Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania: Novemba 12

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Chama cha Mawakili wa Serikali chalaani vikali vurugu na maandamo ya Oktoba 29, wadai maandamano hayakuwa halali
Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kimelaani vikali vurugu, mauaji na uharibifu wa mali vilivyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu 2025, na kutoa pole kwa waathirika huku kikiunga mkono agizo la Rais Samia la kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya wahusika waliofanya vurugu wakati wa uchaguzi huo.

TPBA imeeleza kuwa, maandamano ya Oktoba 29 hayakuwa halali kwa kuwa yalikiuka zuio la Polisi, huku ikisisitiza matumizi ya nguvu kubwa yalikuwa ya lazima na kwa uwajibikaji wa kisheria. Pia kimeeleza kuwa udhibiti wa mawasiliano ya intaneti unaweza kufanywa kisheria kwa ajili ya Usalama wa Taifa, na kukumbusha kuwa haki huambatana na wajibu wa kuheshimu Katiba na Mamlaka halali.

Chama hicho kimetoa wito wa utulivu, umoja na mazungumzo ya maridhiano ili kudumisha amani ya Taifa.

Maoni ya wananchi:
Wananchi wengi wamekosoa msimamo wa TPBA wakisema chama hicho kimeonyesha kujiondoa kutetea maslahi ya wananchi na haki za kikatiba, hasa pale panapotetea matumizi makubwa ya nguvu kutoka kwa vyombo vya dola.

Wengine wameshangazwa na tamko hilo lililoegemea kulaani maandamano badala ya mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola. Baadhi wamepinga suala la maridhiano wakisema hayawezi kuwepo bila uwajibikaji kwa wote waliosababisha mauaji.

Lissu aweka mapingamizi kwa mashahidi wa kificho, kesi yaahirishwa kwa muda usiojulikana
Kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, imeahirishwa hadi Msajili wa Mahakama atakapopanga ratiba, baada ya Lissu kupinga chumba ambacho aliwekwa shahidi ‘P11’ ambaye ni shahidi anayelindwa (shahidi wa kificho).

Lissu ameeleza kuwa shahidi anatakiwa kukaa kwenye eneo ambalo ataonekana na Jaji au Hakimu pekee bila kuonekana na watu wengine. Hata hivyo Lissu amesema chumba kilichopo mahakamani jaji hawezi kumuona shahidi pindi kesi inapoendelea.

Aidha, amepinga uhalali wa sheria ya ulinzi wa mashahidi akidai haijachapishwa katika gazeti la serikali, huku akieleza kuwa majaji hawajapewa orodha ya mashahidi waliolindwa kinyume na agizo la awali la mahakama.

Upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga, umeomba muda zaidi kujibu hoja hizo.

Maoni ya wananchi:
Wengi wanona ni ubabaishaji tu wa Jamhuri kuendelea na kesi hiyo wakidai hakuna kesi ila Serikali wanahofu ya kumwachia huru kutokana na nguvu aliyonayo kwa umma.

Heche: Vyombo vya kimataifa vifanye uchunguzi kilichotokea Oktoba 29
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, ametaka uchunguzi ufanyike na Vyombo Huru vya Uchunguzi vya Kimataifa kufuatia mauaji makubwa ya watu yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, na sio vyombo kutoka ndani ya nchi kwa kuwa ndivyo vinavyotuhumiwa.

Pia, Heche ametangaza kuwa CHADEMA kimetoa mawakili nchi nzima kwa ajili ya kuwasaidia wote wanaokabiliwa na kesi za uhaini kufuatia matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi akisisitiza kuwa hakuna kurudi nyuma mpaka ukombozi upatikane.

Maoni ya wananchi:
Wananchi wamepongeza hatua ya CHADEMA kutoa wito huo wakisema msukumo ukiendelea kutoka kwa vyombo na taasisi za kimataifa haki itapatikana na wote waliohusika kwenye mauaji ya Watanzania watawajibishwa. Wengine wamepongeza juhudi za chama hicho kwenye kuongeza mawakili wa kuwatetea wananchi wanaoshtakiwa kwa ugaidi ili kuhakikisha mtu anapata uwakilishi mzuri juu ya kesi hizo na haki inapatikana.

Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini akamatwa na Polisi ‘wakihisi’ anataka kutoroka nchini
Watu waliojitambulisha kuwa ni Askari Polisi wamemkamata Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kaskazini, Wakili Samwel Welwel, maeneo ya Kibaoni Arusha, akiwa anaelekea kijijini kwao Karatu.

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Mwenyekiti huyo amepelekwa kituo cha polisi Karatu na anahojiwa kwa sababu "wanahisi" anataka kutoroka nchini.

Maoni ya wananchi:
Wananchi walio wengi wamekasirishwa na matukio ya watu kukamatwa kiholela na Jeshi la Polisi, huku wakiona sababu iliyotolewa kumkamata kiongozi huyo haina mashiko wala msingi wa kisheria.

Wananchi wanasema vitendo hivyo vinazidi kuporomosha imani ya wananchi kwa vyombo vya sheria na kulazimisha hofu isiyo na sababu.

Nondo amjia juu Mwenyekiti wa UVCCM, alaani mauaji ya waandamanaji, asema yanahitajika maridhiano kwa makundi yote nchini
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo Taifa, Abdul Nondo, amelaani mauaji ya wananchi waliouawa kwa risasi wakati wa maandamano, akisema hakuna sheria inayoidhinisha mtu kuuawa kwa kosa la kuandamana bila kibali akikisitiza wote waliohusika kwenye mauaji hayo wanatakiwa kuwajibishwa baada ya uchunguzi wa kina kufanywa.

Akijibu kauli za viongozi wa Serikali na Mwenyekiti umoja wa vijana (UVCCM), Mohammed Kawaida, Nondo amesema badala ya kutumia risasi, Polisi walipaswa kuwakamata na kuwapeleka mahakamani.

Nondo pia ametoa wito wa maridhiano ya kitaifa yanayoshirikisha makundi yote ya kijamii, kisiasa na kidini, akisema maridhiano hayo yanapaswa kuratibiwa na mhusika huru (mtu wa tatu) badala ya Serikali ili kuhakikisha haki, uwazi na ushirikishwaji wa kweli, ili kujenga umoja wa kitaifa na kuponya makovu ya kijamii.

Maoni ya wananchi:
Wananchi wengi wameonyesha kutoridhishwa na wito wa maridhiano, wakisema ACT-Wazalendo na vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi vinapaswa kubeba sehemu ya lawama kwakuwa wananchi walitaka maridhiano kabla ya uchaguzi lakini wakapuuzwa.

Aidha, wengine wamemkosoa kwa kumuita mnafiki yeye pamoja na chama chake maana wanakuja kwa wananchi kwakuwa walishindwa kulinda kura na hivyo wanatumia nafasi hii kama sehemu ya kutoa hasira yao kwa CCM.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…