Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
MWAKA MPYA 2020 NA KITABU KIPYA
‘’THE SCHOOL TRIP TO ZANZIBAR’’
Na Mohamed Said
Tunauanza mwaka mpya kwa kuingiza kitabu kipya nchini katika orodha ya vitabu vilivyoandikwa na Watanzania.‘’THE SCHOOL TRIP TO ZANZIBAR’’
Na Mohamed Said
Tegemeo la mwandishi ni kuwa kitabu hiki kitaingizwa katika shule zetu, maktaba na maduka ya vitabu nchini kuchochea usomaji wa vitabu kwa vijana wadogo kwa nia ya kuongeza elimu ili kusaidia kuelewa historia na utamaduni wa nchi yao.
Kitabu kinaanza kwa kupitia shule na wanafunzi wake wakiongozwa na mwalimu wao kundi la wanafunzi wanafunzwa kwa vitendo kwa kutembezwa hatua kwa hatua ndani ya historia ya Tanzania wakianza safari yao Dar es Salaam kuelekea Zanzibar wakikata Bahari ya Hindi ndani ya chombo.
Katika safari hii wanafunzi wanatambuka mpaka wa nchi moja kuingia nyingine na kwa kitendo hiki wanatambua nini maana ya kuunganisha nchi mbili katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Lakini ni wazi kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar usingeliwezekana kufanyika bila ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964.
Hapa ndipo wanafunzi wanapofanywa kutambua historia ya Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika, Sultan wa Zanzibar na baada ya mapinduzi, Rais Abeid Amani Karume na athari zake.
Fikra za wanafunzi zinaelekezwa kuangalia alama za utawala kupitia katika makazi ya viongozi wa Tanganyika na Zanzibar katika miaka mingi ya nyuma wakati nchi mbili hizi ziko chini ya utawala wa Waingereza.
Ujenzi na kuwapo kwa wa nyumba hizi mbili hadi sasa ni historia tosha.
Katika safari yao kuelekea Zanzibar wakitokea Kigamboni wanafunzi wanaiona Ikulu, Dar es Salaam, makazi ya Gavana wa Tanganyika wakati wa ukoloni na baada ya uhuru makazi ya marais wa Tanganyika kisha Tanzania baada ya muungano.
Wakiingia Zanzibar bado wakiwa baharini na ndani ya chombo, wanafunzi wanaishuhudia kwa macho yao wenyewe, Beit el Ajaib jengo lenye historia kubwa.
Leo Beit el Ajaib imebakia kuwa kumbukumbu ya historia ya Zanzibar.
Nyumba hii imebeba historia kubwa inayostahili kusomeshwa kwa makini na kuhifadhiwa.
Safari hii ya wanafunzi ni ufunguo uliowafungulia mengi katika Zanzibar na utamaduni wake ambayo laiti si kama kusafiri na kufika visiwani, hayo yote kuanzia vyakula mashuhuri vya Zanzibar, mavazi na mengi mengineyo yangebakia maelezo yaliyo mbali sana na fikra zao.
Kuisikia kaimati na mkate wa ufuta na kuula ni vitu viwili tofauti.
Halikadhalika kuwaona watu wengi waliovaa kanzu kofia na makubadhi sokoni na barabarani ni tofauti na kuona mavazi hayo yakiwa yamevaliwa na mtu mmoja mmoja Dar es Salaam.
Hakika kuona ni kuamini na kuona ni dhahiri kuliko kusoma peke yake bila ya jicho kushuhudia.
Kitabu hiki kina mengi ya kuwasomesha wanafunzi ili kuwawezesha kuelewa historia ya Tanzania na jinsi utamaduni wa nchi mbili hizi unapolingana na kwengine kupishana.
Kuna mengi ya manufaa kwa kitabu hiki kusomeshwa na kusomwa kwa makusudio ya kuhifadhi historia ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.