Mwanangu Mwanasiti Kijino Kama Chikichi

Mwanangu Mwanasiti Kijino Kama Chikichi

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
MWANANGU MWANASITI KIJINO KAMA CHIKICHI...

Laiti kama kuta zingekuwa na masikio.

Picha hiyo ya kwanza hapo ni Muthaiga Country Club, Nairobi mwaka wa 1989 niko na Ally Sykes (1926 - 2013).

Picha ya pili niko na Bilal Rehani Waikela (1932 - 2022) Magomeni Mapipa mwaka wa 2019.

Wote wawili wamepigania uhuru wa Tanganyika na Allah alinijaalia nikawa karibu na wao sana na wao bila khiyana wala bila hofu yoyote wakanieleza kila walichokijua kuhusu historia ya TANU na harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.

Wazalendo hawa wakanipitisha katika barabara ambayo wachache sana wamebahatika kupita na wakanifikisha katika nchi wachache wamepata kutia mguu.

Kila nilipokuwanao kwa miaka yote mimi nilikuwa nasoma na kujifunza.

Wazalendo hawa hawakuogopa kuzungumza na kinasa sauti changu wala hawakuogopa kalamu yangu ilipokuwa inaruka kutoka ukurasa mmoja kwenda mwengine wa note-book yangu wala hawakusita kujibu maswali niliyowauliza.

Wala hawakuliogopa jicho la camera yangu.

Wala hawakupata kunong'ona kwa ajili ya hofu wakati wananihadithia historia ya TANU.

Miaka hiyo ninayoiziungumza hapa watu wakiogopa kutaja majina ya wazalendo wengine waliokuwa ndani ya TANU na wakipambana na Muingereza bega kwa bega na Julius Nyerere.

Ulikuwa mwiko mkubwa kumtaja Sheikh Suleiman Takadir au Mufti Sheikh Hassan bin Ameir kama wapigania uhuru.

Ulikuwa mwiko kueleza mchango wa Abdul Sykes na yote yaliyokuwa yakitendeka Soko la Kariakoo ambako Abdul Sykes alikuwa Market Master.

Soko la Kariakoo ilikuwa moja ya kituo cha harakati na wasukuma mambo hapo sokoni ukimtoa Abdul Sykes alikuwa Shariff Abdallah Atttas na Mshume Kiyate.

Haya yalikuwa majina yaliyokuwa watu wakiogopa kuyataja hadharani na kuyaunganisha na Mwalimu Nyerere, chama cha TANU na harakati za kupigania uhuru.

Miaka mingi imepita na hawa baba zangu, wazee wangu wametangulia mbele ya haki.

Lakini linalonielemea katika fikra zangu kila ninapowakumbuka ni yale mapenzi waliyokuwanayo kwangu.

Hujiuliza historia ya Mwalimu Nyerere, TANU na uhuru wa Tanganyika ingekuwaje kama wazalendo hawa wangekaa kimya wasinieleze historia hii?

Nimebeba deni kubwa sana kwao ambao mimi siwezi kulilipa wala sina uwezo huo.

Bwana Ally alipoanza kuumwa mimi niko Tanga na nilipokuja Dar es Salaam nilikwenda kumjulia hali ofisini kwake, Mtaa wa Makunganya.

Nilishtuka sana na nikaingiwa na simanzi kubwa.
Alikuwa amekonda lile tambo lake nililolizoea lilikuwa halipo tena.

Hali kadhalika sauti yake ilikuwa imefifia.

Lakini Ally Sykes akipenda kufanya kazi na hakutaka kukaa nyumbani ingawa kwa kweli hakuwa anahitaji kufanyakazi kupata riziki yake.

Alichokifanya ni kupunguza muda tu wa kukaa ofisini.
Alikuwa kwa miaka mingi ameacha kuendesha gari.

Siku moja nimetoka Tanga nikaenda kumjulia hali ofisini kwake.
Nilifurahi kwani nilimkuta kachangamka na akanipokea kwa bashasha.

Mkononi alikuwa kashika sigara anavuta.
''Baba unavuta sigara ilhali daktari kakwambia uache kuvuta...'''

Nikaingiza mkono wangu mfukoni nikatoa simu yangu.
''Mimi nampigia Alma namweleza.''

Alma ni binti yake na ni daktari.

Mimi nilikuwa natishia tu lakini yeye kuona simu yangu iko mkononi akajua nampiga kweli Alma.

''Kwa hisani yako bwana usimpigie basi hii naizima.''
''Nampigia aje hapa aone ukaidi unaotufanyia.''

Akatoa mkasi akaikata ule upande ulio na moto akaiweka sigara kwenye ''ash tray.''

Bilali Waikela sote tulifurahi serikali ilipochukua dhima ya matibabu yake na wakamleta kutoka Tabora hadi Muhimbili.

Miaka mitatu iliyopita alikuja nyumbani kwangu asubuhi sana.
Nilifurahi kumuona na tukazungumza kama ilivyo kawaida yetu.

Lakini ilinidhihirikia kuwa Mzee Waikela amechoka sana na nilimsindikiza hadi Msikiti wa Kichangani anapofikia kila akija Dar es Salaam.

Nikaja kumuona baada ya miaka mitatu hospitali.
Ilikuwa asubuhi na mapema.

Nimemkuta kalala kitandani kanipa mgongo.
Nikamtolea salaam.

''Nani mwenzangu?''
''Mimi Mohamed wa Popo.''

Jibu lake lilinifurahisha nikatabasamu.
Mzee Waikela alinijibu, ''Maarufu.''

Babu yangu Salum Abdallah Popo walifungwa wote Jela ya Uyui kizuizini mwaka wa 1964 baada ya maasi ya Tanganyika Rifles.

Babu yangu na Mzee Waikela walikuwa wote ndani ya TANU wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

''Alitokea Chanjagaa akajenga nyumba akakaa,
mwanangu Mwanasiti kijino kama chikichi,
Cha kujengea vikuta na vilango vya kupita.

Hapo zamani za kale...''

1712261469266.png

Ally Kleist Sykes
(1926 - 2013)
1712261518199.png

Bilali Rehani Waikela
(1932 - 2022)​
 
Mwanangu Mwana Siti Kijino kama Chikichi.

old is gold.

Jungu Kuu Halikosi Ukoko.

Heko.
 
Mzee wangu, kwanini majina hayo yaliogopwa kutajwa hadharani yakiunganishwa pamoja na Mwalimu Nyerere?
Nifah,
Uhuru wa Tanganyika mwaka wa 1961 ulikuja na changamoto nyingi na kubwa katika hizo ni mchango wa Waislam kama jamii maalum iliyokuwa.mstari wa mbele katika kupigania uhuru.

Ghafla Uislam ukawa nyeti katika historia ya uhuru.

Naamini ikiwa umefuatilia makala zangu utakuwa umesoma najina mengi ambayo hayamo katika historia rasmi.
 
Back
Top Bottom