Mwanafunzi wa kidato cha tano, katika Shule ya Wavulana ya Umbwe, iliyopo Kata ya Umbwe Onana, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Thomas Edward Kogal (19) amefariki dunia wakati akifanya mazoezi shuleni hapo.Mwanafunzi huyo ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma, anadaiwa kufariki dunia juzi jioni, Agosti 12, 2024.
Mkuu wa shule hiyo, Elirehema Mungaya akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Agosti 13, 2024, amethibitisha kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo huku akisema alikuwa uwanjani akifanya mazoezi na wenzake.
Soma Pia:
"Ni kweli mwanafunzi wetu amefariki jana (juzi) jioni wakati akiwa uwanjani na wenzake wakifanya mazoezi, lakini alikuwa na tatizo la moyo," amesema mkuu huyo wa shule.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Agosti 14, 2024, amekiri kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo huku akisema taarifa zaidi atazitoa baadaye.