SoC04 Mwanahabari: Msemaji aliyekosa wa kumsemea

Tanzania Tuitakayo competition threads

Marta journalist

New Member
Joined
Jul 18, 2022
Posts
2
Reaction score
1

Picha mtandao

Taaluma ya uandishi wa Habari, ni miongoni mwa taaluma inayozalisha wahitimu wengi katika vyuo mbalimbali hapa nchini Tanzania kila mwaka. Wahitimu hao wanakwenda kufanya kazi kwenye vyombo vya habari kama redio, televisheni, magazeti na vyombo vya habari vya mitandaoni.

Kazi kubwa ya wanahabari ni kuhabarisha umma, kusaidia wananchi kupaza sauti zao ili kutatua changamoto na kuchochea uwajibikaji na maendeleo endelevu katika jamii.

Mwanahabari amekuwa msemaji anayewasemea wanajamii na kuwakutanisha na mamlaka ili kutatua changamoto zao. Licha ya kutumiwa na jamii kama daraja lakini ni wazi ameshindwa kujisemea na kutatua changamoto zake zinazomkosesha amani na ari ya kufanya kazi.

Sheria ya ajira na uhusiano kazini ya mwaka 2004 kifungu cha 14 kuhusu mikataba na wafanyakazi na kifungu cha 15 vinaelezea aina za mikataba na kwamba mwajiri anatakiwa atoe mkataba wa maandishi kwa wafanyakazi wake.

Lakini suala hilo limekuwa ni ndoto kwa wanahabari wengi nchini Tanzania kwani waajiri katika baadhi ya vyombo vya habari hawatekelezi matakwa ya sheria hiyo hali inayochangia wanahabari wengi kufanya kazi bila mikataba na kutokuwa na uhakika wa malipo na stahiki zao.

Ripoti ya kamati iliyoundwa Januari 24, 2023 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Azam Media Tido Mhando kutafiti hali ya utendaji na uchumi kwenye vyombo vya habari Tanzania Bara inaeleza, asilimia 56 ya wandishi wa habari wanafanya kazi bila mikataba kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi miaka sita.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa Juni 18, 2024 ilibainisha pia kwamba asilimia 38 ya mikataba wanayopewa waandishi wa habari haigusi bima za afya na wengine wakilipwa shilingi elfu mbili (2000) kwa kila habari wanayochapisha.

Lakini pia utafiti uliofanywa na Twaweza kwa kushirikiana na Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC) iliyotolewa mwezi February 2024 inaeleza asilimia themanini (80%) ya waandishi wa habari hawana mikataba.

Ili kuelezea ukubwa wa tatizo hili bwana Ernest Sungura mwenyekiti wa umoja wa haki ya kupata taarifa CoRI akizungumza katika kongamano la maendeleo ya sekta ya habari alisema “fanya makisio ya chombo kimoja cha habari kinaajiri waandishi wa habari na wafanyakazi ishirini tu ni sawa na kusema katika idadi ya vyombo vya habari vilivyosajiliwa tuna waandishi wa habari na wafanyakazi elfu 20, lakini katika hao elfu ishirini watakuwa ni wafanyakazi na waandishi wa habari elfu nne tu wenye mikataba, hawa wengine elfu kumi na sita hawana mikataba ya ajira.”

Suala hili limekuwa ni mwiba kwa wanahabari hali inayochangia kuishi maisha ya kutegemea posho za mashirika au watu wanaotaka habari zao zitolewe kwa umma. Hii inachangia kupungua kwa uadilifu wa wanahabari kwasababu inamlazimu kutoa taarifa fulani kwa mlengo anaotaka mwenye habari na sio kwa kufuata maadili na miongozo ya taaluma ya habari.

Mwandishi huyu wa habari anayetumiwa na serikali, wanasiasa, wafanyabiashara na wananchi, amejifunga mikono na mdomo bila kusema yanayomkabili. Hajui atakapostaafu kazi ataishije kwani kufanya kazi bila mkataba kunafanya asiwe na akiba kwenye mifuko ya hifadhi wa jamii itakayomsaidia baada ya kustaafu.

Wakati wa kusoma bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya mwaka 2024-2025 bungeni, mbunge wa viti maalum Easter Bulaya katika kutoa mchango wake alisema “Asimilia 80 ya wanahabari hawana mikataba,l akini hawawezi kukaa nyumbani.. wanafamilia hili tunaomba lifanyiwe kazi, hata hao wenye mikataba hawalipwi, leo hii sijui waandishi wa habari kikokotoo kitawakokotoa zaidi maana hata michango yao haipelekwi”.

Ukosefu wa ajira ni miongoni mwa kisababishi kikubwa cha wanahabari kufanya kazi katika mazingira magumu bila mikataba wakihofia iwapo watatoka kwenye eneo hilo ni ngumu kupata eneo lingine la kufanya kazi. Changamoto hiyo isiwe kigezo cha waajiri kuajiri wanahabari bila kuzingatia sheria ya kazi na uhusiano kazini.
Nini kifanyike?

Waajiri wanatakiwa kuiona taaluma ya habari kama taaluma nyingine na kwamba inaumuhimu wake katika jamii na hivyo wanapoajiri wazingatie sheria ya kazi na uhusiano kazini inayohimiza kutoa mikataba kwa wafanyakazi na kuizingatia kama ilivyo kwenye sekta nyingine.

Waandishi wa habari kupitia vyama vyao na wadau wa habari wawe na nguvu ya kulisemea suala la mikataba kwa waandishi wa habari na kulisimamia ili kutetea maslahi yao.

Wamiliki wa vyombo vya habari wawekeze katika teknolojia mpya na kuboresha ubora wa huduma za dijitali hasa vyombo habari vya zamani lazima vifanye mapinduzi kwa kuajiri vijana wanaoendana na kasi ya teknolojia ili kuhakikisha wanazalisha maudhui yenye ubora na yanayoendana na mahitaji ya jamii kwa kufanya hivyo watavutia matangazo na ufadhili kutoka kwa mashirika mbalimbali.

Ni wakati sasa wasimamizi wa vyombo vya habari kuwa na ujuzi wa biashara ili kuweza kuviendesha vyombo vya habari kibiashara, kwa kufanya hivyo wataweza kuwa na mifumo ya kibiashara, kutafuta masoko na kufanya miradi itakayowaingizia pesa za kujiendesha.

Ili kukidhi matakwa ya sheria hiyo, Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) wakati wa utoaji wa leseni kwa vyombo vya habari vipya inatakiwa kuhakikisha mmiliki anakuwa na uwezo wa kukiendesha chombo husika kwa miaka ya awali isiyopungua mitatu bila kutegemea mapato yake.

Serikali pia ilipe madeni inayodaiwa na vyombo mbalimbali vya habari ili viwe na uwezo wa kutimiza matakwa ya kisheria, mikataba na taratibu za kuwalipa wafanyakazi wake.

Ni wazi kwamba haya yakifanyika yatawawezesha waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadali ya uandishi wa habari, ubunifu na kuongeza mchango wao katika jamii pia kukuza tasnia ya habari kwa ujumla. Na hii ndiyo Tanzania tuitakayo.
 
Upvote 6
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…