pamoja na kutaka uwajibikaji ufanyike, wakisema sauti hizi zikiwa nyingi, Samia na Serikali yake hawatakuwa na cha kufanya zaidi ya kuwajibika! Wapo waliosema matamko haya yanazidi kuharibu taswira ya Tanzania kimataifa, mahusiano na nchi nyingine pamoja na fursa kwa vijana.

Ubalozi wa Canada nchini kusimamisha huduma Desemba 8 hadi 10

Ubalozi wa Canada nchini Tanzania umetangaza kusitisha utoaji wa huduma za ana kwa ana kuanzia Desemba 8 hadi 10. Taarifa iliyotolewa Desemba 4 kupitia ukurasa wao wa X (Twitter) imeeleza kuwa huduma zote za kawaida za ubalozini hazitapatikana katika kipindi hicho.

Hata hivyo, ubalozi umefafanua kuwa huduma za dharura kwa raia wake waliopo Tanzania zitaendelea kupatikana saa 24 kwa siku kupitia Kituo cha Dharura cha Ufuatiliaji na Majibu (Emergency Watch and Response Centre).

Maoni ya wananchi:
Wengi wametafsiri taarifa hiyo kama namna ya ubalozi huo kutambua mpango wa Maandamano yanayopangwa kufanyika desemba 9, na hivyo kupisha tukio hilo muhimu kufanyika kwa nafasi kwani ni haki yao (Watanzania) Kikatiba.

Wengine wameeleza kuwa inasikitisha kuona balozi za nje zikitambua umuhimu na haki ya wananchi kuandamana wakati mamlaka za ndani, hasa vyombo vya ulinzi, zinaendelea kutoa vitisho kwa raia pamoja na kukamata watu kutimiza wajibu wao.

Meta walipewa amri ya kisheria na TCRA kuzuia akaunti ya Instagram ya Maria Sarungi, Mange alikiuka sheria za Meta

Mwandishi wa habari wa CNN, Larry Madowo ameweka wazi majibu ya kampuni ya Meta kuhusu sababu za kuzuiwa kwa akaunti za wanaharakati wa Kitanzania Mange Kimambi pamoja Maria Sarungi, baada ya kuhoji hatua hizo.

Meta imeeleza kuwa akaunti ya Instagram ya Mange Kimambi imefutwa kabisa na pia amezuiwa kutumia WhatsApp kwa sababu ya kukiuka mara kwa mara sera za kampuni, hususan sera ya urejeshaji wa uhalifu, ambayo hairuhusu watumiaji kufungua akaunti mpya zinazofanana na zile zilizofutwa kwa makosa ya awali.

Kuhusu Maria Sarungi, Meta imethibitisha kuwa akaunti yake ya Instagram imezuiwa kuonekana nchini Tanzania kufuatia amri ya kisheria kutoka TCRA. Meta imesisitiza kuwa inathamini uhuru wa kujieleza, lakini inalazimika kutii matakwa ya udhibiti wa ndani ya nchi inapopewa maelekezo ya kisheria.

Maoni ya wananchi:
Baadhi wamesema kuwa hatua ya kuzuia na kufungia akaunti za wanaharakati hao hazitarudisha nyuma nguvu na jitihada za wananchi kuendelea kudai haki na kupaza sauti kupitia mitandao ya kijamii, wengi wakiituhumu Serikali kuhusika kwani mitandao imekuwa ikitumiwa kufichua maovu mengi yanayofanyika nchini.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…