Tanzania yaongoza nchi za Afrika Mashariki kuvutia uwekezaji
in
images,
Latest,
News and Events /
Imeelezwa kuwa Tanzania imeshika nafasi ya kwanza katika nchi zinazovutia uwekezaji katika nchi za Afrika Mashariki na kushika nafasi ya tisa barani Afrika.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Australia kwa nchi za Afrika Mashariki, Mhe.Geoff Tooth wakati akihitimisha Maonesho ya Kimataifa ya Madini yaliyofanyika Perth, Australia yajulikanayo kama Africa Down Under (ADUC) ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa fursa kwa nchi za kiafrika zenye utajiri wa madini ikiwemo Tanzania kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya madini ili kuvutia wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Balozi Tooth alitumia fursa hiyo kuiasa Tanzania kuendeleza juhudi za kuvutia uwekezaji nchini kwa kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kuwa na mundombinu madhubuti ya barabara, bandari, reli, kuboresha upatikanaji wa umeme na kuwa na sera na sheria zisizobadilika mara kwa mara.
Ujumbe wa Tanzania uliohudhuria Maonesho ya Kimataifa ya Madini, katika mji wa Perth nchini Australia, ukiwa mbele ya banda la Tanzania lililokuwa linatumiwa na wataalam wa Tanania katika kutoa elimu kwa wageni zaidi ya 2000 waliohudhuria maonesho hayo. Ujumbe huo uliongozwa na Naibu Katibu mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eng. Ngosi Mwihava,(wa saba kutoka kulia). Wengine katika picha ni Mkuu wa mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo (wa nne kutoka kushoto mstari wa mbele), Kamishna wa Madini Eng.Paul Masanja (wa sita kulia), Mtendaji Mkuu wa TMAA, Eng.Dominic Rwekaza (wa pili kulia), Kamishna Msaidizi Madini-Uchumi na Biashara, Salim Salim (wa tatu kulia), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Prof. Abdulkarim Mruma (wa tano kulia), Kaimu Mkurugenzi wa Kazidata (Database) (GST), Bi Yorkbeth Myumbilwa (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Utawala wa Fedha na Utawala (TMAA), Bruno Mteta (wa tatu kushoto mstari wa mbele), Meneja Masoko na Mahusiano kwa Umma , STAMICO , Koleta Njelekela (wa kwanza kulia) na wataalam wengine kutoka Wizara na Taasisi zake.
Akizungumzia kuhusu mafanikio ya ushiriki wa Tanzania Katika maonesho hayo ya siku tatu yaliyoshirikisha nchi mbalimbali duniani, Kamishna wa Madini, Wizara ya Nishati na Madini, Eng. Paul Masanja ameeleza kuwa Tanzania ilipata upendeleo wa kipekee katika maonesho hayo kwani mnamo tarehe 4 Septemba mwaka huu, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Eng Ngosi Mwihava alipata nafasi ya kutoa mada mahsusi kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya madini hapa nchini.
Aliongeza kuwa, tarehe 5 Septemba mwaka huu, Tanzania ilipangiwa muda maalum wa kueleza kwa undani kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya madini nchini (Tanzania Investment Forum), pamoja na kukutana ana kwa ana na wawekezaji wenye nia ya kuja kuwekeza nchini.
“Kupitia fursa hiyo, Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava, ulipata fursa ya kueleza masuala mbalimbali ikiwemo historia ya Tanzania, maendeleo ya sekta ya madini, vivutio mbalimbali vya uwekezaji, pamoja na miradi ambayo inaweza kuendelezwa kwa ubia kati ya wawekezaji hao na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)”. Alieleza Kamishna.
Mbali na kupata muda maalum wa kutoa mada katika mikutano iliyokuwa ikienda sambamba na maonesho hayo, Kamishna wa Madini ameeleza kuwa, wataalam katika banda la Tanzania, walikuwa wakitoa elimu na taarifa mbalimbali ikiwemo sera ya madini ya mwaka 2009, sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo, madini yapatikanayo Tanzania, tafiti za kijiolojia na mashapo yaliyopo Tanzania, pamoja na huduma za kijiolojia zinazotolewa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST).
“Watalaam wetu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, GST, STAMICO, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) pia walikuwa wakitangaza miradi ambayo STAMICO inahitaji wawekezaji wenza, walitangaza shughuli za maabara ya kisasa ya TMAA, taarifa mpya za kijiolojia zilizokusanywa na GST, walikutana ana kwa ana na wawekezaji kwa maana ya kupata ufahamu zaidi kuhusu masoko na mitaji na vilevile walipata fursa ya kujifunza jinsi nchi nyingine za kiafrika zinavyosimamia sekta ya madini”. Alisisitiza Mhandisi Masanja.
Maonesho hayo ya Kimataifa ya ADUC yaliyoanzishwa rasmi mwaka 2003, yalikutanisha zaidi ya washiriki 2000 kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri wa Madini kutoka baadhi ya nchi za Kiafrika na Australia, maafisa waandamizi wa madini wa nchi hizo, wataalam kutoka taasisi za fedha duniani, wawekezaji, na watoa huduma kwenye sekta ya madini.
Pamoja na Tanzania, nchi nyingine zilizoshiriki maonesho hayo ni pamoja na Angola, Botswana, Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Comoro, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Gabon, Ghana, Guinea-Conakry, Kenya, Lesotho, Malawi, Madagascar, Msumbiji, Namibia, Niger, Nigeria, Rwanda, Jamhuri ya Afrika Kusini, Sudan, Uganda na Zimbabwe.
Imeandaliwa na: Teresia Mhagama,
Afisa Habari, Wizara ya Nishati na Madini, 754/33 Mtaa wa Samora, S.L.P 2000 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7,
Nukushi:+255-22-2121606
Barua Pepe: info@mem.go.tz Tovuti: www.mem.go.tz