Mustakabali wa Jamii

Mustakabali wa Jamii

Nayyar

New Member
Joined
Jul 16, 2021
Posts
2
Reaction score
3
July 30th 2021

MUSTAKABALI WA JAMII

Ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwanza kwa kunipa pumzi na fahamu za kuweza kuweka mada hii mbele ya jamii. Naomba aniwezeshe ili niweze kufikia jamii husika kuhusu mada hii mahsusi kwa rika zote, kabila zote, wake kwa waume na dini zote. Naomba tusafiri katika safari yangu hii sote kwa pamoja nikikunjua mwelekeo wa ummah.

Tukianza kuangalia mapinduzi ya wanawake duniani kote, Umoja wa Mataifa ulifanikiwa kutayarisha mikutano mikubwa minne. Katika mkutano wa kwanza uliofanyika katika jiji la Mexico mnamo mwaka wa 1975. Katika mji wa Copenhagen mnamo 1980. Katika mji wa Nairobi hapa jirani, mwaka wa 1985 na mkutano wa nne katika mji wa Beijing mnamo mwaka wa 1995. Katika mikutano yote, mkutano wa Beijing ndio uliotia fora na kuwa ‘’turning point’ kwa wanawake dunia nzima. Maazimio yake yalileta mwamko miongoni mwa wanawake kote duniani katika nyanja mbali mbali kama ujasiriamali, nyadhifa za serikalini, ufundi, usafiri, afya n.k. Wanawake waliweza kuvamia hizi nafasi. Kilichoonekana ni kutengwa au ubaguzi dhidi ya mwanamke. Haukuishia hapo, ila walijadili maswala ya mwanamke na usawa (gender equality).

Nafikiri baadhi yetu kama siyo wote, ni washuhuda wa athari za mkutano huu wa Bejing. Kitokeo cha hapo, vuguvugu kali sana lilipita na kuhamasisha mataifa mengi kuhusu ‘’haki za mwanamke.’’ Hili wimbi lilileta mwamko na msisimko haswa katika bara hili letu la Afrika. Tukashuhudia namna serikali zilivyong’ang’ana kuweka nafasi za wanawake katika nyadhifa mbali mbali. Ikawa ndiyo gumzo mitaani. Ni jambo lisilopingika ya kwamba hili lilizua mwamko fulani kwa wakina mama aidha hasi au chanya kwa jamii nzima haswa yakitanzania mijini na vijijini.

Wanawake wakaanza kujitokeza wazi wazi kudai ‘’haki’’ zao katika sehemu tofauti tofauti. Majumbani mkawa hakukaliki kwasababu mama alihisi amekuwa ‘’empowered’’ yaani amewezeshwa kutoka nje na kufanya kazi azifanyazo mwanamume. Mama akahisi yeye ni mtafutaji na ni muhangaikaji na ndivyo ‘’haki’’ zake zingepatikana. Mama akatelekeza majukumu yake na kukimbilia majukumu ya nje na pengine yasiyomuhusu.

Kuna haki, majukumu, maadili na tamaduni lazima vizingatiwe katika jamii mara zote endapo uamuzi fulani utafanyika. Hili ni la muhimu siku zote. Na lazima kuwe na ‘’thinkers’’ au wanafalsafa katika nchi amabao wataona mbele na kutoa ushauri kabla ya maamuzi kufanyika yanayohusu jamii. Kujua tatizo ni nusu ya kulitatua.

Tunasonga mbele, kama haitoshi, jamii inafaa kuwa na wasomii wa kike na wakiume katika nyanja za elimu, hospitali, serikalini, ujenzi, usafiri na hata jeshini lakini iangaliwe nani anashika nini na kwa wakati gani na muda gani. Hili halikuangaliwa vizuri. Sababu mwanamke aliingizwa bila kujali maumbile yake, majukumu yake, maadili yake, haki zake na kila kitu chake, katika sekta tofauti tofauti hivyo kupelekea kusahau jukumu lake kubwa na zito la ‘’ULEZI’’.

Tulimkuta mwanamke viwandani, ujenzini, kama ni dereva, na katika kila sekta uijuayo wewe, biashara ndiyo usiseme, mama aliingia hivyo kusahau jukumu lake la kujenga jamii na kusimamia ulezi kule nyumbani. Mwanamke alisafiri katika nchi mbali mbali katika mambo ya kibiashara. Mwanamke alitoka bila kuzingatia umbile lake, jukumu lake na tamaduni yake, akaenda kufanya kazi ya ‘’watchman’’ au udereva wa safari ndefu au utingo na nyingi nyenginezo.

Jukumu la kulea akawachiwa baba. Baba akang’ang’ana sana na pia bado anashikilia hiyo nafasi lakini ilifika mahali akaona kheri amwachie mdada wa kazi au ‘’aunty’’ ukipenda. Huyu baba ameona mama sasa amenogewa na kutafuta, kwa hivyo ameamua yeye akae nyumbani na mama aendelee kutafuta. Wazungu wanasema, ‘’the tables have turned’’. Ndiyo tunayoyashuhudia sasa hivi katika jamii. Kuwa asilimia 50 mpaka 60 ya jamii Africa nzima na duniani mwanamke ndiyo anayetafutia jamii ilhali wanaume wao ni kupewa pesa ya kutumia na wanawake.

Vijijini mama ndiyo mwenye kwenda shamba akamwacha baba na wanawe. Atatoka shamba aende kwenye vyama vya vikoba n.k ili tu mwisho wa siku aweze kuweka chakula mezani. Wale mjini hali kadhalika. Baba ataendelea kulala, akiamka aende kuoga na kula na kwenda kwenye mabaraza ya kucheza karata, bao au kunywa kahawa na kushabikia mipira. Hapo kashaachiwa nauli ya kufanyia mizunguko yake.

Wakati huo mama katoka ameenda kazini, amehakikisha ameacha chakula nyumbani ili watoto wasishinde njaa. Mwisho wa mwezi pia atafute kodi. Yeye akiulizwa hana au ‘’kamuulize maa’’. Huyu mama atahangaika kutwa baba ame-relax. Kweli ‘’the tables have turned’’. Si Tanzania wala Nigeria, wala Congo wala magharibi, ni kila mahali mwanamke amekuwa yeye ndiye muhangaikaji. Si alitaka mwenyewe lakini? Ametaka haki amepewa. Cha kusikitisha ni kuwa hii ‘’haki’’ ni ya majukumu tu, masikini!!! Yote kaachiwa yeye. Asomeshe watoto yeye, alipe kodi ya nyumba yeye, anunue nguo yeye, chakula pia yeye, Ameyataka!

Wanawake siku hizi ndiyo wamiliki wa makampuni, magari, mashamba na kila aina ya utajiri, wanaume nao wanangojea kulelewa. Wanawake wanaona sifa lakini wapi? Wanaumia sana. Vilio hivi vipo kila mahali. Wanawake wanateseka na wanaume wamebweteka na kuwaachia majukumu yote. Na sasa imekuwa kinyume, yule mwanamke mwenye pesa ndiye atakiwae. Matokeo ni kama yale tunaosikia ‘’Serengeti boys’’ na pwani wale ‘’ma-beach boys’’ wenye kubebwa na wamama wa kizungu. Maadili yameporomoka. Familia zimeparaganyika. Ndoa hazidumu.

Watoto wamepotea hawajui wamuige nani baba hayupo, na mama ameenda ‘’Dubai’’, dada asipotembea na baba basi anabadilisha badilisha watu wanaokuja mle nyumbani. Mtoto kama siyo kulelewa na katuni, social- media au picha chafu, anampeleka shule ya bweni tangu akiwa na miaka miwili. Masikini! Yule mtoto hamjui baba wala mama wala bibi/babu mpaka baada ya miezi sita akiwa likizo. Kisha akiwa chokoraa tunamtafuta mchawi.

Akiwa shoga/ msagaji tunasema karogwa.Akilawitiwa na babake mdogo fitina kubwa imeikumba familia! Wewe mama ulikuwa wapi kumpa malezi bora? Ulikuwa wapi kumzuia mwanao asidhuriwe na jamii inayomzunguka? Ulikuwa wapi kumfundisha yale yanayofaa/yasiyofaa? Kumjengea ujasiri? Yabidi tuchukue tahadhari sasa!

Ndoa nazo hazidumu sababu ni hii hii. Wanaume washindani na wanawake ndiyo usiseme ati kwa kuwa walienda Beijing kwa hivyo wanatambua haki zao. Hawataki kuheshimu ndoa zao, utamaduni wao na dini zao. Ndoa zimepoteza maana siku hizi si hapa kwetu tu ni dunia nzima. Watu hawana utu si hapa ni kote ulimwenguni.

Waume wanaangamia ulevini au wanajitia vitanzi, wengine wanawaua familia zao, wengine wanatelekeza familia. Na la ajabu ni kwamba sisi tuliharibika, na kizazi hiki chetu kimeharibika, hatujui huko mbele kutakuwaje? Tunalea watoto wetu kimayai mayai matokeo ni kuwa wao pia hawatakuwa mababa au mama wazuri kwa watoto wao. Mwanao wa kiume atangoja umlishe yeye na mkewe na wajukuu. Sababu hutaki kumwambia au kumuelekeza unachelea atakasirika. Twazungumza lugha moja lakini hatuelewani. Kwanini? Tukimbilie wapi?

Mimi na wewe tutaendelea kulaumu tu na huenda tusipate jibu. Hizo zote hapo juu ni changamoto tulizozizalisha sisi wenyewe au ni babu/bibi zetu. Lakini kuna msemo ndani ya Qur’an tukufu kwamba, ‘’Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyo ndani ya watu, mpaka watu wabadilishe yaliyokuwemo katika nafsi zao’’. Hivyo basi kama Muumba wetu ameshatoa sharti hilo, basi wakati umewadia sisi tubadilike au tubadilishe yaliyo katika nyoyo zetu ili Muumba aweze kutubadilishia hali zetu.

Ndiposa, sisi wenyewe wahusika tutafute namna ya kujikwamua kutoka kwenye janga hili. Inabidi kwanza turudi kwenye maadili na tamaduni zetu za Kiafrika. Kila mmoja achukue na avae jukumu lake kama ilivykuwa hapo awali. Jukumu la kutafuta liwe la baba na jukumu la mama liwe la ulezi. Kazi ngumu afanye mwanamume na mwanamke afanye kazi zinazoendana na umbile lake. Mwanamke apewe haki zake zilizoainishwa na dini yake au sharia za nchi au hata tamaduni za kwao. Mwanamke arudi kwenye nafasi yake ya msingi nayo ni kujenga jamii kwa kuwapa malezi bora watoto wake na kutengeneza ‘’home’’, mahali ambapo kila mtu atapata utulivu anapokwenda pale. Kuna msemo tunaambiwa, ‘’Mama ni madrasa ya kwanza’’ na mwengine unasema ‘’Ukimfunza mwanamume umemfundisha yeye peke yake, lakini ukimfundisha mama umefundisha ummah mzima’’. Basi kutokana na hivi mwanamke anashikilia nafasi kubwa katika kujenga maadili katika jamii!

Pili, kila mtu ajue nafasi ya Mwenyezi Mungu katika nafsi yake. Yaani ifikie mahala kila mmoja wetu awe mcha Mungu ili dunia irudishe amani inayizidi kutoweka katika nyakati hizi. Ambapo unaweza kusoma au kusikia kwenye mitandao visa vilivyokithiri vya matumizi ya madawa ya kulevya, wizi, ubakaji, mauaji ya kila sampuli nay a kiholela holela, ukatili wa kijinsia, Imani za kishirikina, uporaji wa mali za binafsi na mali za ummah, na mengi mengineyo ya kusikitisha na kutamausha.

Tatu, serikali iongeze nguvu katika wizara ya masuala ya jinsia na jamii kwa kutoa maafisa ambao watazungukia jamii hadi mashinani kuwaelimisha kuhusu namna ya kuilea familia na kurejesha utu kwa wananchi na heshima ya familia kwa wanafamilia husika wote. Hiki kitengo kiwe imara kwa kuzingatia makuzi na malezi ya jamii ikiwemo elimu, lishe, afya na athari za kuitupa jamii na kuiwacha ikasambaratika.

Kwa kumalizia, wewe msomaji, chukua nafasi yako kama Mtanzania mwenye uzalendo, uwe chachu ya mabadiliko chanya katika jamii inayokuzunguka. Mabadiliko yanaanza kwangu mimi na wewe ili tuioneshe jamii kuwa yote yanawezekana tukifanya kama timu moja kwani kidole kimoja hakiui chawa. Wewe na mimi tunaweza tukazuia ufisadi, tunaweza kuzuia matumizi ya madawa ya kulevya, tunaweza kufundisha jamii au vijana juu ya mbinu za ujasiriamali, afya na kufanya vizuri katika masomo. Ni kuamua tu na kuchukua hatua katika sehemu au nafasi uliyo nayo katika jamii si lazima tuwe viongozi. Si lazima pesa, tufanye tunachokiweza kwa kutumia rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu ametugawia. Mwisho kabisa tusisahau kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko na kuzingatia masharti yaliyowekwa na mamlaka ili kudhibiti usambaaji wa maradhi haya ya Uviko 19!
 
Back
Top Bottom