Mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) Fredrick Parsayo, amefariki dunia ghafla leo Ijumaa, Machi 21, akiwa nyumbani kwake Kinoo, Eneo Bunge la Kikuyu. Kwa mujibu wa taarifa ya KBC, Parsayo amefariki katika mazingira ya kutatanisha kwani alikua mzima na hakulalamika kuumwa popote. Jana baada ya kutoka kazini alielekea nyumbani kwake huko Kinoo, umbali wa kilomita 15 kutoka Nairobi lakini leo hakuripoti kazini asubuhi tofauti na ilivyo kawaida yake.
Baada ya kupiga simu yake na kutopokelewa ndipo jitihada za kumfuata nyumbani zilipofanyika, ambapo walielezwa na majirani kuwa tangu aingie ndani jana usiku hakutoka. Jitihada za kuvunja mlango zilipofanyika Parsayo amekutwa ameaga dunia kitandani kwake.
Serikali imetangaza kuanza uchunguzi mara moja ili kubaini chanzo cha kifo cha mwandishi huyo kijana aliyeanza kuwa mashuhuri katika tasnia ya habari nchini humo. Mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya St.Theresa kaunti ya Kiambuu.
Parsayo alikuwa Mwandishi na mmoja wa timu ya uhariri ya KBC ambaye alijiunga na shirika hilo mwaka wa 2021 mara baada ya kukamilisha masomo yake katika Chuo Kikuu cha Nairobi.Kifo chake kinaongeza sintofahamu katika tasnia ya habari nchini Kenya baada ya mwandishi wa zamani wa NTV Rita Tinina kufariki mwaka jana katika mazingira yanayofanana na Parsayo.
Tinina aliondoka kazini tar.08 March 2024 na alikuwa amepangwa kusoma taarifa ya habari ya saa 7 mchana tar.09 March 2024. Hata hivyo muda ulipokaribia hakuonekana kazini na alipopigiwa hakupokea. Jitihada za kumfuata nyumbani kwake zilifanyika lakini walikuta amejifungia kwenye appartment aliyokua akiishi huko Brooklyn Springs, Kileleshwa, Nairobi.
Baada ya kuvunja mlango ndipo wakakuta amefariki dunia kitandani kwake. Serikali ilianza uchunguzi mara moja, na juzi March 19, 2025 Pathologist Mkuu wa Serikali ya Kenya Dr.Peter Ndegwa ametoa ripoti ya uchunguzi ikionesha kuwa Tinnina alifariki kwa changamoto za mapafu.
Ikiwa ni siku moja tu toka ripoti ya kifo cha Tinina itoke, hatimaye Mwandishi mwingine Fredrick Parsayo amekufa katika mazingira yaleyale na kipindi kilekile cha mwaka (mwezi March). Je ni coincidence au kuna kitu kinaendelea?