KARIBU MWANAHALISI ILA EPUKANA NA UDAKU
Nimefurahi kuliona MwanaHalisi mitaani. Ni ahueni kubwa kwa wapenda demokrasia ya kweli na uhuru wa vyombo vya habari. Hata sisi waandishi wa habari, tunaponea MwanaHalisi pale ambapo stori zetu zinakwama kwenye vyombo vyetu vinavyomilikiwa na mafisadi.
Nawapongeza MwanaHalisi, lakini wakati huohuo nampa tahadhari kaka yangu Kubenea kuwa anabeba dhamana kubwa, hivyo atumie zaidi waandishi waadilifu, shupavu, jasiri na waliosomea taaluma kama akina Ndimara Tegambwage na Ansbert Ngurumo. Akianza kuokoteza articles kutoka kwa makanjanja na watunga habari wa vijiweni, basi heshima ya MwanaHalisi itapotea haraka sana katika jamii.
Mfano halisi ni makala ya "Wazo Mbadala" ukurasa wa 4 wa toleo "mwali" la MwanaHalisi. Unapochapisha makala ya kumtuhumu kiongozi mwenye mvuto kwa wapiga kura wake, kama Dk. Mwakyembe, kwa kutumia vyanzo visivyo vya uhakika, ni rahisi kuwavunja moyo wapenda uwazi na ukweli wanaolipenda gazeti hili.
Mimi na waandishi wa habari wenzangu watatu wa Majira, Mwananchi na Uhuru tulikuwepo "uwanja wa siasa" mjini Kyela kumsikiliza Dk. Mwakyembe. Yaliyonukuliwa kwenye makala hayo, hakuyasema Dk. Mwakyembe. Aidha hata nukuu kutoka kwenye gazeti la Mwananchi toleo la tarehe 14 Januari, 2009, imeongezwa maneno kwa sababu ambazo huyo "mwandishi mwanafunzi wa SAUT" anazijua. Wananchi wengi wa mjini Kyela ambao ni wapenzi wa MwanaHalisi, kama mwanaharakati Mzee Benson Mwaikeke, wameshtushwa na kuanza kujiuliza kama MwanaHalisi nalo limeanza kutumiwa na mafisadi.
Wilayani Kyela, taarifa za Mbunge wao kuhujumiwa na mafisadi zimeenea sana kutokana na fedha nyingi kutumika kwenye uchaguzi wa viongozi wa jumuiya za CCM ili kuwaengua wale wote walioonekana kumuunga mkono Dk. Mwakyembe. Fedha za kampeni, kwa mujibu wa Diwani wa Kyela Mjini, Viski Mahenge, ambaye alipata kura nyingi kuwa Mwenyekiti wa Wazazi wa Wilaya, zilitoka kwa Karamagi na Lowassa kupitia kwa mfanyabiashara mmoja wa malori aishie Dar es Salaam kwa jina Elias Mwanjala.
Hivyo basi, si vibaya kukumbushana kuwa MwanaHalisi lina jina katika jamii. Jina hilo tulilee kwa uandishi mzuri na wa makini.