Leo, Oktoba 15, 2026, Kenya inaadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Amolo Odinga, mwanasiasa aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika historia ya siasa za Kenya na mapambano ya demokrasia nchini.
Raila alifariki Oktoba 15, 2025, akiwa na umri wa miaka 80 katika jimbo la Kerala nchini India, alikokuwa amesafiri kwa masuala ya afya. Kifo chake kilisababisha maombolezo makubwa nchini, huku maelfu ya Wakenya wakijitokeza kumuaga kiongozi waliyemfahamu kwa jina la Baba.
Soma pia Raila Amolo Odinga afariki dunia nchini India kwa mshtuko wa moyo
Mwaka mmoja baadaye, maelfu ya Wakenya wamekusanyika katika uwanja wa Migwena, Bondo, Kaunti ya Siaya, kuadhimisha maisha na mchango wake. Hafla hiyo imewaleta pamoja wanafamilia, viongozi wa kisiasa, viongozi wa kidini na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Maadhimisho hayo yameandaliwa kupitia shughuli za siku tatu zilizoanza Oktoba 13, zikihusisha mijadala ya vizazi tofauti mjini Kisumu, shughuli za kuwasha mishumaa katika eneo la Kang'o ka Jaramogi na mkutano mkuu wa kumbukumbu uliofanyika leo Bondo.
Katika maisha yake ya kisiasa, Raila alihusika katika mapambano ya mfumo wa vyama vingi, mageuzi ya kikatiba na harakati za kuimarisha demokrasia nchini. Alihudumu kama Mbunge wa Lang'ata, Waziri katika serikali mbalimbali na Waziri Mkuu kati ya mwaka 2008 na 2013.
Pia alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwa mstari wa mbele katika mchakato uliopelekea kupitishwa kwa Katiba ya Kenya ya mwaka 2010. Licha ya kuwania urais mara tano bila kushinda, Raila aliendelea kuwa mhusika mkuu katika siasa za kitaifa, akijenga ushawishi mkubwa ndani na nje ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM).
Hata hivyo, mwaka mmoja tangu kifo chake, chama cha ODM na washirika wake wa kisiasa wanaendelea kukabiliana na maswali kuhusu mustakabali wa uongozi wa chama hicho, mwelekeo wa ushirikiano wa kisiasa na namna urithi wa Raila utakavyoendelezwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Kwa familia yake, maadhimisho haya pia ni kumbukumbu ya kumpoteza baba, mume na mwanafamilia. Mkewe, Ida Odinga, ameeleza jinsi maisha yalivyobadilika tangu kifo cha mumewe, akikiri kuwa wakati mwingine bado ni vigumu kuamini kwamba hayupo tena.
Ingawa Raila hayupo tena katika ulingo wa siasa, jina lake linaendelea kutajwa katika mijadala kuhusu demokrasia, haki za wananchi, ugatuzi na mustakabali wa siasa za Kenya.
Mwaka mmoja baada ya kifo chake, je, ni mchango gani mkubwa zaidi wa Raila Odinga unaopaswa kukumbukwa katika historia ya Kenya? Na je, viongozi wa sasa wanaendeleza misingi aliyokuwa akiitetea?