Hebu chungulieni makala hii labda kuna concept ya alichouliza mtoa mada japo kwa kunusanusa!
Na Joseph Mihangwa
HATIMAYE wimbi la migomo katika Vyuo vya elimu ya juu nchini limetulia. Chanzo ni kusimamishwa masomo kwa wanafunzi wengi, waliopinga sharti la kuwataka kulipia asilimia 40 ya gharama za masomo, wakidai kuwa walikuwa wakiadhibiwa hivyo kwa sababu tu wao walikuwa watoto wa wazazi masikini.
Wanafunzi hao hawakuona mantiki kwa Serikali kuwasimamisha masomo kwa kosa tu la kuzaliwa katika familia masikini, wakati Serikali imeshindwa kudhibiti matumizi yake makubwa na yasiyo ya lazima; ufisadi uliokithiri, ubinafsishaji na uwekezaji usiojali, huku mikataba mibovu na uporaji wa rasilimali za taifa ukiendelea kulitafuna Taifa. Migomo hii iliashiria migongano ya kitabaka inayoanza kuibuka katika jamii yetu.
Kama ilivyokuwa mgomo wa Oktoba, 1966, ambapo asilimia 90 ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam walifukuzwa kwa kupinga mpango wa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, na Agizo la kukatwa kwa lazima asilimia 60 ya mishahara ya wahitimu na hatimaye wote wakarejeshwa bila masharti, migomo ya sasa inabeba maudhui yale yale na yametafsiriwa na jamii ya wasomi kama "ushindi" kwa kuifanya Serikali itambue jinsi tabaka la walio nacho linavyoweza kushindwa kupora demokrasia na haki za msingi za wanyonge, zikiwamo haki ya elimu kwa wote, kwa mfumo wa sera kandamizi na za kitabaka, kama umma utaungana.
Tofauti na mgomo wa 1966, ambapo baadhi ya Wabunge wenye msimamo makini waliwaunga mkono wanafunzi, katika migomo ya Zanzibari, hakuna Mbunge aliyetoa sauti, isipokuwa Viongozi wachache tu wa vyama vya upinzani wenye jadi ya kupigia kelele karibu kila jambo, walitoa malalamiko yao.
Hata hivyo, Wabunge waliounga mkono mgomo wa 1966 walifukuzwa ubunge na uanachama wa Chama pekee cha Tanganyika African National Union [TANU], licha ya Serikali kutambua mahali ilipoteleza kwa kuwafukuza wanafunzi hao.
Hatua hiyo kali ya Serikali dhidi ya wasomi [1966] iliitwa na mwanazuoni mahiri barani Afrika, Professa Ali Mazrui, akiandikia Jarida "Transition" mwaka 1967, kuwa ni ugonjwa wa Kitanzania [Tanzaphylia] wa kuchukia wasomi, na kwamba Rais Julius Nyerere alikuwa msomi mla nyama ya wasomi [Intellectual cannibal].
Akijibu tuhuma hizo dhidi yake, kwa hotuba aliyoitoa Chuo Kikuu cha Liberia, Februari 1968, juu ya "Msomi anahitaji Jamii", Mwalimu alidakiza kuwa, wasomi wanakuwapo kwa ajili ya Jamii na siyo kinyume chake.
Alisema, wajibu mkubwa wa Msomi katika jamii ni kukidhi mahitaji ya jamii yake ambayo inaundwa pia na wasio na elimu. Msomi anapaswa kumulika njia; ni mshika kurunzi.
Tatizo la mtazamo huu ni kuhusu jinsi msomi huyu anavyoshirikishwa katika kubainisha mahitaji ya jamii yake. Swali linalozuka hapa ni; Nani anayepanga mahitaji ya jamii? Ni watu?. Ni Viongozi?. Viongozi wa aina gani?.
Tunapodai kwamba jamii yetu inatakiwa kujitosheleza kwa wataalamu ili tuweze kuendelea, ni nani anayeweka mfumo wa elimu na masharti ya utoaji elimu hiyo?. Nani anayeweka sera za uchumi?. Kwa manufaa ya nani?.
Je, ni mahitaji ya jamii kujenga matabaka ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, kama inavyotokea sasa?. Je, ni mahitaji ya jamii kwamba wenye nguvu ya pesa ndio washike hatamu za uchumi wa nchi, utawala na siasa?.
Uzoefu umeonyesha kwamba ni Viongozi [wanasiasa] wanaopanga mahitaji ya jamii kupitia bunge lililodhibitiwa na watawala. Tazama jinsi wabunge wasomi wanavyoasi maadili ya taaluma zao kwa kujifanya popo wanapoingia bungeni kwa kuridhia hoja na sera wanazofahamu fika ni za kuangamiza jamii, wakitetea pepo ya tabaka la watawala!
Alvin Toffler, katika kitabu chake "Powershift", anatoa changamoto kwa wasomi kwamba, "kwa kuwa elimu [usomi] ndiyo kisima pekee cha demokrasia na madaraka, basi, wasomi wana wajibu wa kutetea na kulinda uhuru wa mawazo, kukosoa na kufundisha pamoja na kupinga kwa nguvu zote urasimu na ukandamizaji. Wanatakiwa kuepuka utii pofu, kujikomba na nidhamu ya woga".
Naye Profesa Arthur M. Schelesinger Jr, anatukumbusha katika kitabu chake: The Cycles of American History, kwamba, demokrasia haijiendeshi pekee; na kwamba jukumu la kujenga, kulinda na kuimarisha demokrasia na utawala bora haliwezi kuwa la Serikali pekee, vyama vya siasa na "vigogo" wachache wenye nguvu za kiuchumi au kisiasa; bali jamii nzima inapaswa kuwa wakala wa demokrasia na udemokrasishaji. Na kwa sababu hiyo, wasomi wana wajibu mkubwa katika hilo kwa kuwa wao wanazo zana [elimu] na nyenzo za uchambuzi wa jamii na mahitaji yake.
Na katika kufanya hivyo lazima watakumbana na vikwazo vya wasiotaka mabadiliko, na vya wenye kulinda na kutetea maslahi binafsi kwa maangamizi ya jamii. Wafanye nini?.
Msomi hapaswi kuogopa kutetea maslahi ya walio wengi, lazima akubali kuwa mhanga wa mfumo. Socrates [Greece] alikuwa mmoja wa wahanga wa kwanza wa mifumo kandamizi katika kutetea misingi ya demokrasia [L. Housman: The Death of Socrates]. Na karibu na zama zetu, tunakumbushwa na Abraham Lincoln, [1863] kwamba: "Taifa hili, chini ya Mungu, litazaa uhuru mpya; na kwamba Serikali ya watu, iliyo mikononi mwa watu, na kwa ajili ya watu, haitaangamia juu ya nchi".
Ni wajibu wa wasomi kuona kuwa Serikali kama hiyo inazaliwa na kudumu. Lakini nani kama Socrates, miongoni mwa wasomi wetu?.
Katika jukumu hilo, kuna wakati [miaka ya 1967 – 1977] Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam [UDSM] kilijipatia jina na sifa ya kuwa kitovu cha mawazo na fikra za kimapinduzi, uwanja wa harakati na changamoto za kimapinduzi na kimaendeleo, kiasi cha kuonewa wivu na Vyuo Vikuu vingine ndani na nje ya bara la Afrika.
Sifa hizi zilianza kutoweka baada ya 1977 pale wanasiasa [wasio na hoja] walipogeuka "wala nyama ya watu wasomi" [intellectual cannibals], kwa kuwaona eti ni wabishi na kidhibiti mwendo kwa maendeleo ya nchi, ambapo ukweli ni kinyume chake.
Kwa mtazamo wa wanasiasa, maendeleo na umoja wa kitaifa ni kipaumbele kabla ya demokrasia. Matokeo yake yalikuwa ni kuporomoka kwa uchumi kwa kiwango sawa na cha kulewa madaraka kwa watawala.
Hii ilitokana na mfumo wa chama kimoja uliozuia uhuru binafsi wa mawazo juu ya mchakato wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hakutokea "Socrates" msomi wa kuiokoa hali mpaka tumekutwa na sera kandamizi za utandawazi kwa maangamizi yetu.