Tanzania inayokimbia hoja Gambia
Ndimara Tegambwage
SITAKI kuamini kwamba Tanzania imesusia mkutano wa 46 wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) ya Haki za Binadamu unaoendelea mjini Banjul, Gambia – Afrika Magharibi.
Hakuna kibao kinachoonyesha ujumbe wa Tanzania unakaa wapi. Hadi jana, jina la mjumbe kwenye mkutano huu lilikuwa halijaonekana kwenye orodha ya wajumbe kutoka nchi za Afrika. Tanzania iko wapi?
Huu ni mkutano mkubwa unaoleta wajumbe kutoka nchi wanachama wa AU. Hoja kuu ni Haki za Binadamu. Kila nchi ina wawakilishi wa serikali. Vilevile kuna wawakilishi kutoka asasi mbalimbali za kijamii zinazojihusisha na haki za binadamu.
Tanzania iko wapi? Kikao cha Alhamisi kilikuwa na hoja zinazohusu Tanzania. Hoja kuu na ambayo haijapatiwa ufumbuzi ni ile ya wafugaji wa Loliondo na sehemu nyingine nchini. Mara hii aliyeanza kuchokonoa hakuwa Mtanzania. Alikuwa Marianne Wiben Jensen wa Copenhagen, Denmark.
Marianne ni Mratibu wa Mipango wa kundi la kimataifa linalohusu masuala ya jamii za asili (indigenous people) kwa kanda ya Afrika (IWGIA) alivyosema Marianne:
"Hali ya wafugaji wanaohamahama inaendelea kuwa ngumu zaidi katika nchi za Afrika ikiwamo Tanzania ambako wafugaji wametupwa nje ya ardhi walikokuwa wakiishi miaka nendarudi." Baada ya hapo aliorodhesha kinachowasibu wafugaji.
Alisema kitendo cha kuchoma makazi ya Wamasai katika vijiji vinane vya Loliondo; mali zao kuunguzwa na mifugo yao kusambaa na mingine kupotea kabisa, ni cha kuvunja haki za binadamu. Aliorodhesha yafuatayo na kutaka yajibiwe na serikali.
Kwamba zaidi ya makazi 200 ya Wamasai yalichomwa moto; maghala ya chakula chao yaliunguzwa; kwamba zaidi ya watu 3,000 hawana mahali pa kuishi kutokana na ukatili huu na mashamba ya mahindi ambayo yalikuwa na mazao yaliyokomaa yaliunguzwa moto. Mtu wa serikali hayupo. Nani atajibu?
Hayo yametendeka wakati ukame mkali umesababisha njaa kubwa, mito midogo kukauka; madimbwi kuwa mashimo tu yasiyokuwa na tone la maji na kufanya mifugo kukosa malisho na maji; hivyo kufa kwa wingi.
Mratibu wa IWGIA anasema mali ya thamani ya mamilioni ya shilingi imeharibiwa katika zoezi lililohusisha askari wa FFU na walinzi wa kampuni ya Ortello Business Corporation iliyopewa na serikali eneo la Loliondo kwa ajili ya kufanyia uwindaji.
Kwamba askari wa FFU walifanya ukatili kwa wafugaji; kwamba katika zoezi hilo , wanawake walibakwa na wengine waliofukuzwa makazini mwao walitoa mimba wakiwa wanakimbia moto wa risasi za polisi. Mtu wa serikali hayupo. Nani atajibu tuhuma hizi?
Marianne haishii hapo. Anasema familia zimevunjwa na mafundo yake kuteketea kwani baadhi ya watoto wamepotea kutokana na woga wakiwa wanakimbia milio na moto wa risasi. Kwamba matambikio ya Wamasai yalichomwa pia na baadhi yao wamekamatwa na polisi na kutungiwa mashitaka ya kubuni.
Mwanaharakati huyo anasema serikali haijachukua hatua yoyote kusaidia waliokumbwa na maafa hayo; badala yake imewaacha wajihangaikie katikati ya ukame, njaa, ukosefu wa makazi na ukosefu wa malisho kwa ng'ombe waliosalia nao. Hakuna msemaji wa serikali. Nani atajibu haya?
"Tunataka kukumbusha kwamba serikali ya Tanzania, Septemba 2007, iliunga mkono Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya haki za watu wa asili…na Tanzania imetia saini mikataba kadhaa ya kimataifa inayolinda haki za binadamu," ameeleza Marianne.
Lakini anasema tendo la serikali kuhamisha wafugaji wa Loliondo, kwa mabavu na a kuharibu makazi yao na chakula chao, ni kukiuka sheria na mikataba ya kimataifa. Hakuna msemaji wa serikali. Nani atajibu?
Inawezekana mjumbe hajatoka Dar es Salaam au yuko katika moja ya hoteli za mjini hapa akisubiri siku ziishe. Lakini kwa vyovyote vile, haya ni madai makubwa ambayo yanastahili kujibiwa na serikali.
Juzi Alhamisi, wakati wasilisho hilo likifanywa, watu wengi walikuwa wakitupa macho huku na kule kutafuta kuona msemaji wa serikali ya Tanzania. Kwa kuwa hoja hiyo itaendelea kujitokeza leo na kesho, bado shauku ya kuona msemaji wa Tanzania ingalipo.
Agosti mwaka huu, Tume ya Haki za Binadamu ya AU ilimwandikia Rais Jakaya Kikwete ikimwomba maelezo juu ya hali ya Loliondo – wafugaji kutishiwa, kufukuzwa kwenye makazi yao, kuchomewa nyumba, mazao na mifugo.
Kwa mujibu wa ofisa wa tume hiyo, serikali ya Tanzania haijatoa maelezo yoyote. Haijulikani itatoa lini maelezo hayo. Haijafahamika ni hatua gani zitachukuliwa iwapo haitatoa majibu. Aidha, wafugaji wawili wa Loliondo wako mjini hapa na kwa mujibu wa ofisa wa tume, watakutana na Mwenyekiti wa Tume hii ya AU kesho, Jumatatu.
Yuko wapi mjumbe wa Serikali ya Tanzania kumaliza kiu ya Watanzania walioko hapa pamoja na wajumbe kutoka Afrika nzima ambao wamesikia tuhuma hizi? Labda atafika kesho. Sitaki ashindwe kufika.
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=10350