Muswada wa Mabadiliko ya Katiba ni haramu kwa kupitishwa na idadi chini ya nusu kisheria

Muswada wa Mabadiliko ya Katiba ni haramu kwa kupitishwa na idadi chini ya nusu kisheria

Candid Scope

JF-Expert Member
Joined
Nov 8, 2010
Posts
11,897
Reaction score
6,925
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013 umezidi kuibua mapya, baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kudai kwamba, kikao cha Bunge kilichofanya maamuzi ya kuupitisha hakikuwa halali.

Kimedai akidi ya wabunge inayohitajika na kanuni za Bunge ya kufanya maamuzi haikutimia wakati wa kupitisha muswada huo.

Muswada huo uliozua tafrani kubwa bungeni, iliyohusisha baadhi ya wabunge, akiwamo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuondolewa na askari bungeni na wengine kurushiana ngumi na maofisa usalama, ulipitishwa ‘kiulaini’ na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ijumaa wiki iliyopita, huku wenzao wa upinzani wakisusia.

Madai hayo yalitolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, katika mahojiano maalum na NIPASHE jijini Dar es Saalam jana.

Mnyika alisema kanuni ya Bunge ya 77 (1) inataka kikao cha Bunge wakati wa kufanya maamuzi kiwe na wabunge wasiokuwa chini ya 175.

Lakini alidai wabunge waliokuwapo katika kikao kilichofanya maamuzi ya kupitisha muswada huo walikuwa 109.

Kanuni hiyo inasema: “Akidi kwa kila kikao cha Bunge wakati wa kufanya maamuzi itakuwa ni nusu ya Wabunge wote, kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 94 ya Katiba,isipokuwa kwamba, idadi hiyo haitahusu hoja kuhusu uamuzi wa kubadilisha masharti yoyote ya Katiba kwa mujibu wa Ibara ya 98 ya Katiba.”

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina wabunge 352, ambao nusu yake ni 176.

Alipotakiwa kueleza alivyofahamu idadi ya wabunge waliokuwapo katika kikao kilichopitisha muswada huo, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema atafanya hivyo iwapo atapelekwa mahakamani.

Alisema Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliijua idadi hiyo ya wabunge ndiyo maana alitumia fursa hiyo kujitetea japo kuwa utetezi wake haukuwa na msingi.

Mnyika alisema katika utetezi wake, Ndugai alisema akidi ilitimizwa na wabunge wa upinzani waliotoka bungeni kwa kuwa waliingia bungeni na kusaini mahudhurio, hivyo wanahesabika pia katika orodha ya wabunge waliokuwapo katika kikao kilichofanya maamuzi ya kupitisha muswada huo.

Hata hivyo, Mnyika alisema Sekretarieti ya Kamati Kuu (CC) ya Chadema chini ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, inakutana kuanzia leo kupitia na kujadili kwa kina mambo yote yaliyojiri bungeni, kutoa maamuzi na kutengeneza msingi wa mwelekeo wa baadaye.

Alisema mbali na hilo, Chadema pia itakutana na wadau wote wa katiba nchini, vikiwamo vyama vingine vya upinzani vyenye wabunge na visivyokuwa na wabunge na makundi mbalimbali ya kijamii ili kujenga sauti ya pamoja.

Alisema yote yaliyojiri bungeni, ikiwa ni pamoja na wabunge wa upinzani, akiwamo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuzuiwa kuzungumza, kutolewa nje na kupitishwa muswada huo kwa mabavu, ni njama zilizokuwa zimepangwa.

Mnyika alidai njama hizo zilipangwa na CCM kwa nia mbaya ya kuliteka Bunge Maalum la Katiba litakaloanza Novemba, mwaka huu, ili walitumie kuchakachua Rasimu ya Katiba. Alidai njama hizo zimepangwa na CCM baada ya jaribio lao la kuichakachua rasimu hiyo kupitia mabaraza ya katiba kushindwa na operesheni iliyofanywa na Chadema nchini kote.

Mnyika alidai njama hizo zilijadiliwa na kupitishwa pia katika kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika mjini Dodoma, wiki iliyopita.

Alidai kitendo cha yeye (Mnyika) na wabunge wengine, hasa wa Chadema kuzuiwa kuzungumza bungeni kilifanywa makusudi.

Mnyika alidai CCM walijua kuwa kama wabunge wa Chadema wangeruhusiwa kuzungumza bungeni, wangeweka hadharani mambo yote, ambayo walijadiliana na timu ya serikali kuhusu masuala yanayohusu katiba katika vikao viwili baina ya timu zao za majadiliano.

Alidai katika vikao vyote vya timu hizo, Chadema hawakukubaliana na mambo mengi ya msingi yaliyomo kwenye muswada uliopitishwa bungeni, ambao alidai ni mbaya kuliko kile kilichoandaliwa awali.Mnyika alisema baada ya yote yaliyojiri bungeni, walipokea mapendekezo tofauti kutoka kwa wadau juu ya hatua za kuchukua.

Alisema baadhi ya wadau wamependekeza kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya sheria ili kuzuia Rais Jakaya Kikwete asiusaini muswada huo ili kuanza kutumika kuwa sheria rasmi.

Mnyika alisema wadau wengine wamependekeza kutumia njia za kibunge kumshtaki Naibu Spika kwenye Kamati ya Bunge ya Kanuni kwa kukiuka kanuni za Bunge.

“Hata hivyo, kipaumbele chetu (Chadema) ni kurudi kwa wananchi. Tutajikita zaidi katika kutafakari namna tutakavyounganisha nguvu ya umma,” alisema Mnyika na kuwashauri wadau wengine kuendelea na mchakato wa kwenda mahakamani.

Wakati huo huo, Chama cha Wananchi (CUF), kimelaani vikali kitendo cha Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wabunge wa upinzani akiwemo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni Freeman Mbowe.

Vurugu hizo zilizuka bungeni wakati wa mjadala wa kupitisha Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 wiki iliyopita, baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kusimama na kuomba kuongea.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba.

Alisema kitendo cha Naibu Spika kumkataza Mbowe asiongee na kuamuru askari wamtoe bungeni kwa nguvu, hakikubaliki na kusema Serikali na kiti cha Spika wajitazame upya kwenye mchakato wa Katiba.

Profesa Lipumba alisema, ni kitendo cha aibu na hakikupaswa kufanywa na Naibu Spika wa Bunge.

“Sisi CUF tunajiuliza, angesimama Mizengo Pinda kuongea Naibu Spika angemnyima nafasi? na angethubutu kuamrisha askari wamtoe nje? Kwa nini haya yanatendwa na kiti cha Spika kwa vyama vya pinzani na hayatokei viongozi wa serikali,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza kuwa:

“Serikali ina mamlaka makubwa katika Bunge kuliko Bunge lenyewe, hadi kiti cha Spika kiendeshe masuala kwa taratibu za kupendelea serikali kwa kadri ambavyo Spika ataona,” alisema.

Alisema, muswada husika uliojadiliwa kwa dakika 90 ulikuwa na utata mkubwa, serikali imeubadili kwa nguvu na kuondoa maoni muhimu ya wadau, pia upande wa Zanzibar haukushirikishwa ipasavyo na wajumbe wa Kamati ya Sheria na Katiba ya Bunge.Alisema, akiwamo Tundu Lisu, wamesisitiza kuwa hawakupewa fursa ya kuchukua maoni kutoka kwa taasisi na watu muhimu waliopo Zanzibar.

Aliongeza kuwa, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF upande wa Zanzibar Hamad Masoud ambaye pia ni mjumbe wa baraza la Wawakilishi anathibitisha kuwa Zanzibar haikushirikishwa.
Imeandikwa na Muhibu Said, Mary Geodfrey na Enles Mbegalo
 
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba hautafika mbali hata kama wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walitumia uwingi wao bungeni kuupitisha na kwamba kuendelea kulazimisha suala hilo kunaweza kusababisha machafuko nchini.

Akizungumza katika mahojiano na kipindi cha NIPASHE, kinachorushwa na Redio One, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema wabunge wa CCM na viongozi wa serikali lazima watambue kuwa katiba ni jambo la maridhiano si jambo la kulazimishana.

"Wabunge wa CCM wanaweza kutunga sheria na muswada wanayotaka sababu wapo wengi lakini lazima waelewe kwamba kutumia wingi wao kulazimisha jambo muhimu kama la katiba ni kuweka machafuko ndani ya Taifa,"alisema.

Mbowe alisema mchakato wa katiba unahitaji hekima na busara sana lakini mambo yanayofanywa na CCM ni wazi kuwa muswada huo hautafika salama.

"Tunawataka na tunamuomba Rais na viongozi wengine wa CCM ambao pengine wana hekima kuliko hata wale waliopo ndani ya bunge watumie fursa hiyo kutafuta namna ya kufikia mwafaka katika masuala ya katiba,"alisema.

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema hivi sasa zipo taarifa kuwa wanaharakati ambao ni kundi lililopo nje ya wanasiasa wanajipanga kwenda mahakamani kupinga sheria ya marekebisho ya katiba iliyopitishwa wakati wa mkutano wa 12 wa bunge.

Alisema Naibu Spika Job Ndugai hakuweza kuheshimu nafasi yake (Mbowe) kama kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni kwa kukataa kumpa nafasi ya kuzungumza jambo ambalo ni kinyume cha kanuni
"Naibu Spika badala yake aliruhusu askari kuingia bungeni wakaanza kupiga wabunge, kutumia nguvu ,kutukanwa na mambo ya kudhalilishana, mnategemea hiyo amani ambayo ingeturudisha bungeni kuendeela na mjadala ingetoka wapi,"alisema Mbowe.

Mbowe alisema maamuzi ya kutaka muswada huo ujadiliwe bungeni yalikuwa yamekwisha pitishwa kwenye kikao cha wabunge wa CCM na kwamba hilo ndilo tatizo la kuwa na viongozi wanatoka chama kimoja cha siasa.

Kwa upande wake, Naibu Spika, Job Ndugai alisema wabunge wa kambi ya upinzani walishiriki mjadala wa majadiliano ya Muswada wa Marekebisho ya Katiba licha ya kuonekana wakitoka nje ya ukumbi wa ubunge kwasababu walijiandikisha kwenye kitabu cha mahudhurio na kupata posho ya siku hiyo.
 
Chama cha Wananchi (Cuf), kimesema kitendo cha Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kukataa kumpa nafasi Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na kuamuru askari wa Bunge wamtoe nje ya ukumbi huo ni kumhujumu Rais Kikwete kwenye azma yake ya kupata Katiba Mpya.

Pia, chama hicho kimesema kinafanya juhudi za kuwasiliana na viongozi wa vyama vingine ili kuweka mkakati wa pamoja wa kukabiliana na hujuma dhidi ya mchakato wa kupata Katiba Mpya na kuimarisha umoja wa kitaifa kwenye kipindi hiki cha kukabiliana na changamoto za nchi jirani.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema, Cuf inalaani vitendo vya kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wabunge wa upinzani akiwamo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kudai kuwa inaonyesha wazi CCM wanampango wa kutengeneza katiba ya upande mmoja.

"Kwa mfumo wa mabunge ya Jumuiya ya Madola, kwa Tanzania Waziri Mkuu na kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ndiyo wanawakilisha pande mbili ndani ya Bunge, hivyo kumnyima Mbowe fursa ya kuzungumza ni unyanyasaji na udhalilishaji na kwamba kitendo hicho hakikubaliki," alisema.

Profesa Lipumba alisisitiza muswada uliokuwa unajadiliwa ulikuwa na utata, Serikali imeubadili kwa nguvu na kuondoa maoni muhimu ya wadau.
 
kumbe hata CCM waliingia mitini,mbona hawakufikia idadi ya kupitisha muswada?
 
kumbe hata CCM waliingia mitini,mbona hawakufikia idadi ya kupitisha muswada?

Ninachoshangaa CCM wenyewe wanafanya kama hawajui kanunu za bunge inapobidi kupitisha mswada kama huo idadi gani ya wabunge inatakiwa ifikie idadi, vinginevyo ni mtego kwao, ipo siku watafikisha mahakamani sheria hiyo ikikubaliwa na raisi iwapo ni kwali idadi haikufikiwa bungeni.
 
Back
Top Bottom