dubu
JF-Expert Member
- Oct 18, 2011
- 3,502
- 3,483
Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi. Picha/JOSEPH KANYI
Na SAMMY WAWERU
Kwa Mukhtasari
Aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa bunge 11 Bw Justin Muturi amehifadhi kiti chake katika uchaguzi ambao umefanyika Alhamisi katika makao makuu ya wabunge jijini Nairobi.
ALIYEKUWA Spika wa Bunge la Kitaifa bunge 11 Bw Justin Muturi amehifadhi kiti chake katika uchaguzi ambao umefanyika Alhamisi katika makao makuu ya wabunge jijini Nairobi.
Bw Muturi aidha amechaguliwa kwa wingi na wabunge wa mrengo wa Jubilee ili kuhudumu katika kipindi cha miaka mitano ijayo katika bunge la 12.
Uchaguzi huo umefanyika saa chache baada ya jumla ya wabunge 348 waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita wa Agosti 8, 2017 na walioteuliwa kuwakilisha vyama vyao kuapishwa rasmi kuanza kuhudumia taifa.
Shughuli hiyo imetekelezwa licha ya muungano wa National Super Alliance (Nasa) kudai awali kuwa wabunge wake hawangeshiriki katika uchaguzi huo.
Mnamo Jumatano Nasa iliwapa idhini wabunge wake kuapishwa japo ikaonya kuwa hawatafanya biashara nyingine zaidi ya hiyo.
"Tumekubaliana kwa kauli moja kuwa wabunge wetu ambao ni zaidi ya 100 watahudhuria kikao cha kwanza bungeni," alisema Seneta wa Bungoma Moses Wetang'ula wakati akihutubia kikao cha waandishi wa habari Lavington, Nairobi kwa niaba ya muungano huo.
"Ajenda inayowalazimu kuhudhuria ni kuapishwa pekee wala hakuna biashara nyingine," akaongeza Bw Wetangula ambaye ni kinara mwenza Nasa na kiongozi wa chama chake cha Ford Kenya.
Uadilifu
Kwenye hotuba yake baada ya kuapishwa, Spika Muturi ameahidi kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.
"Nimenyenyekea na kuwashukuru kwa dhati kwa kunichagua. Nitahudumia taifa hili kwa bidii, uadilifu na heshima," akapongeza wabunge waliomchagua.
Akaongeza: "Tutafanya kazi kwa pamoja ili kukuza nchi yetu."
Aidha alipongeza wabunge wa jinsia ya kike waliochaguliwa akifichua kuwa bunge la 12 lina wabunge wengi ikilinganishwa na la 11.
"Bunge la 12 lina wabunge 76 wa kike waliochaguliwa ikilinganishwa na la 11 lililokuwa na wabunge 68 pekee wa kike. Hili linadhihirisha Kenya imekua kidemokrasi," akasema.