Kakke
JF-Expert Member
- Dec 4, 2010
- 1,883
- 1,482
Mwanasheria wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Othuman Masoud, ametupilia mbali hoja ya mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Christopher Ole Sendeka, la kutaka hati ya Muungano kutoonyeshwa hadharani, badala yake iwe siri.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Sendeka kupinga hoja ya John Mnyika ambaye alitaka kanuni ziweke wazi upatikanaji wa nyaraka mbalimbali za kitaifa ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa hati ya maridhiano ya Muungano.
Baada ya Mnyika kutoa hoja hiyo, Sendeka alipinga pendekezo hilo kutaka ufafanuzi wa kisheria kutoka kwa Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda kuhusu kanuni za Bunge hilo kama kweli ni sahihi hati ya Muungano kuwekwa wazi.
Masoud alisema hakuna tatizo lolote la upatikanaji wa hati ya Muungano kwani hati hiyo ni wazi kwa Watanzania wote.
"Labda kama mjumbe (Sendeka) anazungumzia hati nyingine ambayo si ya Muungano wa Tanzania, lakini kama ni Muungano huu ambao mimi naujua, sioni kama kuna tatizo lolote ambalo linazuia kupatikana kwa hati hiyo na kuisoma kwa hati hiyo ni taarifa ya wazi kwa Watanzania wote," alisema.
CHANZO: NIPASHE